KERO Changamoto Sugu ya Ukatishaji Maji na Ucheleweshaji wa Matengenezo Mlandizi (Pwani): Tunaomba Majibu Kutoka DAWASA

KERO Changamoto Sugu ya Ukatishaji Maji na Ucheleweshaji wa Matengenezo Mlandizi (Pwani): Tunaomba Majibu Kutoka DAWASA

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Ndugu zangu wa JamiiForums Wasalaam,

Naleta mada hii mbele yenu nikiwa kama mkazi wa eneo la Kata ya Mlandizi mkoani Pwani. Lengo langu kuu ni kuomba hifadhi ya utambulisho wangu (Anonymous), lakini pia kutumia jukwaa hili adhimu kufikisha kilio chetu kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Kuna changamoto sugu ya upatikanaji wa maji katika eneo letu la Msufini ambayo sasa inadumu kwa zaidi ya miezi miwili (2) mfululizo bila utatuzi wa kudumu.

Hali halisi ya ratiba ya maji ilivyo sasa:

A. Siku za Katikati ya Wiki: Maji yamekuwa yakikatwa kila siku ifikapo saa 1 au 2:00 usiku, na kufunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi au wakati mwingine hadi saa 6:00 mchana wa siku inayofuata kama hivi leo.

B. Siku za Wikiendi: Hali huwa mbaya zaidi; kwa mfano, siku za Jumamosi maji yamekuwa yakikatika kwa siku nzima.

Juhudi zilizofanyika na Mifano ya Changamoto za Kiutendaji:

1. Kufuatilia: Kama mwananchi mtiifu, nimeshafuatilia na kupiga simu katika ofisi za mamlaka husika kwa zaidi ya mara ishirini (20) kutoa taarifa na kulalamikia changamoto hii ya kukatika kwa maji. Cha kusikitisha ni kwamba, hadi sasa hakuna majibu ya kuridhisha wala ufumbuzi wowote uliochukuliwa.

2. Ucheleweshaji wa matengenezo (Mtaa wa Kilimanjaro). Ili kuonyesha jinsi ufuatiliaji unavyokuwa mgumu, mnamo mwezi wa February, 2026 nilipita njiani Mtaa wa Kilimanjaro na kukuta bomba kubwa likivuja maji.

Niliripoti changamoto hiyo mara mbili (2) mfululizo. Cha kushangaza, maji yaliendelea kupotea hovyo kwa wiki mbili nzima. Nilipofuatilia tena, niliambiwa na mamlaka kuwa "tatizo limeshafanyiwa kazi", wakati uhalisia ulikuwa bado maji yanavuja! Ilinilazimu kupaza sauti tena kwa nguvu ndipo mafundi walipokuja kufanya matengenezo.

Wito wangu:
1. Kuna tatizo gani la kiufundi linalosababisha mgao huu usio rasmi na wa muda mrefu katika eneo la Msufini?

2. Mfumo wa usimamizi wa dharura na matengenezo ya mabomba yanayovuja (kama ilivyotokea mtaa wa Kilimanjaro) una shida gani hadi uchukue wiki mbili na kutoa majibu yasiyo ya kweli?

3. Ni lini suluhisho la kudumu litapatikana ili wananchi wapate huduma stahiki na endelevu?

Nawasilisha, nikiomba ushirikiano wenu.

Namba ambazo nimekuwa nikizitumia kuwasilisha kero zangu: 118, 0800110064, 0734130133 & +255222194800.
 
Back
Top Bottom