Kwa zaidi ya miongo miwili, sera ya China kwa Afrika ilijikita zaidi katika maendeleo na miundombinu. Lakini sasa imepanua mawanda yake na kuingia ndani zaidi hadi kwenye utamaduni na lugha, ikitumia njia ya kukikuza na kukieneza Kiswahili ili kujenga ukaribu zaidi na wenzao wa nchi za Afrika Mashariki zinazozungumza lugha hii.
Mwezi Machi mwaka 2023, Rais Xi Jinping alipendekeza Mpango wa Ustaarabu wa Dunia (GCI) ili kukuza heshima kwa ustaarabu tofauti duniani, ambapo ustaarabu huu unaonekana kwenye mambo mbalimbali ya utamaduni yakiwemo chakula, lugha, mavazi n.k.
Mbali na lugha nyingine za Afrika zinazofunzwa hapa China, Kiswahili imekuwa lugha inayozidi kujibebea umaarufu mkubwa kwa sasa. Hivi karibuni tamthilia mpya ya Kichina inayoitwa “Karibu Katika Kijiji cha Milele” ilioneshwa hapa nchini na kupata mwitikio mzuri sana.
Tamthilia hii inasimulia hadithi ya wafanyakazi wa matibabu wa China waliokwenda kuokoa maisha na kujenga urafiki wa kina na wenyeji wao wa barani Afrika. Kabla ya kufunga safari kwenda kusaidia kutibu watu wa Afrika, madaktari na wafanyakazi wa matibabu wanafunzwa lugha hii adhimu ya Kiswahili ili watakapofika huko wasipate tabu sana kwenye masuala ya kuwasiliana.
Kinachovutia zaidi kwenye tamthilia hii ni kwamba mwalimu anayewafunza Wachina Kiswahili pia ni Mchina. Hii inathibitisha kwamba walimu wa Kiswahili ambao ni Wachina wamebobea kwenye lugha hii.
Imekuwa ni kawaida ya China kutuma vikundi ama timu za madaktari barani Afrika kwenda kusaidia kutoa huduma za matibabu, na kufanikiwa kutibu magonjwa mbalimbali, ambapo hadi leo wenyeji wa nchi hizo wanaishukuru na hawataisahau China kwa msaada wake kwa watu hao.
Ni nadra sana kuona tamthilia za Kichina zikitumia lugha za Afrika, mara nyingi imezoeleka kuonekana tamthilia hizi zikitumia lugha ya Kiingereza ama za Ulaya. Hii ni mara ya kwanza kutumika maneno mengi ya Kiswahili kwenye tamthilia ya Kichina, jambo ambalo linaonesha kwamba sasa China imedhamiria kwelikweli kuwa pamoja na kushirikiana na wenzake wa Afrika.
Kuna sababu zinazoifanya China ijikite kwenye Kiswahili, na hii ni kutokana na kwamba Wachina wanafahamu kwa kina historia ya lugha hii. Kiswahili ni lugha ambayo baharia, mvumbuzi, mwanadiplomasia na kiongozi wa misafara ya majahazi ya China, Zheng He (1371-1433), alikutana nayo wakati wa safari zake saba za Kenya na Ukanda mpana wa Pwani ya Waswahili. Kwa sasa, Kiswahili ambacho kimsingi ni lugha ya Kibantu yenye athari mbalimbali za Kiasia, kimeibuka kuwa lugha kuu ya diplomasia.
Ikiwa mojawapo ya lugha zinazokuwa kwa kasi zaidi na yenye wazungumzaji zaidi ya milioni 200 katika zaidi ya nchi 14, Kiswahili kimeingia kwenye orodha ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani. Pia Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi zinazotumika kwenye Umoja wa Afrika (AU). Mwaka 2021, mnamo mwezi Novemba, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliipa heshima lugha ya Kiswahili kwa kutangaza rasmi kwamba kila ifikapo tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni siku ya Kiswahili duniani.
Toleo la Kiswahili la kitabu cha “Utawala wa China” cha rais Xi Jinping, pia linakuja kama kichocheo kingine cha lugha hii kujivunia nafasi yake muhimu kwa Wachina na pia inajivunia kuwa miongoni mwa lugha kuu za kimataifa. Hii ni juzuu ya kwanza ya mfululizo wa juzuu nne, kikiwa na mkusanyiko wa hotuba na maagizo mbalimbali ya Rais Xi Jinping katika vipindi mbalimbali tangu awe Rais wa China.
Wakati mwaka huu China na Tanzania zinaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi, kauli mbiu ikiwa ni “Mwaka wa utamaduni na utalii”, ni matarajio ya kila mdau wa Kiswahili kwamba mbali na kazi hii ya China ya kukitangaza Kiswahili nje ya mipaka ya nchi zinazozungumza lugha hii kupitia kwenye tamthilia yake ya “Karibu Katika Kijiji cha Milele”, pia kutakuwa na shughuli nyingi sana za kukuza lugha hii.