Leon Bahati, Mwananchi - 11/02/2012
UTAFITI wa hivi karibuni uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Johns Hopkins nchini Marekani, umegundua kuwa matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARV) yanaweza kuwafanya waathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU) kukutana kimwili na wapenzi wao bila kondomu, pasi kuwapa maambukizi.
Wakati wataalamu hao wakifikia hatua hiyo muhimu katika kupata jibu la janga hilo lililoitesa dunia kwa miongo kadhaa sasa, kuna taarifa njema pia za kugunduliwa kwa chanjo mpya ya Ukimwi.
Kwa upande wa utafiti wa ARV walioufanyiwa majaribio kwenye sehemu mbalimbali za dunia, umebaini kuwa mtu ambaye anatumia dawa za kurefusha maisha, anaweza kufanya tendo la ndoa bila ya kutumia kondomu na mtu ambaye hana Ukimwi na asimwambukize kwa asilimia 95.