Hili tangazo la William Malecela na reactions kutoka kwa wasomaji wake, vimenifanya nipeleleze kidogo ili kubaini kulikoni huko New York.
Nimebahatika kuchimba na kuyapata ya New York. Endapo ni ya uzushi tu, basi yatupilieni mbali. Lakini kama yana bifu yeyote kuhusu NY (na, pengine, kwenye jumuia nyingine za wa-Tanzania ughaibuni), inafaa sana kujizatiti katika kukabiliana na virusi vya mgawanyiko wa u-siasa, u-kabila na u-dini ili kuweza kujenga jumuia hizo kuwa chimbuko la utamaduni wa m-Tanzania, ughaibuni; kuliko kumeremeta ki-vyama vya siasa, kiu-kabila na/au ki-u-dini.
Enzi za Balozi wetu (wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa) mmoja kulikuwepo na tetesi kuwa Mwalimu Nyerere alifikiria kuteua ma-Balozi waliokuwa wanachama tu wa CCM. Huo ulikuwa ni wakati wa Chama Kushika Hatamu (Vanguard Party).
Walikuwepo wa-Tanzania waliokuwa wakifanya kazi kwenye Sekretariati ya Umoja wa Mataifa waliokuwa wanategemewa kwamba huenda Mwalimu Nyerere angewakumbuka na kuwazawadi na wadhifa wa kuwa ma-Balozi.
Baadhi ya wa-Tanzania hao walikuwa ni wazee: Dixon Nkembo na Asanterabi Nsilo Swai. Lakini wengine walikuwa bado vijana-jana: Remi Michael Tiruhungwa, Bernard E. Muganda, Leo Msuya, Joseph Kotta, C.S.M. Mselle, Ismat Steiner na Fortunatus Lwanyatika Masha. Kuna tetesi kuwa baadhi yao walitafuta nafasi ya kuteuliwa kuwa ma-Balozi.
Hii haina maana kuwa kila mmoja wa hao wa-Tanzania alikuwa akiota kuwa Balozi siku moja; la hasha! Kwani wengine walikuwa wameishatengwa na TANU/CCM.
Waliofikiria kuwa huenda Mwalimu Nyerere angewakumbuka, walikimbia kimbia kuanzisha Tawi la CCM hapo New York kupitia Ofisi ya u-Balozi!
Na kweli Tawi hilo lilifunguliwa. Mwenyekiti wake alikuwa ni Mzee Dixon Nkembo. Mlezi wa tawi alikuwa ni Balozi. Lakini waliokuwa mbele kuanzisha Tawi hilo walisubiri bila Mwalimu Nyerere kuwakumbuka kuwa ma-Balozi. Njozi ya Tawi la CCM ikaishiwa mafuta; likafa!
Kundi lingine la wa-Tanzania wa NY lilikuwa ni la graduate wanafunzi wakisoma hapo New York University na Columbia University, ambao hawakupenda sana kuwa wanachama kwani walikuwa huko NY kwa muda tu. Uanachama wao ulibakia hapa hapa Tanzania.
Baadaye, likaja wimbi la vijana: Watoto wa ma-Balozi na watoto wa vigogo na wakubwa kutoka Bongoland na kutua sehemu za Mt. Vernon. Wengine waliahama Tanzania kabisa na kumwacha baba yao huko Tanzania na kuanzisha nyumba yao mpya hapo Mt. Vernon ingawa baba yao huwa anakuja kuwatembelea.
Watoto wa ma-Balozi (waliobaki huko Amerika wakati wazazi wanamaliza muda wao na kurudi nyumbani au wengine kubadili kazi na kujiunga na Sekretariati ya Umoja wa Mataifa) na wa vigogo na wakubwa kutoka Bongoland walipenda kujumuka kwa kufanya parties zaidi kuliko kufikiria kuunda Umoja wa Jumuiya ya wa-Tanzania.
Kutokana na kundi hili kukutana kutana kwa ajili ya parties, walijitokeza vijana wengine wenye kutaka kuunda Umoja wa Jumuiya ya wa-Tanzania wa kudumu. Kwahiyo, kila mara walipokutana, suala la kutaka kuunda Chama cha wa-Tanzania huwa linaibuka na kutongoza akili zao.
Wa-Tanzania wengine huwa wanajiweka mbele mbele kutekeleza lengo hili la kuunda Chama cha wa-Tanzania kutokana na kuwa karibu karibu na Balozi, kupitia tabia ya ki-mtandao ya u-dini au u-kabila na/au vyote viwili.
Ya NY yanasisimua kweli! Balozi akiwa m-Islamu, wa-Islamu wengi wanajitokeza kutoka kila mahali NYC na vitongoji vyake. Hii ilikuwa wazi sana wakati wa enzi za ma-Balozi wa-Islamu. Kuna wakati mmoja nyumba ya Balozi ilikuwa kama Msikiti siku ya Ijumaa.
Wenye kujua hayo majambo wanaeleza kuwa kulikuwepo na wakati m-tanzania mmoja (nasikia kuwa sasa ni Alhaj) na kijana mwingine wa kutoka sehemu za Boston (nasikia ana cheo cha Maalim) walijifanya kama kiungo cha wa-Tanzania hapo NY, ikiwa ni pamoja na William Malecela kuwa, pia, mbele, kama Community Organiser wa wa-Tanzania.
Habari hizo zinaelezea kuwa huyo wa Boston bado anavinjari vinjari NY kwa sababu ma-Balozi wawili waliofuatana wanatoka sehemu za kwao. Sijui kama NY ikipata Balozi mpya asiyetoka sehemu za kwao, huyo Boston ataendelea kufunga safari za kila mara kwenda NY!
Lakini ya NY yana harufu mbaya ya ubaguzi baguzi. Balozi akiwa m-Kristu, hivyo hivyo tena. Kuna Balozi m-Kristo mmoja, ambaye alipata kusoma huko huko New York aliunda mtandao wake na ma-rafiki walioselea na kuishi NY miaka mingi.
Wakati wa enzi za Balozi niliyemtaja paragrafu ya tatu mtandao wake ulivuka mipaka hadi Uingereza, ambako kulikuwa na kundi kubwa la wa-Arabu waliokimbia Zanzibar.
Kuna habari za kuaminika zenye kueleza kuwa baadhi ya wa-Arabu hao wa Uingereza walikuwa wakitumia Ofisi ya u-Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa katika kupata pasi mpya au kubadilisha zile zilizoishia muda wake. Badala ya kutumia Ofisi ya u-balozi wetu mjini London, walipendelea kupeleka pasi zao mjini New York!
Zaidi, kuna pia habari kuwa kulikuwa na binti wa ki-Sukuma aliyepata mchumba mzungu, m-Diplomasia wa Australia. Binti huyo alikuwa akiishi kwa muda nyumbani kwa m-Pemba wa kutokea sehemu za Mwanza, rafiki wa Balozi huyo hapo Kurasini karibu na Bendera Tatu. Mchumba wake huyo alikuwa ahamishiwe huko Papua New Guinea. Huyo binti alitafuta pasi ya Tanzania bila kufanikiwa. Lakini alifanikiwa kupata pasi kutoka kwa Balozi huyo huyo iliyoandikwa huko New York!
Balozi huyo alipalilia sana mahali pa uzawa, ikiwa ni pamoja na kupendelea wa-Arabu wa Tanzania waliokimbilia huko Ulaya. Kwani kuna ukweli kuwa hao wa-Arabu wengine walikuwa hawabadilishi pasi zao huko waliko. Pasi zao zilikuwa zililetwa New York na kubadilishwa ikiwa ni pamoja na mpya kutolewa!
Wengi sana walimpenda Balozi huyo. Na wakati wa hafla walijazana hapo nyumbani 30 Overhill Road, MT. Vernon, NY 10552. Mtindo huo wa kuwaalika wa-Tanzania hapo nyumbani aliuendeleza Balozi m-Kristo, niliyemtaja hapo awali.
Kuna habari za kusisimua kwamba wakati wa enzi za balozi huyo wa-tanzania walicheza dansi hapo nyumbani wakikanyaga hayo mazulia na kukalia hivyo viti mpaka vikachoka. Washiriki wengine walipata breakfast hapo kuliko pengine kuendesha magari yao kurudi majumbani kwao na huku wamelewa chakari! That was a good idea!
Halafu alikuja Balozi m-Islamu mwingine. Hakuna aliyekanyaga hapo nyumbani. Balozi huyo alifuatiwa na ma-Balozi wengine wawili waliokuwa wa-Kristo, ambao walifungua mlango wa nyumba hiyo nyumba tena kwa wa-Tanzania, kupitia kwa vijana wao kujumuka na vijana wenzao kwa parties kwenye basement yake tu. Na wakati mwingine kukita hema hapo kwenye uwanja wa nyumba hiyo ya Balozi.