Operesheni Sangara yamtikisa Malecela
na Joseph Senga na Janeth Josiah, Dodoma
MIKUTANO ya Operesheni Sangara inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Dodoma, jana ilitikisa nyumbani kwa Mbunge wa Jimbo la Mtera, John Samuel Malecela, katika kijiji cha Mvumi Misheni baada ya wapambe wake kuingiwa kiwewe kwa kutaka kuzuia mkutano huo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wapambe wa mbunge huyo, walilazimika kuita timu za mpira wa miguu kucheza kwenye uwanja huo kwa lengo la kuzuia mkutano huku wakijiandaa kufanya fujo ambazo hazikufanikiwa.
Katika hali ya kuonyesha kuchanganyikiwa, wafuasi hao waliamua kucheza soka kuanzia saa 8 mchana mpaka saa 11 jioni kabla ya kukatizwa na helikopta inayotumiwa na Mbowe kutua uwanjani hapo na wao kulazimika kukimbia.
Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Freeman Mbowe, alieleza kusikitishwa kwake na siasa za chuki zinazopandikizwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Ndugu zangu wananchi wa Mvumi Misheni hakuna sababu ya kugombana kwa sababu ya vyama vya siasa, tugombane kwa mustakabali wa maisha ya watoto wetu, msikubali watu kupandikiza chuki… nimefika hapa na kuelezwa kwamba kuna watu walitaka kuzuia mkutano usifanyike …hizi ni chuki ambazo hazitakiwi wala kukubalika.
Alisema muda wa Malecela kung'atuka ama kuachia ngazi umefika kutokana na kukalia kiti cha ubunge miaka mingi bila kulisaidia jimbo ambalo wakazi wake ni maskini wa kutupwa.
"Huyu amekuwa mkuu wa mkoa, waziri, waziri mkuu na makamu wa pili wa rais, makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, tangu nikiwa mdogo namsikia mpaka sasa… jamani ana jipya gani la kuwaeleza wakati hata barabara hakuna hapa Mvumi Misheni?" alisema Mbowe.
Mwenyekiiti huyo pia aliwatahadharisha wananchi wa jimbo la Mtera kutoendelea kuikumbatia CCM wakati imeshindwa kuwaletea maendeleo husasan kwa kuendelea kumchagua Malecela kwa kipindi kirefu namna hiyo; jambo ambalo limekuwa likidumaza maendeleo yao kila kukicha.
Alisema kwamba mkoa wa Dodoma ni mkoa wa pili kwa umaskini Tanzania ukiondoa Shinyanga; hali liyosababishwa na wananchi wa Dodoma kuichagua CCM.
"Tunahitaji kumpumzisha Malecela maana hata mwenyezi Mungu alifanya kazi kwa siku sita ya saba akampumzika kwa nini Malecela asipumzike?"aliuliza Mbowe.
Pia aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuondoa woga hasa kutokana na kutishwa na viongozi wa serikali ya CCM na kwamba CHADEMA ndiyo chama mbadala ambacho kitaweza kuwakomboa wananchi wa mkoa huo katika lindi la umaskini.
"Kuendelea na CCM ni sawasawa na kuendeleza utawala wa kisultani kwa maana sultan anatawala mpaka kufa kwake na kisha kumrithisha mtu anayemtaka yeye jambo ambalo kamwe haliwezi kuleta maendeleo kwa wananchi," alisema Mbowe.
Wakionyesha mwitikio, wananchi wa Mvumi Misheni walimuomba Mbowe aendelee kuhutubia hata kama ni usiku wa manane kutokana na sera alizokuwa akizinadi kwao.
Aidha, wananchi hao walitoa kilio kuhusu kero zao mbalimbali kwa mwenyekiti huyo; ikiwemo kuuziwa chakula kilichotolewa kama msaada na viongozi wa serikali ya kijiji kwa sh 1,250 na kwamba malalamiko hayo yamefikishwa kwa mbunge wao mpaka sasa hakuna ufumbuzi uliopatikana.
Operesheni Sangara imeingia mkoani hapa kwa siku kumi na tatu ikizunguka majimbo na kata zote za mkoa huo kwa lengo la kuwahasisha wananchi kuchagua viongozi na vyama mbadala. Ikiwa siku ya tatu, jana operesheni hiyo iliingia katika jimbo la Mtera na kufanya mikutano zaidi ya 12. Leo operesheni hiyo itaendelea katika jimbo la Kondoa Kusini ambapo viongozi wandaamizi wa chama hicho, akiwemo Makamu Mwenyekiti, Said Arfi, na Katibu Mkuu, Wilbrod Slaa, wanatarajia kuongeza nguvu.