China yaweka Sheria kuzuia Mahusiano ya Kimapenzi kati ya AI na binadamu

China yaweka Sheria kuzuia Mahusiano ya Kimapenzi kati ya AI na binadamu

Richer

JF-Expert Member
Joined
Jun 9, 2025
Posts
2,318
Reaction score
4,079
Julai 15, 2026, China ilianza kutekeleza sheria kali zaidi duniani zinazobana roboti za mazungumzo za akili Unde (AI) zinazojifanya kama wanadamu, lengo likiwa ni kuzuia watu kuzizoea kupita kiasi kihisia na kulinda afya ya akili ya jamii.

Serikali ya China imeweka sheria hizo nzito ili kuzuia teknolojia ya akili unde (AI) kuchukua nafasi ya mahusiano halisi ya kibinadamu, pamoja na kukabiliana na changamoto kubwa za kijamii kama vile kuporomoka kwa kiwango cha uzazi na vijana kujitenga na jamii.

Sheria hizi zinazilenga kampuni zote zinazotengeneza mifumo ya AI na roboti za wahusika wa kufikirika nchini humo, huku zikiwaathiri mamilioni ya watumiaji—khususan vijana na watoto.

Chini ya kanuni hizi mpya, watoto walio chini ya miaka 18 wamepigwa marufuku kabisa kuwa na wapenzi au mahusiano ya karibu ya kipekee na AI, huku walio chini ya miaka 14 wakihitaji idhini ya wazazi kutumia wasaidizi wa AI. Kwa watu wakubwa, huduma hizo zimewekewa mipaka mikali: AI inatakiwa kutoa taarifa kila baada ya saa mbili kuwakumbusha muda waliokaa mtandaoni, na vipengele vinavyosababisha uzoefu wa kupindukia au mawazo ya kujidhuru vimepigwa marufuku.

Kampuni zitakazokiuka zinakabiliwa na faini ya hadi yuan 200,000 (sawa na Pauni 22,000 za Uingereza) au kufedheheshwa hadharani na serikali, hatua iliyozifanya kampuni kubwa kama Alibaba na ByteDance kufunga vipengele vya urafiki kwenye AI zao kabla hata sheria haijaanza kufanya kazi.

Hali ilikuaje awali?
Kabla ya kanuni hizi kuanza kutumika, matumizi ya AI za Mahusiano na urafiki nchini China yalikuwa makubwa sana.

Kulingana na kampuni ya utafiti wa masoko ya Sensor Tower, kuna takribani watumiaji milioni 128 wanaotumia programu za AI za mahusiano kila mwezi nje ya China. Nchini China pekee, makadirio mengi yanaonyesha idadi hiyo iko kati ya milioni 29 hadi 70.

Sheria mpya za China zinazilenga programu zilizotengenezwa mahususi kuwa marafiki, wapenzi wa kiume au wa kike wa AI; lakini pia zinahusu mfumo wowote mkubwa wa lugha (LLM) unaoiga jinsi mwanadamu anavyozungumza na kutangamana.

Hatua hii imeleta simanzi na hasira miongoni mwa watumiaji waliopoteza 'rafiki' zao wa AI, huku ikionyesha pia jitihada za serikali za kuwalinda wananchi dhidi ya teknolojia zenye ushawishi mbaya na wakati huo huo kuongeza udhibiti wa maisha yao ya binafsi.



Source: BBC
 
Back
Top Bottom