Jubilee inalenga kutumia kadi mpya kuiba kura - Amani
CHAMA cha Amani (ANC) kimedai kwamba kadi mpya zinazotumiwa kuwasajili wanachama wa Jubilee Party (JP) ni njama ya kisiri ya kuongeza idadi ya wapigakura katika ngome za chama hicho.
Aidha, kilisema kuwa kadi hizo zimeunganishwa kisiri na mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bodi ya Kitaifaya Usajili wa Watu (NRB) na Afisi ya Msajili wa Vyama vya kisiasa hali ambayo inatumika kisiri kuandaa mikakati ya wizi wa kura.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi Alhamisi, mwenyekiti wa chama hicho Bw Godfrey Osotsi alisema kuwa wana ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa matatizo ya usajili sawa wa vitambulisho unahusiana na uunganishaji wa kadi hizo na mitandao hiyo.
“Si siri kuwa hizi ni njama za wizi kwani uzinduzi wa kadi hizo ulikujia siku chache kabla ya kuanza kwa mchakato wa wapigakura.
Tumeshitikiana na kundi la wataalamu wetu ambapo tumegundua kwamba wanaopewa kadi hizo wanaweza kuingilia mitandao ya asasi hizo, hivyo kuiweka katika hatari ya kudukuliwa,” akasema Bw Osotsi.
Kwa hayo, alisema kuwa lazima usajili wa wanachama kupitia kadi hizo usitishwe mara moja na uchunguzi kamili kuanza ili kuhakikisha kuwa njama hizo hazipo.
Rais Uhuru Kenyatta alizindua kadi hiyo maalum mapema mwezi huu, kama njia moja ya kuhakikisha chama hicho kimewasajili wanachama wengi zaidi iwezekanavyo.
Kadi hizo maalum pia zinalenga kuhakikisha kuwa ni wanachama wa chama hicho pekee ambao watashiriki katika shughuli za uteuzi, ili kuondoa madai ya mapendeleo ambayo huandama shughuli hizo. Inadaiwa kuwa JP inalenga kuuza kadi milioni 10 kote nchini.
Wakati huo huo, chama hicho kinataka majina ya wapigakura wote milioni tisa ambao hawajasajiliwa kuchapishwa rasmi na serikali ili kuepuka hali ambapo baadhi ya watu wamesajiliwa kama wapigakura kwa namba sawa za vitambulisho.
“Ikiwa majina hayo yanaweza kuchapishwa, rais na viongozi wengine serikalini hawangeacha majukumu yao kwenda kufanya kampeni wakati wananchi wanaendelea kuteseka kutokanana ukosefu wa huduma muhimu kama afya,” akasema mojawapo ya wanachama wa bara kuu la chama Bw Basil Mwakilingo.
Alisema kuwa ikiwa rais ameshindwa kusuluhisha changamoto zinazowaathiri Wakenya anapaswa kujiuzulu.