Kila tukio, jema au baya, kwa mwenye akili hulifanyia assessment. Kama ni jema, unajiuliza ufanye nini ili unufaike zaidi. Kama ni baya, unajiuliza ni wapi ulikosea? Na ufanye nini ili kusahihisha makosa.
Serikali ya awamu ya 5 pamoja na sisi wananchi, kuna maeneo mengi tumefanya makosa:
1) Kujenga uadui kati ya sekta binafsi na Serikali, na serikali kuwaaminisha wananchi kuwa wafanyabiashara, wawekezaji ni watu wabaya. Wengi wameumizwa sana na falsafa mpya ya awamu ya 5. Na kwenye falsafa hiyo, hakuna aliyenufaika. Serikali, sekta binafsi na wananchi, kila mmoja ameumizwa kwa namna yake. Ni falsafa hii imetengeneza uonevu wa hali ya juu. Watu walikamatwa kwa makosa ambayo yalikuwa ya kodi, wakabadilishiwa kuwa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, ili tu wakae mahabusu. Wengine wana zaidi ya mwaka, mashtaka hayaeleweki, kila siku - ushahidi haujakamilika. Halafu eti tunasema tunamwomba Mungu! Huu ni unafiki mkubwa. Biblia inasema, ukitaka kuomba msamaha kwa Mungu, kwanza kapatane na uliyehitilafiana naye, ndipo ukaombe msamaha kwake. Huwezi kwenda kumwomba msamaha Mungu, huku una rundo la watu umewasweka ndani kwa uonevu, halafu utegemee kusikilizwa. Ujue kuwa huyo unayemwonea, pengine kwa chuki na kulipiza kisasi, ndiyo image ya Mungu. Kabla hatujamwendea Mungu, tuwaachie tuliowaonea, tusameheane, tupendane, tushirikishane, tuaminiane, tukusanye nguvu zetu zote, ndipo tumwombe Mungu wetu akaweke baraka katika jitihada zetu, na atuongezee hekima ya kuzitambua mbinu nyingine.
2) Kutowashirikisha watu katika mambo yanayowagusa. Nchi hii tupo zaidi ya watu milioni 55. Hakuna hata mmoja, yeye pekee yake akawa na akili na uwezo kuwazidi wote waliosalia, katika umoja wao. Utofauti wetu katika karama, uwezo, utaalam na mengine mengi, ndiyo nguvu ya Taifa. Tulipojua kuwa kuna tishio la huu ugonjwa tulistahili, kila kundi kukaa na kutafakari na kutoa mapendekezo namna ya kulihami Taifa letu. Watu wa Afya walistahili kukaa na kujadili kwa mtazamo wa kiafya, halikadhalika wanauchumi, watu wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama, wataalam wa utalii, kilimo na sekta nyingine zote za uchumi. Wote hawa wangeonesha namna maeneo yao ambavyo yangeathirika, na namna ambavyo yangeshiriki kikamilifu katika haya mapambano. Hilo halikufanyika. Watu wachache tu wanaoamini wana ufahamu kuwazidi Watanzania wote, ndio wakawa wanatoa matamko, na nyinyi wengine mnatakiwa kufuata tu, kwa sababu hamna akili! Mathalani mnaambiwa haiwezekani kuwazuia watalii kwa sababu uchumi utayumba - hakuna kujiuliza, hao watalii watatoka wapi wakati wa janga kama hili ambapo nchi mbalimbali zilikuwa zinafunga mipaka yake. Na nani ataendelea kuwa na hamu ya kutalii wakati wenzake nyumbani wanaangamia. Hatukuwazuia watalii, je, sasa hivi wanakuja? Hapo inaonesha tatizo la upeo wa kuona mambo kabla hayajatokea. Kipimo kizuri cha IQ, ni uwezo wa kuiona kesho kabla hujaifikia.
3) Ukosefu wa Continuous Assessment. Unapofanya mipango yoyote, ni lazima kuwe na continuous assessment. Assessment hiyo inakufanya uweze kubadilisha mbinu kwa kadiri ya matukio yanavyokwenda. Hii inatakiwa kufanywa na super intelligent brains. Siyo sahihi kazi hiyo kufanywa na Mkuu wa Mkoa, Waziri au Rais. Viongozi wa kisiasa, wanatakiwa tu kuwa wasemaji lakini siyo watu wanaofanya kazi hiyo. Inaonekana hatuna watu wa namna hiyo. Kwa sasa sisi tunaamshwa na matukio.
4) Nguvu ya Pamoja. Taifa letu limekosa nguvu ya pamoja. Wakati wa majanga, ni wakati wa kusahau tofauti zenu ndogo ndogo ili kujenga nguvu ya pamoja kupambana na tatizo. Lakini hilo halitokei tu, bali linatengenezwa. Mara baada ya kutokea janga hili, haionekane kuwepo kwa jitihada za kuwaunganisha Watanzania. Kwenye tatizo hili bado wanasiasa wanaongea kama CCM na WAPINZANI, badala ya kuongea kama Watanzania. Ni jitihada gani ilifanyika kuhakikisha tunalikabili tatizo kama Watanzania? Bahati mbaya, hatuna watu wenye hekima hiyo katika uongozi. Kama kuna kitu Mwalimu Nyerere alifanikiwa wakati wa vita dhidi ya Idd Amin, ni kwaunganisha Watanzania. Kila mmoja, mpaka mwananchi wa kijijini aliona analazimika kushiriki. Ndiyo maana watu waliuza kuku, mbuzi, ngombe ili hela ikasaidie vita. Kwenye vita hii dhidi ya Covid 19, watu wapo kwenye ari ya namna hiyo?
5) Diplomasia. Kama kuna kosa kubwa lililofanywa na awamu hii, ni kuharibu kabisa haiba ya Tanzania kwenye mahusiano ya kimataifa. Tanzania leo inafahamika kwa ukiukaji wa haki za kiraia, kidemokrasia na kisiasa. Ukiukaji huo umetujengea kuta za wazi na za siri dhidi ya marafiki zetu na taasisi za kimataifa ambazo zingekuwa na msaada mkubwa nyakati kama hizi, na baada ya janga hili. Tusidanganyike, bado tunaihitaji sana Dunia kuliko Dunia inavyotuhitaji sisi. Tuna mambo mengi ambayo hatuwezi kufanikiwa bila ya kuwa na mahusiano mazuri na jamii ya kimataifa. Wakati wa vita dhidi ya Idd Amin, Mwalimu alikuwa na timu nzuri ya wanadiplomasia. Wakati tunapigana, timu hii ilikuwa inazunguka Duniani, kuuhabarisha Ulimwengu, kwa nini tunapigana, ni nini wanaweza kutusaidia, n.k. Diplomasia inahitaji watu makini, siyo watu arrogant, watu wenye kiburi cha aina yoyote ile. Awamu hii, tumejitahidi sana kuwapata watu wenye kiburi na jeuri ya madaraka katika nafasi mbalimbali, mbaya zaidi mpaka kwenye diplomasia.
6) Ushabiki wa Kijinga. Mtaani, Serikalini, Bungeni mpaka Mahakamani, tumepeleka ushabiki wa kijinga. Hata jambo liwe zuri kiasi gani, kwanza inatazamwa aliyelitamka ni wa chama gani. Hata jambo liwe la hovyo kiasi gani, ili kulipinga, tunaangalia limetamkwa na nani. Kama ni wa chama changu, basi hili jambo la hovyo litafanywa la maana. Nasikia kule Bungeni kuna wabunge walitaka madhara na Covid 19 yajadiliwe, lakini hoja ilitupwa kapuni kwa sababu aliyetoa hoja siyo wa chama kinachoongoza Serikali. Kwa fikra hizo hatuwezi kufika popote. Kama tunataka kupambana na janga la Covid 19, na athari zake, tunatakiwa kusimama kama familia moja, na kusahau tofauti zetu za kisiasa.
Turudi, tuyaone mapungufu yetu, tujisahihishe. La sivyo matarajio makubwa, yatageuka kuwa anguko kubwa.