KATIKA moja ya taarifa zetu za leo tumeripoti kuhusu baadhi ya kinamama wanaojifungua katika zahanati za wilayani Same mkoani Kilimanjaro, kurudi nyumbani na taka za uzazi.
Kama wadau wa uzazi salama taarifa hizi zimetuchoma na kutuumiza. Hili jambo ambalo kwa namna yoyote linaleta fedheha na halikubaliki kwa taifa na jamii inayojua thamani ya uzazi na jukumu la mwanamke katika uzazi wa watoto.
Tunaona kuwa hatua hiyo ni kinyume na haki za binadamu na utu wa mwanamke ambao unaweza kufananishwa na udhalilishaji usio na kifani. Kama taifa haipendezi mama kujifungua na kurudi nyumbani akiwa amefungashiwa mfuko au nyumba ya mtoto (kondo la nyuma), lakini pia bila kuoga wala kufua nguo zilizotumika wakati wa kumpata mtoto, kisa hakuna maji.
Suala hili lililoripotiwa na vituo vya Taarifa na Maarifa vya Kata za Lugulu linadokeza kuwa tatizo la maji katika hospitali hizo limekuwa sugu.
Aidha, inasemekana kuwa kinamama wanaojifungua katika zahanati hiyo wanatakiwa kwenda na majini wodini. Hii ni ajabu na jambo la kizamani. Lakini, taarifa zetu zinaeleza kuwa hakuna tanuru la kuchomea taka hizo, wala shimo la kutupa taka mbichi za uzazi hasa nyumba ya mtoto pindi mjamzito anapojifungua.
Inasikitisha zaidi inapoelezwa kuwa huwalazimu kinamama hao kufungashiwa taka hizo na kurudi nazo nyumbani wakatupe wenyewe.
Habari hizi ni za kusikitisha mno na kukatisha tamaa kinamama na wadau wa uzazi salama. Tunaomba juhudi za lazima zifanywe ili kuwasaidia kinamama hawa ambao ndiyo wanaozaa wapigakura, walipa kodi na taifa letu.
Tunaona kuwa si jambo jema kwa sababu kuna mambo mengi mengine yanayoelezwa ambayo nayo hushusha heshima ya mwanamke. Inashuka zaidi kwani kuna habari zinazosema katika zahanati hizo hakuna eneo la kujifungulia na wanawake hao hulazimika kujifungulia kwenye chumba cha sindano ama eneo la kufunga vidonda.
Tunaiomba serikali ifanye utafiti na kuchukua hatua. Haitoshi kusema kuwa kinamama wanajifungua bure na kuhudumiwa bila gharama wakati wanapokwenda kujifungua, huku tena kuna madai kuwa baadhi ya zahanati za nchi yetu hazina wodi za wazazi wala maji ya kuoga baada ya kujifungua.
Tunaomba suala hilo lipewe uzito maalumu kwa kuwa pengine si Wilaya ya Same pekee, inawezekana sehemu nyingine za nchi yetu kuna tatizo hilo na pengine kubwa zaidi. Inawezekana shida hiyo haipo vijijini hata mijini pia. Ndiyo maana tunaomba utafiti wa kina na wa haraka ufanyike ili kupata ufumbuzi.
Tunashukuru kuwa serikali inafanya jitihada nyingi za kusaidia uzazi salama, kutoa chanjo kwa watoto na kupunguza idadi ya vifo vya wanawake na watoto, lakini bila kujali huduma muhimu kama maji kwenye chumba cha uzazi juhudi hizo zinaweza kukwama.
Tunapenda kusisitiza kuwa jitihada hizo zinapata doa iwapo wanawake wataachwa kurudi nyumbani na taka mbichi za uzazi kutokana na ukosefu wa maji.
Hali hiyo inaongeza mashaka kwa sababu ni rahisi kuwa na maji kuliko kuwa na wataalamu wa kushughulikia dharura za wajawazito. Aidha, kama ni vigumu kujenga tanuru la kuchoma taka za uzazi itawezekana kuwa na wabobezi wa kuwasaidia matatizo yakitokea?
Tunapenda kukumbusha wanawake wanaweza kususia kujifungulia hospitalini ikiwa wanakutana na changamoto kama hizo.
Tunarudia tena kuiomba serikali ifanye juu chini kuchunguza na kufahamu ukubwa wa tatizo hilo kitaifa na kurekebisha kasoro hiyo ili kuwanusuru kinamama na aibu hiyo na kurejesha heshima na utu wa mwanamke.
Chanzo: Nipashe