Mazingira ya choo kwa ajili ya Abiria kwa Wanawake katika Kivuko upande wa Magogoni hayana privacy’ na pia kuna muda hakuna usalama kwa watumiaji hasa wakati wa Usiku.
Kero ya kwanza, wakati wa mchana abiria wanapokuwa hapo wakisubiri usafiri, watu wanakaa hadi karibu na mlango wa kuingia kwenye choo hicho.
Hivi unaingiaje chooni na watu wamekaa hadi mlangoni, unadhani utakuwa na utulivu humo ndani utakapoingia?
Soma Pia: Hali ya Choo cha MV KOME II ni hatari kwa afya na usalama wa Watumiaji
Kero nyingine ni kuwa ukiingia ndani hakuna maji, ukiyahitaji unalazimika kutoka nje, unachota kwenye kikopo hapo nje ambapo wamekaa watu wengine, kisha unaingia na kikopo chako kufanya yako.
Jambo lingine ambalo hili naomba lifanyiwe kazi haraka ni kuhusu usalama wa watumiaji hasa majira ya usiku.
Wanawake wanaoingia kwenye choo hicho wanaweza kuvamiwa kwa wahalifu wanaowasubiri eneo hilo wakati wa kuingia au kutoka kisha wakishafanya yao wanakimbilia maeneo ya baharini.
Matukio hayo yametokea mara kadhaa, hivyo kuna ulazima wa kuimarisha ulinzi lakini pia kutengeneza mazingira bora ya watu kutumia.