Mfanyabiashara Maarufu, Mohamed Raza akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Mfanyabiashara maarufu, ambaye pia, ni mshauri wa zamani wa masuala ya michezo wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Mohamed Raza, amepinga wazo la kuanzishwa serikali moja katika mfumo wa Muungano wa Tanzania akisema jambo hilo ni uhaini kwa vile linalenga kufuta utaifa wa Wazanzibari.
Raza, alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na kusisitiza kwamba wazo hilo pia ni utovu wa maadili, ukiukwaji wa sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katiba ya nchi na pia ni hatari kwa mustakabali wa CCM, kwani inaweza kupoteza kura zote, ikiwamo kura yake Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Alisema viongozi wa serikali ya Muungano wamekuwa wakidai kuwa serikali ya Tanganyika imefutwa, lakini ukweli ni kwamba, bado ipo na kwamba, imejificha ndani ya Tanzania.
Alisema sera ya CCM inatambua serikali mbili katika mfumo wa Muungano, na si moja wala tatu na kuongeza kuwa suala la kiongozi wa serikali ndani ya Muungano kutaka kuanzishwa serikali moja, ni ishara kwamba, wamepotoka kimaadili.
"Ndio maana G55 (kundi la wabunge 55) ilipokuja na hoja ya kuanzishwa serikali tatu, Mwalimu Nyerere alisimama na kuipinga kwa nguvu zake zote kwa vile sera ya CCM na Katiba ya nchi inazungumzia serikali mbili. Kuzungumza serikali moja ni uhalifu sababu unataka kumfutia mtu utaifa wake. Ninahofu sana ushindi kwa CCM.
Kama chama hakijawekwa sawa halafu tunakwenda kwenye uchaguzi, ni hatari. Wallahi leo CCM iseme kuna serikali moja, tuone kama watapata hata kura moja Zanzibar, yangu ikiwamo," alisema.
Hata hivyo, alisema kama kumeonekana hapana budi kuanzishwa serikali moja katika mfumo wa Muungano, ni vema wananchi wakatangaziwa mgogoro wa Katiba na kwa sababu hiyo, hata kamati iliyoundwa kushughulikia kero za Muungano, Wazanzibari hawawezi kuwa na imani nayo.
Hata hivyo, alisema ili kuimarisha Muungano, Watanganyika waiachie Zanzibar ijitegemee kiuchumi ambapo alisema: "Hata Dubai kuna Muungano wa Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE), unaoziunganisha nchi kama vile Sharja na nyinginezo, lakini kila moja inajitegemea."
Alisema wanachokitaka Wazanzibari ni "kuheshimiana, kuvumiliana na kujadiliana" inapokuja hoja kuhusu Muungano na kusisitiza kuwa hakuna anayetaka kuvunja Muungano.
Alisema jambo lingine analopinga, ni kundi la watu kudhani kwamba lenyewe tu ndilo linaweza kuongoza nchi au wanafikiria wao ni bora wa kuongoza nchi.
Alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kueleza walikofikia wanasheria wa pande mbili za Muungano katika kushughulikia utata wa hoja ya kama Zanzibar ni nchi au la. "Mmetamka hadharani, iko wapi ripoti?," alihoji Raza.
Juzi akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Culture, Vuga Mji Mkongwe, Zanzibar, Maalim Seif alisema kauli ya Pinda aliyoitoa bungeni mjini Dodoma hivi karibuni kwamba anatamani kuwe na serikali moja sio ngeni na kwamba mpango huo upo siku nyingi, kama ambavyo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alivyowahi kusema siku za nyuma