Dar es Salaam. Watu watatu wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa katika machimbo ya kikikaka, Mjimwema - Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kudondokewa na kifusi wakati wakipakia kokoto katika gari.
Tukio hilo limetokea leo Aprili 3, 2022 saa saa tatu asubuhi katika machimbo hayo ambayo awali yalikuwa yakitumiwa na wachimba kokoto wadogo kabla ya Serikali kuyafunga mwaka 2018.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amesema baada ya taarifa za tukio, jitihada za uokoaji zilianza.
"Mwanzoni tulikuwa hatuna idadi kamili kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kuthibitisha kuna watu wangapi huko chini, lakini tulipoongea na viongozi wa maeneo haya walituambia kuwa siku za mwisho wa wiki huwa hazina watu wengi.
"Jitihada zimefanyika za uokoaji na tumefanikiwa kutoa kifusi hadi kugusa mwamba na kutoa miili mitatu ya jinsia ya kiume na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Vijibweni” amesema Fatma
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa maeneo hayo kuwa yeyote ambaye atakuwa na taarifa au kutomuona ndugu yake na anafanya kazi katika machimbo hayo atoe taarifa ili hatua nyingine za ufuatiliaji zichukuliwe.