Benki za Tanzania, CRDB Plc na NMB Plc, zimeingia kwenye orodha ya Forbes ya Benki Zinazofanya Vizuri Zaidi Duniani mwaka 2026, zikishika nafasi miongoni mwa benki 500 zilizotathminiwa kutoka nchi 89.
Benki hizo zimewekwa kwenye Kundi la 6, linalojumuisha benki zenye mali zenye thamani ya kati ya dola bilioni 3, sawa na takribani Sh7.9 trilioni kwa kiwango cha sasa cha ubadilishaji fedha, hadi dola bilioni 10, sawa na Sh26.6 trilioni.
Forbes kwa kushirikiana na kampuni ya utafiti wa soko ya Statista, ilizitathmini benki hizo kwa kuangalia faida, ukuaji na ubora wa mapato, uwezo wa mtaji na upatikanaji wa fedha, pamoja na ubora na ufanisi wa mali.
Faida ilichangia asilimia 30 ya tathmini, huku ukuaji na ubora wa mapato ukichangia asilimia 20. Uwezo wa mtaji na upatikanaji wa fedha, pamoja na ubora na ufanisi wa mali, kila kimoja kilichangia asilimia 25.
Orodha hii ni tofauti na orodha nyingine za Forbes za benki za kitaifa na kimataifa, ambazo kwa kiasi kikubwa hutegemea maoni ya wateja yaliyokusanywa kupitia tafiti. Tathmini ya mwaka 2026 ilitumia taarifa za kifedha kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo jukwaa la S&P Capital IQ, tafiti na taarifa zilizowasilishwa na benki zenyewe.
Kuingizwa kwa CRDB na NMB kwenye orodha hiyo kunakuja baada ya benki zote mbili kuripoti matokeo mazuri ya kifedha mwaka 2025. CRDB ilipata faida baada ya kodi ya Sh725 bilioni, huku mali zake zikifikia Sh22.2 trilioni, sawa na takribani dola bilioni 8.44. NMB ilipata faida baada ya kodi ya Sh750 bilioni na kuwa na mali zenye thamani ya Sh17.2 trilioni, sawa na takribani dola bilioni 6.6.
Takwimu za benki hizo mbili zimeendelea kuongezeka na kufikia viwango vipya katika kipindi cha miezi minane ya mwaka huu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, alisema mafanikio ya benki hizo yanatokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, kuongezeka kwa imani ya wafanyabiashara na kuongezeka kwa upatikanaji wa mikopo.
Alisema benki hunufaika zaidi zinapoweza kukusanya amana na kuzitumia kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wananchi
“Biashara zimekua na watu wengi wana imani ya kupata mikopo, kufanya biashara na kurejesha mikopo hiyo,” alisema.
Tutuba alisema kiwango cha mikopo chechefu katika sekta ya benki cha asilimia 2.6 kinaonyesha kuwa wakopaji wengi wanarejesha mikopo yao kama walivyokubaliana