ASILI YA UGOMVI WA EDWARD LOWASSA NA SAMUEL SITTA
MWAKA 1995, ilianza misheni ya kumshawishi Dk Salim Ahmed Salim, aachane na ukatibu mkuu wa OAU, arejee kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM.
Misheni hiyo ilipofeli, wazee, Mwalimu Nyerere na Mzee Rukhsa, walimketisha Jakaya, wakamshawishi achukue fomu. Jakaya akawa anasita. Hakujiamini.
Mtu wa mipango, Edward Lowassa, aliusoma mchezo, akaupa tafsiri chanya. Akampa somo kaka mkubwa, Samuel Sitta. Ikawa timu. Edward na Sitta, wakamwendea Jakaya. Wakamshawishi achukue fomu.
Tofauti na ushawishi wa wazee kwa Jakaya, safari hii Edward na Sitta, walibeba ramani ya upacha. Jakaya na Edward waingie ulingoni kama mapacha. Ambaye angekwama njiani, angemsaidia mwenzake ashinde. Sitta akawa meneja kampeni.
Edward na Sitta, walimhakikishia Jakaya kuwa wangemfanyia kila kitu. Jakaya alikuwa Waziri wa Fedha. Alitingwa na maandalizi ya bajeti ya Serikali 1995-1996. Edward na Sitta, walizungusha fomu ya Jakaya nchi nzima, ikapata wadhamini. Jakaya akiwa zake ofisini, Dar.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ndoa ya kisiasa ya Jakaya na Edward. Sitta ni mhusika muhimu. Watu hao watatu, jumlisha Rostam Aziz, aliyeingia baadaye, ndiyo vichwa vikuu vya mtandao ulioshinda kiti cha urais mwaka 2005. Jakaya akaingia Ikulu.
Ajabu, miaka mwili baada ya ushindi wao, walivurugana. Moto uliwaka bungeni. Edward alitoswa uwaziri mkuu kupitia "ajali" ya Richmond, Sitta akiwa Spika wa Bunge.
Edward akasema: "Tatizo ni uwaziri mkuu."
Eti, Sitta alimwonea kijicho Edward kuwa waziri mkuu. Kwa nini na walikuwa timu moja?
Jibu ni hili; wanamtandao walikuwa desperate kuhakikisha Jakaya anashinda urais 2005. Mizungu mingi ilichezwa kupitia kanuni: "Sema Chochote, Kubali Chochote, Ahidi Chochote, Chafua Yeyote, Mradi Jakaya awe Rais."
Kanuni hiyo ndiyo asili ya mgogoro wa Edward na Sitta. Wote waliahidiwa uwaziri mkuu. Edward akapata, Sitta akatakiwa awe Spika wa Bunge.