Baadhi ya watu huamini hamna tiba ya chunusi ila dawa huzipunguza tu. Je ulisha wahi kuwa na chunusi zikaisha kabisa? Tuambie ulifanyaje tufaidike pamoja.
Chunusi zina dawa zake na zinapona kabisa. Tatizo kubwa ni kwamba wahanga wengi wanahangaika kutokomeza vipele badala ya chanzo cha chunusi zenyewe. Sababu kuu za chunusi ni kama nne:
1. Kuzidi au kubadilikabadilika kwa kiasi cha homoni za uzazi (Hii ndo hujumuisha na zile chunusi za kubalehe)
2. Matumizi ya kemikali kali usoni (Vipodozi visivyo salama kama vile Carotone, Perfect white, Extra Clair, Caro light nk)
3. Mafuta mengi usoni na uchafu kunakoweza kuzuia baadhi ya matundu ya kutokea mafuta
4. Maambukizi ya bakteria wanaosababisha chunusi (Propionibacterium acnes)
Sasa ukitaka kutibu chunusi moja kwa moja ni lazima kutumia dawa na vipodozi vitakavyokabiliana na visababishi hapo juu, ambapo mara nyingi huwa ni zaidi ya kimoja. Huwezi kutumia losheni tu kisha ukapona chunusi, na huwezi kutibu chunusi kwa kutumia dawa au kipodozi ambacho hakikabiliani na chanzo cha chunusi husika.
MATIBABU YA CHUNUSI
Kwenye matibabu ya chunusi kitu cha kwanza kabisa kutambua ni ya kwamba chunusi huweza kuwa ugonjwa kama magonjwa mengine. Ni vyema zaidi kwenda hospitali au kliniki (hata kama zimetokana na mkorogo) kwa ajili ya ushauri na matibabu maana dawa zote za chunusi ni zile za kuandikiwa na daktari (Prescription Only Medicines/POM).
Ili kutibu chunusi inabidi ufanye au ufanyiwe uchunguzi ili kujua nini kimesababisha na/au kuchochea chunusi zako
1. Kuzidi au kubadilikabadilika kwa kiasi cha homoni za uzazi ?
2. Vipodozi ?
3. Mafuta mengi usoni na uchafu ?
4. Maambukizi ya bakteria ?
Mara nyingi chunusi husababishwa na kuchochewa na sababu zaidi ya moja kati ya hizo, hivyo na matibabu yake huhitaji mchanganyiko wa dawa na vipodozi mbalimbali.
A. Mafuta mengi usoni na uchafu
Haya unaweza kuyadhibiti kwa kutumia poda na sabuni zake. Mifano ni Poda ya Pond's iliyoandikwa Oil Control, Sabuni ya Protex iliyoandikwa Deep Clean, Sabuni ya Pears iliyoandikwa Oil Clear nk. Pia punguza kiasi cha mafuta kwenye vyakula na epuka vyakula vyenye mafuta mengi
B. Kuzidi au kubadilikabadilika kwa homoni
Kama ndo unabalehe basi pata matibabu endelevu maana homoni huwa juu kwa muda kiash umri ukisogea utarudi katika hali ya kawaida na chunusi zitaisha. Kama ni mtu mzima pata matibabu yatakayosaidia kuweka homoni zako sawa kisha utadhibiti vizuri chunusi zilizojitokeza
C. Vipodozi vikali/visivyo salama
Kama unaamini dawa ya moto ni moto basi hapa hicho kitu hakipo. Huwezi ukapata chunusi kutokana na matumizi ya krimu fulani halafu uweze kuzitibu kwa kutumia carotone, maxi tone, maxi white, perfect white, mekako nk.
Kwa urahisi na usalama zaidi anza kuacha vipodozi vilivyokuletea chunusi na usipake chochote, hususan kemikali kali, hadi utakapopata ushauri wa mtaalam wa ngozi
D. Maambukizi ya bakteria
Haya ndiyo huwacost wengi maelfu kwa malaki bila kupona. Huwezi kutibu chunusi zilizotokana na maambukizi ya bakteria kwa kutumia losheni au krimu ambayo haina dawa ya kuua bakteria. Zinaweza kupungua tu lakini haziwezi kuisha.
Pata ushauri wa mtaalam wa ngozi na matibabu ya kuondoa bakteria hawa kisha baada ya hapo utapona kabisa.
Zingatia mambo yafuatayo:
1. Usipasue chunusi
Kupasua chunusi ndiko hukuachia makovu na madoa, ambayo ndiyo magumu kuondoka kuliko chunusi zenyewe
2. Safisha uso wako vizuri, mara kwa mara
Tumia sabuni zenye uwezo mzuri wa kuondoa vijidudu na uchafu. Usitumie sabuni kali
3. Usitumie vipodozi vinavyochubua
Epuka vipodozi vya kung'arisha au kuchubua ngozi. Vitakuongezea hasara nyingi zaidi kuliko faida
Kwa elimu na ushauri zaidi tafadhali "like" ukurasa wetu wa facebook (AFYA ZAIDI Consultants) na/au tembelea website yetu