Hivi sasa China imekumbwa na wimbi jipya la janga la COVID-19, hususan huko Shanghai, ambapo kesi za maambukizi ya virusi ni nyingi. Ili kulinda maisha ya watu, China imechukua hatua mbalimbali madhubuti. Lakini kwa mara nyingine tena, Marekani imejitokeza na kuishutumu China, ikisema mwitikio wa kupita kiasi wa China utaathiri mwitikio “sahihi” dhidi ya virusi vya Corona duniani. Pia utaathiri utulivu wa mnyororo wa ugavu duniani, na ufukukaji wa uchumi wa dunia ambao umeathiriwa na mgogoro kati ya Russia na Ukraine.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imetoa shutuma moja baada ya nyingine dhidi ya China, ikiegemea sauti yake ya juu na uungaji mkono wa wenza wake wa magharibi. Machoni mwao, chochote kinachofanywa na China ni makosa, na chochote Marekani inachofanya ni sahihi. Huu ni mtazamo wa umwamba!
Katika zaidi ya miaka miwili iliyopita, China ikiwa nchi ya kwanza kuathiriwa na janga la COVID-19, ilichukua hatua madhubuti na kwa wakati ili kupunguza athari za janga hilo kwa maisha ya watu, na maendeleo ya uchumi, na kupata mafanikio makubwa.
Ingawa China ina idadi kubwa ya watu, lakini kesi za maambukizi ya virusi vya Corona na vifo kutokana na virusi hivyo ni chache sana. Hata hivyo, katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19, kutoka mwanzo, China iliwahimiza watu kuvaa barakoa, wale wenye virusi kujitenga nyumbani, na baaadye iliwaweka watu walioingia nchini China kutoka nchi za nje karantini, karibu hatua hizo zote zilikosolewa na kupingwa na Marekani. Lakini jambo linaloshangaza zaidi ni kwamba, mwishowe Marekani ilifuata hatua hizi moja baada ya nyingine, ili kukabilianana hali mbaya ya maambukizi. Mwaka jana, Marekani ilijitangaza kuwa nchi yenye mafanikio zaidi katika kupambana na janga la COVID-19, bila kujali zaidi ya Wamarekani milioni moja wamefariki kutokana na janga hilo. Mwishowe, idadi ya waliofariki kutokana na virusi hivyo iliposhika nafasi ya kwanza duniani, ilijitangaza kuwa nchi yenye mafanikio makubwa zaidi duniani katika kupambana na janga hilo.
Kuhusu China, bila shaka imewekwa nyuma katika orodha hii ya Marekani ya nchi zilizofanikiwa kukabiliana na janga la COVID-19.
Shutuma za Marekani dhidi ya China sio tu katika suala la janga la COVID-19. China ilitoa sheria ya usalama wa kitaifa mjini Hong Kong ili kuzuia ghasia za kuvuruga Hong Kong na kuifarakanisha China, na ikalaumiwa na Marekani kuwa hiki ni kitendo cha kuangamiza demokrasia. China ilianzisha vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi huko Xinjiang, ili kuondoa umaskini ambao ni mzizi wa ugaidi, pia hatua hiyo ililaaniwa na Marekani kwa madai kuwa inawakandamiza Wauyghur, na hata ni mauaji ya kimbari.
Ikiwa ni moja kati ya vyanzo vya mgogoro kati ya Russia na Ukraine, Marekani ilikosoa China kwa kutoiunga mkono kupinga Russia.
Kuhusu uhusiano kati ya China na Afrika, Marekani haijawahi kuacha kupaka matope uhusiano huo. Marekani na nchi nyingine za magharibi kununua mafuta na madini barani Afrika ni biashara ya kunufaishana, lakini China ikifanya hivyo basi ni ukoloni mamboleo.
Mikopo ya Marekani kwa nchi za Afrika ni kwa ajili ya kuzisaidia nchi hizo kupata maendeleo, lakini wakati China inatoa mikopo kwa Afrika kujenga miundombinu na kuboresha maisha ya watu, huu unaitwa mtego wa madeni. Awali Marekani ililimbikiza dozi nyingi za chanjo ya COVID-19 kuliko mahitaji, na kukataa kuzitoa kwa Afrika, ikishutumu China kufanya “diplomasia ya chanjo”, kwani China ilisambaza chanjo hiyo barani Afrika sambamba na matumizi ya ndani.
Katika miaka ya hivi karibuni, maendeleo ya kasi ya China yameleta wasiwasi mkubwa kwa Marekani. Kwa kufuata umwamba na siasa ya kinguvu, Marekani inatumia kila fursa kuipaka matope China, na kuipinga China kwa pande zote, ili kuzuia maendeleo yake. Hata hivyo, vitendo hivyo vya kiubinafsi na kuchekesha havitafanikiwa daima dawama.