Wakuu nimekuwa nikiona watangaza bidhaa za dawa za tiba asili wanadai dawa zao hazina kemikali kabisa na kusisitiza watu kutumia hizo badala ya za hospitali ambazo huwa na kemikali.
Nimekumbuka baada ya kuona Heparin ameandika kuwa dawa zote za asili huwa ni salama kwa silimia mia na hazina Kemikali
Nimekumbuka baada ya kuona Heparin ameandika kuwa dawa zote za asili huwa ni salama kwa silimia mia na hazina Kemikali
- Tunachokijua
- Kemikali ni dutu yoyote ambayo ina muundo maalum au kemikali huundwa na "vitu" vile vile. Baadhi ya kemikali hupatikana kiasili, na Kemikali nyingine hutengenezwa. Kemikali zipo kila mahali, kama kwenye chakula unachokula, nguo unazovaa hata hata wewe mwenyewe kiumbe hai umeundwa na aina mbalimbali za kemikali.
Kumekuwepo na madai kuwa dawa za asili au tiba asili hazina kemikali na ni salama kwa matumizi kwa asilimia mia.
Je, uhalisia wa Madai haya ni upi?
JamiiCheck imepitia tafiti na machapisho mbalimbali yaliyochapishwa kwenye tovuti zinazoaminika ambapo tumebaini kuwa Dawa za asili au tiba asili zina kemikali kwa kuwa zinatokana na mimea au viumbe hai ambao nao wana kemikali.
Dawa za asili zitokanazo na miti mara nyingi hufikiriwa kuwa hazina "kemikali" na husisitizwa zaidi kuwa ni salama na hazina kemikali hatarishi kwa sababu zinatokana na vyanzo vya kiasili kama mimea yaani mizizi, gome, matunda na majani. Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba kila kitu kinaundwa na kemikali kikiwemo dawa za mitishamba ambazo nazo zina kemikali. Hivyo dawa zinazotokana na mimea zinatumia kemikali za kiasili zinazopatikana kwenye mimea hiyo ili kutoa matibabu.
Mimea inazalisha kemikali ambazo ni za kiasili na zinaweza kuwa na athari chanya za matibabu au athari hasi. Kwa mfano, quinine ambayo hutumika kutibu malaria inatokana na mti wa cinchona, mti huo huzalisha kemikali za kiasili lakini inaweza kuwa na nguvu na madhara kama vile kemikali zinazotengenezwa viwandani.
Ingawa dawa za Tiba Asili(mitishamba) zinaweza kuwa na faida kubwa kiafya, zinaweza pia kuwa na madhara iwapo hazitatumika kwa usahihi au kama zinaingiliana na dawa za kisasa. Baadhi ya kemikali za mimea zinaweza kuwa na sumu au madhara mengi, hasa pale zinapochanganywa au kutumiwa kwa dozi isiyofaa au kuchanganywa kwa mimea itakayozalisha kemikali nyingine na kusababisha madhara kwani dawa nyingi za Asili hazijafanyiwa vipimo ili kujua aina za kemikali zilizopo na madhara yake yaliyo hasi au chanya.
Aidha, mimea ina kemikali aina ya phytochemicals ambayo ina athari kwa mwili. Kutumia Dawa asili au mitishamba Kunaweza kuwa na athari kidogo inapotumiwa katika kiasi kidogo na baadhi ya mitishamba huwa sumu ikitumiwa kwa kiasi kikubwa.
Kemikali mbalimbali ambazo husaidia afya ya mimea na wakati mwingine zinaweza kuwa na manufaa au madhara kwa binadamu
1. Tannini, Mfano Tannins hupatikana kwenye chai, kahawa na baadhi ya matunda kama zabibu na pomegranate. ambayo kemikali hiyo huwa na faida na madhara kwa binadamu.
- Tannini zina athari za antibacterial na antiviral, na hutumika sana kusaidia kuponya majeraha na kuzuia maambukizi.
-Tannini nyingi zinaweza kupunguza uwezo wa mwili kufyonza madini kama chuma, hivyo matumizi ya kupindukia yanaweza kusababisha upungufu wa madini mwilini.
2. Glycosides Mfano, Digoxin kwenye foxglove, Salicin kwenye gome la mti wa willow ambazo zina faida na madhara kwa binadamu
-Glycosides kama digoxin hutumiwa kutibu matatizo ya moyo. Salicin hutumika kupunguza maumivu na kuvimba.
-Matumizi mabaya ya glycosides yanaweza kusababisha sumu kali, hasa digoxin, ikiwa itatumika kupita kiasi.
3. Alkaloidi, Mfano Kafeini ambayo ipo kwenye kahawa na chai, Nikotini kwenye tumbaku
4. Flavonoidi, Mfano Quercetin na Kaempferol zilizopo kwenye mboga za majani, matunda, na chai ya kijani
5. Saponini, Mfano Ginseng saponins na Diosgenin kwenye viazi vikuu
6. Terpenoidi Mfano, Menthol kwenye mnanaa, Carotenoids kwenye karoti, mboga za kijani kibichi
7. Phenols na Polyphenols Mfano, Resveratrol katika zabibu nyekundu, Catechins katika chai ya kijani
8. Vitamini na Madini Mfano, Vitamini C kwenye machungwa na matunda yenye asidi, Vitamini K kwenye mboga za majani kama spinachi
9. Resini Mfano, Resini kutoka kwa mimea kama mti wa mwerezi, na miti ya mabalsamu.
10. Essence Oils (Mafuta ya Asili) Mfano, Mafuta ya lavender na mafuta ya tea tree.
Aidha kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine, wanabainisha kuwapo kwa kemikali kwenye mimea ambazo ni salama na nyingine ni sumu kwa matumizi au kutumiwa bila kiwango maalumu hivyo wanasisitiza kuwa ni muhimu kutumia dawa za asili kwa usahihi na mara nyingi kwa ushauri wa wataalamu wa afya.