Tanzania yaanza vibaya Madola
SAFARI ya Tanzania kusaka medali kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola nchini India imeanza vibaya baada ya wanamichezo wake wa kuogelea kutolewa mapema.
Akizungumza na Mwananchi kutoka New Delhi, mkuu wa msafara wa Tanzania, Juliana Yasoda alisema wamepoteza medali katika michezo ya kuogelea na mpira wa meza.
Waliotolewa ni Mariam Foum, mwogeleaji wa mita 50, freestyle ambaye pia hushiriki mita 50 alishika nafasi ya nne, hivyo kutolewa.
Mwanadada huyo alishika nafasi ya sita katika kuogelea mtindo wa breast- stroke huku medali za kwanza zikitarajiwa kuanza kutoka siku ya kwanza ya michezo hiyo jana.
Tanzania, pia ilifungwa na Ghana katika mpira wa meza, ambako mashindano yanafanyika kwa mtindo wa ligi na hivyo kuondolewa, leo watakamilisha ratiba kwa kucheza na Malyasia.
Wakati huo huo, mwanariadha aliyetemwa kwenye kikosi kinachoshiriki michezo hiyo, Zakia Mrisho amesema kuwa anasikitika kushindwa kushiriki katika mashindano hayo makubwa.
Zakia aliyetemwa katika kikosi hicho aliiambia Mwananchi kuwa alitegemea kushiriki mashindano hayo, lakini alipofika nchini aliambiwa hakuna tiketi iliyoachwa kwa ajili yake kwenda India kuungana na wenzake.
"Nina uchungu kuikosa michuano hiyo, ni kweli nilikuwa Italia nikikabiliwa na mashindano ya klabu yangu ambayo ndiyo imekuwa ikinidhamini katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
"Baada ya mashindano hayo nilirudi nchini Septemba 27 siku moja baada ya wenzangu kuondoka , lakini nikaambiwa sina tiketi ya kuniwezesha kufika huku kuungana na wenzangu, imeniuma, " alisema Zakia.
Kabla ya wanamichezo kuondoka nchini kwenda India, serikali ilisema kuwa mchezaji yoyote atakayechelewa kurejea nchini kuungana na wenzake kabla ya kwenda India na hatimaye kukuta wenzake tayari wameondoka, atakuwa amejiengua mwenyewe kutoka mashindano hayo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo alisema kuwa mwanamichezo yoyote atakayeshindwa kurejea nchini wakati timu inaondoka atakuwa amejiondoa.
source: mwananchi
Kweli huu ni uozo...