SoC02 CHUNGU LAKINI DAWA; Tathmini ya uwajibikaji katika jicho la makosa ya kijamii

SoC02 CHUNGU LAKINI DAWA; Tathmini ya uwajibikaji katika jicho la makosa ya kijamii

Stories of Change - 2022 Competition

MutuMuandishi

New Member
Joined
Sep 8, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Ni matamanio ya kufuta alama za nyayo zinazoiendea njia ya uhasama, ni kiu ya kuiangamiza shari, ni msukumo wa kipekee nafsini mwa mtu, ni majuto yanayoleta nia ya kujenga daraja badala ya ukuta- msamaha. Hasa msamaha mbele ya hadhara. Mnamo mwaka 2010, Kampuni ya usafirishaji kwa njia ya reli nchini Ufaransa iliomba radhi mbele ya umma kwa kujihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu wakati wa harakati za wanazi.

Mwaka 2019, Reinhold Hanning, aliyewahi kuwa mlinzi kwenye kambi ya watumwa ya Auschwitz, alionesha kujutia kutochukuwa hatua dhidi ya vitendo viovu vilivyofanyika kambini humo. Mwaka 1992, Raisi mstaafu wa Afrika kusini, Hayati Nelson Mandela alikiri uwepo wa vitendo vya kikatili katika magereza ya ANC- chama kilichokuwa chini ya uongozi wake.

Ni kweli usiopingika kuwa kuomba radhi ni sehemu ya uwajibikaji. Kwa yule aliyekosewa, awe mtu mmoja au jamii, kuombwa msamaha kunamfanya ahisi maumivu yake yameonekana na kutiliwa maanani. Kwa sababu hii, pengine anaweza kubadilisha mtazamo wake,kumtoa yule aliyekosa kutoka kwenye orodha ya waovu na kumvusha mpaka kwenye orodha ya watu wema. Lakini je, vipi kuhusu athari zilizotokana na vitendo viovu vya mtenda dhidi ya mtendwa? Hili ndilo pengo lililopo kati ya msamaha na uwajibikaji.

Niruhusu nikupeleke katika ulimwengu wa kufikirika ambao kila mmoja anawajibika kwa matendo yake. Katika ulimwengu huu, mwalimu akimuadhibu mwanafunzi kwa makosa ambayo siyo yake, basi pindi tu anapogundua hilo, humuita yule mwanafunzi na kumuomba radhi. Lakini haishii hapo tu, huenda mbali zaidi, na kushirikiana na mwanafunzi yule ( labda na baadhi ya walimu na wanafunzi wengine pia) kutengeneza mfumo utakaowezesha kutambua kosa ni la nani hasa kabla ya kutoa adhabu. Huu ndio uwajibikaji.

Tafadhali nikurejeshe tena kwenye ulimwengu wetu ambao tunaizima roho ya uwajibikaji kwa misemo kama 'Mkubwa hakosei '. Hata katika ngazi za chini kabisa za kijamii, mfano familia, imekuwa ni kawaida kujificha chini ya kivuli cha utamaduni ili kuepuka kuwajibika kwa baadhi ya makosa tunayowatendea wengine. Ni kwanini hasa tunajitia upofu na uziwi pale linapokuja swala la kuwajibika?

Moja kati ya sababu kubwa ni mazoea ya kujiona bora kuliko wengine. Kuendekeza hali hii humfanya mtu ajione ana mamlaka juu ya mitazamo, mawazo au maisha ya watu wengine kiujumla. Mtu wa namna hii huamini kabisa kuwa ana haki ya kutowajibika kwa matendo yoyote anayowatendea wengine.

Vile vile kutokutaka kuwajibika kunaweza kusababishwa na hali ya maumivu ambayo mtu aliwahi kupitia kipindi cha nyuma cha maisha yake mfano ; kukataliwa au ukatili wa namna yoyote ile. Mambo haya yanaweza kumfanya mtu aendelee kujiona mwathirika siku zote kiasi cha kutozingatia makosa yake na maumivu anayosababisha kwa wengine kwenye maisha yake ya sasa.

Aibu na majuto pia ni moja ya sababu inayoweza kumfanya mtu asitake kuwajibika
. Hasa mtu huyo anapokuwa na hofu kubwa ya kuwavunja moyo na kuwatia simanzi watu wanaomuamini au kumuheshimu. Huu ni mzigo mzito kihisia unaoweza kufanya mtu huyu kujitenga kabisa na jamii ya watu hao pale anapofanya makosa.

Jambo lingine linalofanya mtu akwepe kuwajibika ni kutokuwa na utayari wa kubadilisha mienendo na tabia yake yenye kuleta madhara hasi kwa mtu au watu wengine. Mara nyingi hii hutokana na kiburi cha fikra ama kutojiamini.

Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazomfanya mtu achukuwe uamuzi wa kutokuwajibika.

Tumekuwa tukiendekeza tabia ya kuamua kutenda mambo bila kuyapima kwenye mzani wa faida na hasara. Pengine ni kwa sababu tunataka sana kuyatenda mambo haya na hivyo tunaogopa tukitekeleza hatua hii muhimu mzani utaelemea upande wa harasa, jambo ambalo litatushinikiza kusitisha hayo tuliyotaka kuyafanya. Tukipima maamuzi ya kutokuwajibika katika mzani huu, ni hakika upande wa faida hautokuwa na uzito wowote ule. Kutokuwajibika kwa makosa kuna madhara makubwa mno yenye hakika ya kuutingisha uhusiano wa mtenda na mtendwa.

Tumaini, ama la kurejesha uhusiano mzuri uliokuwepo baina ya mtenda na mtendwa kabla ya kosa kutendeka, au kujenga uhusiano mzuri baina ya mtenda na mtendwa baada ya kosa kutendeka, huyeyuka kadri muda unavyoenda ikiwa mtenda hatawajibika kwa makosa yake. Kitendo ambacho kinaweza kuleta uhasama si tu kwa wao, bali hata vizazi vyao au wafuasi wao.

Si hivyo tu, kutowajibika kunamfanya mtenda kutokukua kifikra na pia kitabia. Kwasababu bila kuwajibika mtenda hana namna nyingine ya kushuhudia mabadiliko chanya ambayo yangeletwa (kwake na kwa mtendwa) kwa kitendo cha yeye kukiri makosa, kuomba radhi na kuchukua hatua za kurekebisha yale aliyokosea.

Inatupasa kama jamii, kutokuchukulia kuwajibika kama ni adhabu, bali kitendo cha utu na uungwana, chenye kujenga na kurejesha heshima. Tuwe wepesi wa kutambua makosa yetu,na kuwa na utayari wa kubeba jukumu la kutengeneza tulipoharibu.

Haya yanawezekana ikiwa kwa pamoja tutashirikiana kuja na mbinu za kujenga utamaduni wa kupenda ama kuwa wepesi linapokuja suala la uwajibikaji. Mifano ya mbinu hizi inaweza kujumuisha uenezaji wa elimu ya uwajibikaji na faida zake katika vituo vya elimu, kutengeneza maudhui ya picha mnato na picha mjongeo ya elimu hii kisha kuyaeneza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kujumuisha wadau mbalimbali pamoja na viongozi ili kuhamasisha uwajibikaji katika jamii.

Vile vile, tunapokuja upande wa pili wa sarafu ambao ni kuwajibishwa, tunapaswa kuja na mkakati imara ambao utahakikisha kuwa mtenda haishii tu kuomba radhi, bali pia kuziba pengo lililopa kati ya msamaha na uwajibikaji kwa kupatiwa majukumu ambayo moja kwa moja yatamfanya awe mstari wa mbele kukemea uovu wa aina ile aliyoufanya, na kupaza sauti yake, kwa maneno na matendo ili kutetea maslahi ya aina ya waathirika wanaotokana na vitendo hivyo viovu.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom