Mtumishi wa Bwana89
JF-Expert Member
- Jul 23, 2018
- 3,191
- 4,220
Huyo Babu msimpe majeraha
Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Bado unamaumivuSIAMINI kabisa kama mpango wa Clatous Chota Chama kutoka Simba kwenda Young Africans una baraka za kocha Miguel Gamondi. Naamini hii ni mipango ya siasa zetu za kuoneshana ubabe, kuoneshana uwezo na kukerana.
Nikifuatilia suala hili naona mtazamo wa mashabiki wengi wa Simba ukibadilika kwa kasi ya ajabu. Walianza kutoa maneno makali kupinga kwamba Triple C asingeondoka Simba. Sasa naona wengi wanatoa kauli za kusisitiza mchezaji huyo aende tu, inawezekana kwa kukata tamaa au vinginevyo. Hii inaonesha kuwa jambo la kukerana linapoteza nguvu kwani waliokusudiwa kukereka wameanza kuonesha hawakereki.
Inawezekana nguvu kubwa ya kumtaka Chama Young Africans zaidi ni ya kupata faida nyingine na wala si mchango wa mchezaji huyo kwa timu. Kuna faida za kibiashara ya jezi, watu kulipa na kufurika uwanjani siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi na pia viongozi wa Young Africans kuongeza hali ya kupendwa na kuaminiwa na mashabiki lakini kiuchezaji, siioni ofisi ya Triple C Young Africans ikizingatiwa kocha Gamondi mwenye msimamo mkali na asiyeingiliwa na uongozi, tayari ameshawagawia ofisi wachezaji wake alionao sasa na tayari wanatia mzigo vizuri kulingana na falsafa ya uchezaji wa Young Africans.
Palipo na Muddathir Yahya, Pacome Zouzoua, Max Nzengeli na Stephen Ki Aziz ukimtaja pia Khalid Aucho unahitaji nini zaidi? Nani miongoni mwa hawa ajiunge na Salum Abubakar Salum, Zawadi Mauya na Shekhan Khamis ukimtaja pia Jonas Mkude kukaa bench ili Mwamba wa Lusaka apate ofisi ya kudumu Young Africans?
Hoja itatolewa kuwa timu kubwa huwa na wachezaji bora wengi wa nafasi moja ili kuifanya timu iwe imara nyakati zote kwa kutokosa mchezaji mzuri mabadiliko yakifanywa, dharura mbalimbali zikitokea na kukabili mashindano mengi. Kutekeleza hilo palihitajika, kwa pesa inayohusu biashara ya Clatous Chota Chama, angetafutwa mjuzi mno, mwenye kasi iendayo na falsafa ya uchezaji wa Young Africans atakayedumu kwa misimu kadhaa au atakayeuzwa kwa faida kubwa lakini kuingia gharama kubwa hivyo kwa Chama aliyevuka umri wa miaka 30 kulipaswa kufanyiwa tafakari ya kina.
Tunaambiwa timu hununua wachezaji wajuzi wa umri mkubwa kufanikisha malengo ya muda mfupi lakini Young Africans wameshafika fainali Afrika, wamefika robo fainali Afrika na wamechukua ubingwa wa Tanzania Bara mara tatu mfululizo na CRDB Shirikisho. Siamini wanahitaji mchezaji wa umri mkubwa wa uchezaji wa taratibu wa Chama kufanikisha lolote la sasa. Akili yao ilipaswa, kwa kutumia pesa ya kumpata Chama, iwaelekeze kufukua sehemu mbalimbali Afrika na kumpata mchezaji kijana mwenye kasi kama ilivyotokea kwa Ki Aziz ili awasaidie kwa mengi kwa muda mrefu.
Nionavyo kama Young Africans itafanikiwa kumpata Triple C kutoka Simba, Simba watanufaika zaidi ya Young Africans. Hii ni kwa sababu Simba walishampa mchezaji huyo ofisi ya kudumu na alikuwa mfalme. Hawakuwa wakifikiri kutafuta wachezaji wengine bora wa nafasi yake kutokana na ufalme waliompa. Ninachoona kwa sasa ni kama Simba watakuwa wameondolewa mzigo huo na hivyo watatafuta wachezaji wajuzi wa umri wa miaka 20 na kadhaa kuikamata ofisi hiyo. Kwa ufalme wake, Simba wasingempa 'Thank You' kirahisi kama walivyofanya kwa wengine. Pia wasingefanya hivyo kukwepa lawama kutoka kwa mashabiki wao kwani walijua 'Thank You' yao ya hapo Kariakoo ingepokelewa mara moja na 'Welcome' ya upande mwingine wa hapo hapo Kariakoo.
Kwa upande wake, Chama, atakuwa amefaulu kufanikisha kupata pesa kubwa ya malipo ya kusaini mkataba na mshahara mkubwa wa mwezi. Kwa hayo anastahili pongezi kwani hayo ni maisha yake na kila mtu ana maisha yake kipekee. Mwamba wa Lusaka anajua vizuri kuliko sisi wengine kwamba ajira ya soka ni ya muda mfupi kuliko ajira zote. Hivyo ukipata fursa ya kukusanya pesa nyingi kwa muda fulani mfupi ndani ya kazi ya soka, usiitupe fursa hiyo.
Kwa Young Africans, wao watafanikisha malengo yoyote mengine lakini mchango wa mchezaji huyo kwao naamini hautakuwa mkubwa. Ataingia ofisi ya nani? Max? Pacome? Ki Aziz? Muddathir? Au atapewa jukumu jipya? Je atachangamka kuendana na uchangamfu wa Young Africans?
Simba watateseka kwa kuzomewa na kubezwa lakini watakuwa wamepata fursa ya kuingiza vipaji vipya ndani ya ofisi ya Mwamba wa Lusaka. Kwa uhakika mwamba huyo ana ofisi ya uhakika Simba lakini hana uhakika wa ofisi Young Africans. Akifanikiwa kwenda huko, utabaki wajibu wake kupambana kuishi kama mchezaji wa Young Africans akienda na mapigo ya muziki wao.
Vyovyote atakavyoamua kuhusu wapi afanye kazi msimu huu, uamuzi wa mchezaji huyo unapaswa uheshimiwe kwani atakuwa ameamua atakavyoamua kwa kujali maisha yake na si maisha yetu sisi wengine. Kila mtu ana maisha yake na anapanga afanye yapi kuyafanya yampe furaha, amani na afya nzuri. Tumuache Triple C na maisha yake.
Baada ya utumishi wake wa mkataba atakaoingia sasa kokote kule hapo Kariakoo, ni vizuri aweke mkakati kichwani wa kurudi nyumbani Zambia kwenda kumalizia huko kucheza soka. Kwake kufanya kazi Tanzania kutakuwa kumetosha. Ameishi muda mrefu kama mfalme asimalize kama mtu wa kawaida huko Singida Black Stars au Coastal Union. Tuheshimu uamuzi wowote wa sasa hivi wa Mwamba wa Lusaka.
---UZI HUU, NIMEUTOA FACEBOOK, UMEANDIKWA NA BW. IBRAHIM MKAMBA.
Nimevutiwa kuuleta huku, baada ya 'kufikiri' kuwa una VIWANGO vya hapa JF.