THIRD EYE CHAKRA (AJNA):
CHAKRA YA SITA. CHAKRA YA JICHO LA TATU
THIRD EYE CHAKRA, pia ikijulikana kama Ajna, au Chakra ya Jicho la Tatu kwa Kiswahili, ni chakra ya sita katika mfumo wa chakra saba za msingi. Iko katikati ya paji la uso, sambamba na katikati ya macho, na inahusishwa na kipengele cha Mwanga cha asili. Chakra hii inahusishwa pia na hisia, ufahamu, na uangavu wa kiakili.
Chakra ya jicho la tatu ni lango la mifumo ya juu ya ufahamu, na inadhaniwa kuwa ni chanzo cha hekima yetu ya ndani. Wakati chakra hii iko sawa na wazi, tunaweza kuufikia ufahamu wetu wa ndani na hisia yetu ya ndani, ikituruhusu kufanya maamuzi kulingana na mwongozo wetu wa kiroho, badala ya akili yetu ya kimantiki. Tunaweza pia kupata uzoefu wa maono, uwezo wa kuona mambo nje ya ulimwengu huu.
Ajna inahusishwa na hisia ya kuona, kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha kuwa macho yetu yana afya. Kumtembelea daktari wa macho mara kwa mara, kupumzika vya kutosha, na kupunguza kukutana na mwanga wa buluu vyote vinaweza kusaidia kuyaweka macho yetu ya kimwili katika hali ifaayo.
Chakra ya jicho la tatu inahusishwa pia na rangi ya nili na mafuta muhimu ya ubani, mrujuani na msandali. Nili ni rangi ya buluu iliyoiva yaani kati ya buluu na zambarau. Tahajudi, kuandika, na kushikamana na asili au ulimwengu, kunaweza pia kusaidia kufungua na kuiweka sawa chakra ya jicho la tatu.
Chakra ya ajna inawakilishwa na sayari ya Zohali (au "Saturn"). Inawakilishwa pia na vito kama vile yakuti ya buluu ("blue sapphire"), amethisto ("amethyst"), na tanzanaiti ("tanzanite"). Siku yake ya juma ni Jumamosi, na ina nguvu ya kiume na kike au "ying" na "yang" kama ilivyo chakra ya koo.
Kuvaa vito vya yakuti, amethisto au tanzanaiti kwenye mikufu, pete au bangili, kutasaidia sana kufunguka kwa chakra ya jicho la tatu. Kwani mawimbi ya nguvu ya sumaku-umeme kutoka katika vito hivyo huendana na mawimbi ya nguvu ya sumaku-umeme ya chakra ya jicho la tatu, kiasi cha kuipa chakra hiyo nguvu kubwa ya kufunguka na kufanya kazi vizuri.
Tahajudi, yoga, na kutoa sauti ya "AUM" (iitwayo "beej mantra") kwa muda mrefu mara kwa mara, kunaweza pia kusaidia sana kuifungua na kuiweka sawa chakra ya jicho la tatu.
Josè Silva, mwandishi wa kitabu kiitwacho "Mind Control Method', anasema kuwa ikiwa mtu anataka kuijua na kuidhibiti dunia yake ya ndani hana budi kujifunza jinsi ya kutumia jicho la tatu ipasavyo. Anasema kuwa mbinu nzuri zaidi ya kufungua jicho la tatu ni kutafuta kwanza sehemu iliyotulia, hususan usiku kabla ya kulala.
Kisha fumba macho yako ya kimwili. Vuta pumzi nyingi na kuitoa taratibu mara tatu au zaidi, kutuliza fikra zako nyingi. Kisha, ukiwa bado umefumba macho, geuza macho yako kana kwamba unaangalia juu kwenye paji la uso. Utahisi shinikizo fulani katikati ya paji la uso. Shinikizo hilo ndiyo nishati yenyewe ya jicho la tatu, na hadi hapo jicho la tatu linakuwa limeshaanza kufunguka kwa ajili yako.
Kama anavyosema Quazi Johir, mhamasishaji wa jicho la tatu katika tovuti ya YouTube, unachotakiwa kufanya baada ya hapo ni kuhakikisha kifikra kuwa unaona mwanga wa buluu mbele ya paji lako la uso. Katikati ya mwanga huo, hakikisha unaona namba 333, kisha chini yake 222, kisha chini yake tena 111, ili akili yako iende sasa katika hatua ya "alpha" ya ubongo wako. Ukishaona "111" maana yake ni kwamba umeshaingia katika hatua ya "alpha" ya ubongo wako, na sasa uko tayari kufokasi katika jambo unalolitaka.
Kwa mujibu wa Johir, katika hatua hiyo ya "alpha" fikiria tatizo lako! Kisha kifikra lipeleke tatizo hilo moyoni, na lifanye kuwa jambo linalokusumbua sana. Baada ya hapo hesabu kimoyomoyo tatu hadi moja, kisha (kifikra hivyohivyo) lirushe tatizo hilo kwa nguvu hadi juu kabisa ya kichwa chako (ambako sasa ni mbinguni). Ukifanya hivyo, shida yako tayari umeshamkabidhi Mwenyezi Mungu aishughulikie na si kazi yako tena kuifikiria.
Fikiria sasa suluhisho la tatizo lako. Kama ulivyofikiria tatizo, fikiria suluhisho hivyohivyo. Ukiwa bado uko kwenye hatua ya "alpha", lione jawabu la tatizo lako moyoni. Lifanye jawabu hilo kuwa kubwa sana moyoni mwako. Yaani, jione unafurahia sana kupata suluhisho la tatizo lako.
Kisha, baada ya kuhesabu tatu hadi moja, lishike lile tatizo na kulirusha kwa nguvu hadi nje kabisa ya kichwa chako (yaani mbinguni kwa Mungu Baba). Quazi Johir anasema, baada ya hapo shida yako imekwisha. Subiri siku tatu, kama bado hujapata jawabu, rudia tena; ila fanya hivyo kila baada ya siku tatu hadi jawabu lipatikane.
Chakra ya jicho la tatu inatuwezesha kuitazama dunia yetu ya ndani, wakati macho ya kimwili yanatuwezesha kuitazama ya nje. Dunia ya nje ni kivuli tu cha dunia ya ndani. Umewahi kusikia watu wakisema "Dunia hii ni 'illussion'"? Maana yake ni kwamba dunia hii ni kivuli na dunia halisi ni ya ndani.
Ni sawa na kusimama kando ya kioo. Wewe ni dunia ya ndani, kivuli chako upande wa pili wa kioo ni dunia ya nje—hii inayoita "illussion". Ukitaka kubadili dunia yako ya nje lazima ubadili dunia yako ya ndani kwanza, kwa sababu kivuli hakiwezi kubadilika chenyewe. Na hutaweza kufanya hivyo bila nsaada wa chakra ya jicho la tatu.
Kwa kuifungua na kuiweka sawa chakra ya jicho la tatu, tunaweza kuufikia ufahamu wetu wa ndani; hivyo kuturuhusu kufanya maamuzi yenye hekima na busara. Tunaweza pia kuonja uzoefu wa mifumo ya juu ya ufahamu, kupata uangavu juu ya kusudi la maisha yetu, na kushikamana na Mungu wetu wa mbinguni.
View attachment 2622223
—Enock Maregesi, mwanafalsafa na mwandishi wa vitabu