SoC03 “Dagashida” Imulikwe, ni hatari

SoC03 “Dagashida” Imulikwe, ni hatari

Stories of Change - 2023 Competition

KwetuKwanza

Member
Joined
Mar 13, 2023
Posts
82
Reaction score
150
Moja ya eneo ambalo limekuwa utambulisho kwa jamii husika hapa nchini, ni mila na desturi ambazo zinaweza kutofautisha kati ya jamii fulani na jamii nyingine.

Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania tunayo makabila zaidi ya 120, ambapo kabila la Wasukuma likitajwa kuwa kabila kubwa zaidi kuliko mengine hapa nchini.

Wasukuma wanapatikana katika Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, pamoja na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Singida na Tabora.

Kabila hilo limekuwa na utamaduni wa kuunda Jeshi la jadi (DAGASHIDA).

Jeshi hili kazi yake kubwa ni kushiriki katika suala zima la ulinzi shirikishi kwa kufuata kanuni na taratibu zote za nchi.

Jeshi hili la jadi kwa kushirikiana na chombo cha serikali cha kupatambana na uhalifu (Jeshi la Polisi) ushirikiana katika kukomesha uhalifu kwenye jamii husika.

Madhalani katika Mkoa wa Simiyu kila kitongoji au kijiji kimeunda jeshi hili la jadi (DAGASHIDA) ambapo uundwa na vijana wote wenye umri wa kuanzia miaka 18-45 waliopo kwenye Kitongoji au Kijiji husika.
vlcsnap-2023-06-25-04h44m24s095.png

Jeshi hili lina viongozi ambao wanaitwa Sumbamtale hawa ndio wanaongoza Jeshi hili, wakipokea kila amri kutoka kwa Wazee wa Kijiji au Kitongoji wanaoitwa Nyangongo.

Licha ya Malengo ya uanzishwaji wa Chombo hiki cha Kimila kuwa mazuri, sasa Jeshi hili kwa kipindi cha hivi karibuni limegeuka mwiba kwa wananchi.

Dagashida hasa katika Mkoa wa Simiyu sasa inajichukulia sheria mkononi, ikiwemo kusababisha vifo vya watu mbalimbali lakini pia kufanya Uhalifu, Unyang'anyi, Unyanyasaji kwa jamii, na Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

Licha ya hivyo Jeshi hili limegeuzwa kuwa la kisiasa zaidi, kwani wanasiasa wamekuwa wakilitumia katika kitimiza mambo yao ambayo yanakiuka Haki za Binadamu ikiwemo kusababisha vifo.

Mauaji, Uhalifu, Unyanyasaji na Unyang'anyi.

Kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2023, zaidi ya matukio matatu ya watu kuawa na Jeshi la jadi (DAGASHIDA) yameripotiwa na Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Simiyu.

Pia yameripotiwa matukio ya unyanyasaji, ukiukwaji wa haki za Binadamu, uhalifu, yanayofanywa na Jeshi hilo la Jadi.

Meatu Mauaji, Uhalifu na Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

Moja ya tukio lilitokea katika kijiji cha Bukundi Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu ambalo lilitokea Februari 23, 2023 ambapo Wiliam Fumbuka mkazi wa kijiji hicho aliuawa.

Baada ya kuuawa Familia ya Marehemu Fumbuka, walishirikisha Jeshi la Jadi (DAGASHIDA) kuwasaka wahalifu, ambapo Jeshi hilo lilivamia kwenye familia za watuhumiwa watatu na kufanya uhalifu mkubwa.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Jeshi hilo la Jadi lilivamia kwenye nyumba za watuhumiwa na kuchukua mifugo yote kisha kugawana, lakini mifugo mingine iliuawa.

Mbali na hilo jeshi hilo lilichukua vyakula, mali mbalimbali vikiwemo vyombo vya ndani, kuvunja baadhi ya vifaa kwenye nyumba za watuhumiwa, ambapo mali na mifugo waligawana.

Itilima Mauaji.

Tukio jingine ni katika kijiji cha Ntega kata ya Ikindilo Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu ambapo Maduhu Ngasa aliuawa na Jeshi la jadi (DAGASHIDA) katika kijiji hicho.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, Ngasa aliuawa baada ya kupigwa sana kwa silaha za jadi akituhumiwa kuwa anahusika katika wizi mbalimbali kijiji hapo.
vlcsnap-2023-06-25-04h45m28s231.png

Inadaiwa kuwa uliitishwa mkutano wa Dagashida, ambapo Ngasa alikamatwa na kuletwa mbele ya viongozi wa Jeshi hilo, huku akipatiwa kichapo akishinikizwa awataje wenzake anaoshirikiana nao kwenye wizi.

Marehemu alipigwa sana kwa silaha mbalimbali za jadi, hadi kumsababishia umauti, ambapo Diwani wa kata hiyo alidaiwa kuhusika kwenye kuitisha kikao hicho cha Jadi.

Bariadi, ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

Usiku wa tarehe 19.4.2023, mtu mmoja, Njenje Shigilu, alifanya uhalifu wa kuvunja na kuiba TV kwenye Saluni moja kwenye kijiji hicho na baadaye akakamatwa.

Asubuhi mtuhumiwa aliwekwa kati kisha akataja watu wengine wa kijijini hapo ambao ni Kahulya Chalya, Lulyalya Deni, Salum Masunga, Mbelya Mola na Kalomo Juma, wote hao walipigwa vibaya na Dagashida.

Dagashida ya Gilya ilikwenda kwenye familia za watuhumiwa hao kutaka wapewe fedha Sh 500,000 kila familia ya mtuhumiwa na Familia moja ilichukuliwa mbuzi 50.

Familia ya Paul Salumu, Deni Kalimilo na Kalomo Juma zilikataa kutoa Sh 500,000, Dagashida iliamuru Familia hizo zitengwe kushiriki shughuli za kijamii kijijini hapo.

Hakuna kwenda Dukani kununua majitaji yoyote ya kibinadamu na hakuna mtu yeyote kwenda kwenye familia hizo hadi wailipe Dagashida Sh 500,000.
vlcsnap-2023-06-25-04h46m47s790.png

Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Gilya, Dotto Masalu na Diwani wa Kata hiyo, Lewa Safari walishiriki katika maamuzi hayo.

Haya ni baadhi ya matukio tu ambayo kwa namna moja au nyingine yameripotiwa, yanaonyesha jinsi Utamaduni huu wa kabila la wasukuma ambavyo unakiuka haki za Binadamu, lakini unaongeza Uhalifu, na Unyanyasaji.

Matukio mengi ya watu kupewa adhabu bila kipimo, tena mbele ya jamii, watu kutengwa, kunyanyaswa, kuchukuliwa mali zao kwa nguvu, yamekuwa yakifanywa na Jeshi hili, bila ya hata kuchukuliwa hatua.

Katika baadhi ya maeneo ambayo Jeshi la Polisi limetaka kuchukua hatua, viongozi wa kisiasa uingilia kati, hasa Wabunge na Madiwani, lakini pia viongozi hao wanaongoza kushiriki kulitumia Jeshi hilo kufanya uovu huo.

Jeshi hili lenyewe ndilo linakamata na kutoa hukumu kwa mtuhumiwa, na wala halitoa nafasi ya mtu kujieleza, limegeuka mwiba kwa jamii, wapo watu wengi wanaona sasa lipo juu ya sheria.

Takwimu ambazo siyo rasmi zinaonyesha kuwa kila baada ya siku mbili ndani ya Mkoa lazima watu wafanyiwe vitu hivyo na Jeshi hilo, ambapo matukio mengi hayaripotiwi katika vyombo vya kisheria.

Wengi sasa wanaliogopa, wanashindwa hata kutoa taarifa kwa vyombo vya kisheria, wakiogopa kutengwa, wananchi uko vijijini wana hofu, Jeshi hili limejitwalia mamlaka na madaraka, uko vijijini hakuna utawala wa sheria bali ni utawala wa Jeshi la Dagashida.

Ni wakati sasa Serikali, likiwemo Jeshi la Polisi, kuchukua hatua kali dhidi ya Dagashida.

Dagashida wanaona wao ndiyo wenye mamlaka uko vijijini, hakuna mtu mwingine hapa nchini, hawajui uwepo wa utawala wa sheria.

Dagashida imulikwe, hatua zichukuliwe, lipigwe marufu kujichukulia sheria mkononi, libaki katika misingi yake ya kuanzishwa, tusipokuwa makini Dagashida itakuja kuwa kama waasi wa M23 uko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Boko Haram Nigeria.

MWISHO.

(Picha zote kwa Hisani ya Mwandishi wa Makala hii).
 
Upvote 1
Back
Top Bottom