SoC01 Dawa za Kulevya zinavyorudisha nyuma maendeleo ya Taifa

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Aug 19, 2021
Posts
6
Reaction score
7
Rashid Abdallah Makwiro mmoja kati ya wasanii bora zaidi wa Hip Hop nchini. Watu wengi hawawezi kulijua jina hili, huyu anafahamika kwa jina maarufu sana la Chid Benz.

Unamkumbuka Chid Benz katika ubora wake akiwa karibu na kipaza sauti? Alitisha sana, ukibisha unachotakiwa kufanya ni kutafuta kanda za video za nyimbo zake hasa ya Ngoma itambae, Dar es salaam Stand up na Mmenisoma ya mwaka 2010 ambayo ilimpa tuzo ya kuwa mwanamziki bora wa Hip Hop nchini. Hapo utaniamini kuwa Child Benzi alikuwa hatari sana.

Lakini kwa kitambo kidogo Chid Benz alipotea akawa siyo Chid Benzi yule, ambaye wapenzi wa muziki nchini walimjua. Sasa hivi anajitahidi kurudia enzi zake lakini haitazamiki kama ataufikia uwezo wake ule wa miaka karibu kumi na tano iliyopita.

Kwa sasa anaonekana akili yake imechoka na mwili wake pia umechoka zaidi. Yote hii ni kwa sababu utumizi ulipita kipimo cha utumizi wa madawa ya kulevya, ambayo yalimuathiri kwa kiasi kikubwa sana na kuweza kusababisha apotee katika muziki wake ambapo tayari alishachukua nafasi ya kuwa gwiji wa Hip Hop nchini na kuuteka muziki wa kizazi kipya.

Hakuwa tu Chid Benz peke yake katika hili wapo wanamuziki wengine wengi tu ambao wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya.

Mfikirie Haridi Mohamed maarufu kwa jina la TID halafu jaribu kumkumbuka Rehema Chalamila aliyekwenda kwa majina ya Ray C jinsi walivyokuwa miaka kumi na tano iliyopita na leo yao ya sasa walivyo.

Hakuna anayejua ila kila nikitaja matumizi ya madawa ya kulevya kwa wale waumini wanaamini kuwa siku za mwisho zimekaribia maana maovu mengi yameongezeka kila pembe ya ardhi, ukitazama jinsi vijana kwa wazee wanavyozidisha maovu, ndoa za jinsia moja zimekuwa kama mtindo wa kawaida kadri miaka inavyoongezeka.

Kila ukilitazama jiji la Dar es salaam huwa unaweza kupata maswali mengi yasiyokuwa na majibu jinsi ukiona vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa asilimia nyingi wameathiriwa na matumizi ya madawa ya kulevya, Mara nyingi
ukipita katika hospitali ya taifa pale Muhimbili miaka ya 2017 hata 2018 ungeweza kukuta utitiri wa vijana waliokuwa katika kliniki ya kuweza kuacha matumizi ya madawa hayo hatari ya kulevya.

Kote duniani majiji ndio yamekuwa kama kimelea cha vijana wengi kuanza kufanya mambo ya siyokuwa na maadili kama utumiaji wa madawa ya kulevya na uvutaji wa bangi na matumizi mengine ya vilevi kama pombe kali.

Ukitembea kwenye maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ukiamua kutembelea maeneo ya Manzese, Keko,Tandale, Mwananyamala na Buguruni vijana wengi wamepotea katika kula dawa hizo hatari za kulevya.

Kwa wapenzi wa tamthiliya ukiwaona baadhi ya vijana walioathirika na madawa hayo inaweza kukujia taswira ya tamthilia ya ‘Walking Dead’ ambayo ndani yake kuna wahusika wengi wa mazombi tu.

Ukitupa jicho upande wa kulia utamuona mtu asiyeeleweka kwa sura kuwa ni kijana au zzee huku anakwenda akisinzia, anaanguka haanguki, na kushoto pia ukijaribu kugeuka inakuwa ni hivyo hivyo unaweza kumuona mtu haeleweki kama anakwenda au anarudi na usishangae wanasubiri uzubae wakwapue chochote mkononi mwako ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kupata madawa hatarishi.

Kuna ule msemo maarufu sana wa kiingereza aliyowahi kuusema kiongozi wa zamani wa madhehebu ya Ahmadiyya unaosema. "A nation can not be reformed without Reformation of its youth" kwa kiswahili maana yake ‘taifa lolote haliwezi kuendelea bila kwanza kuwaimarisha vijana wake’. Baada ya kukumbuka msemo huo unaweza kujaribu kufikiri vijana wengi wakiathirika na uraibu wa kutumia madawa ya kulevya kisha kuathirika taifa linaweza kupiga hatua na kuendelea mbele?

Najaribu kueleza ili wale kina Pablo Escobar wa leo na El Chapo wadogo wadogo wanaopatikana nchini Tanzania wauzaji madawa ya kulevya washikwe na roho ya huruma kama ya yule Mmarekani aliyelipua miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan kwa bomu lake ambalo liliteketeza mamilion ya viumbe wasiokuwa na hatia na kusababisha madhara makubwa kwa taifa la Japan.

Raia yule wa Marekani alikuja kukaririwa baadae na waandishi wa habari akijuta na kusema kauli ya kusikitisha sana, alisema "nimeleta nini duniani" baada ya kuona uharibifu alioufanya na maafa makubwa kiasi kile aliyosababisha kwa wananchi wengi wasiokuwa na hatia.

Au yule mpiga picha aliyekufa kwa msongo wa mawazo baada ya kupata tuzo ambayo aliandaa makala iliyoonyesha mtoto akifariki kwa njaa lakini yeye alishindwa kumsaidia akiendelea kuandaa habari hadi mtoto akafariki dunia.

Baadae mwandishi huyo akajikuta kuwa ni mkatili kama yule ‘rafiki yake’ mmarekani uliyemsoma hapo juu, huyu sasa akawa na mawazo kwa kushindwa kumsaidia mtoto yule hadi akafariki dunia kutokana na mawazo ya ukatili alioufanya kwa mtoto huyo.

Basi kwa wote wanaohusika na uuzaji na uingiaji wa madawa hayo nafsi ziwasute mnaojiita na mapusha kwa kuchelea mkaja kujuta baada ya kuwasababishia maafa makubwa vijana wengi.

Kila mtu anataka roho za huruma ziwajie kabla na sio baada ya matatizo kutokea kama yule mmarekani na yule mwandishi walivyokuwa wakijuta baada ya matatizo kuwakumba watu.

Angalau aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam aliyepita Paul Makonda alianzisha harakati makhususi dhidi ya madawa ya kulevya lakini matokeo yake yameleta ahueni tu.

Kuhusu kutokomeza madawa ya kulevya ni kazi ngumu kwa kila nchi duniani japo juhudi zimeendelea kutendeka.

Natamani sana vijana waachane na madawa hayo ili waweze kujenga taifa moja lenye uadilifu, hapo haitakuwa kazi ndogo na ya siku moja kiukweli itakuwa kazi ngumu ya jasho na damu kama ya kuiaminisha dunia kuwa kuna siku jua liliwahi likizama mashariki .

Ilifika wakati ambao Chid Benz alijuta kwanini alitumia madawa hayo ambayo yamemfanya awe kama alivyo sasa. Haipendezi vijana wengi wajute baada ya matumizi kama Chid Benz alivyofanya na staki pia wale wauzaji wajute baada ya kuangamiza vijana wengi, nataka kuona roho za huruma zikiwashika kabla ya kusababisha matatizo.

Vijana ndio uti wa mgongo wa taifa lolote hivyo kila nchi duniani inategemea sana vijana wake wao ndio wawakilishi wazuri wa nchi kama ilivyo kwa wanamuziki na wacheza soka karibu asilimia nyingi ni vijana.

Vijana wakilala taifa pia litalala wao ndio muhimili wa taifa kwenye nyanja zote.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…