Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Karafuu
MKUU wa Wilaya ya Mkoani Pemba, Jabu Khamis Mbwana, amepiga marufuku wafanyabiashara binafsi kununua karafuu kwa njia ya rejareja majumbani.
Mbwana alisema hayo juzi baada ya kujitokeza kwa watu binafsi wanaonunua karafuu majumbani, wakijidai kwamba bei ya zao hilo imeshuka katika soko la dunia.
Akifafanua kauli hiyo, alisema kwa mujibu wa sheria, Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) ndiyo lenye mamlaka pekee ya kununua karafuu kutoka kwa wakulima.
"Wananchi wanatakiwa kufahamu kwamba ni makosa kwa mujibu wa Sheria kununua karafuu majumbani, ZSTC ndiyo pekee yenye mamlaka na majukumu ya kununuwa karafuu nchini," alisema.
Alisema Serikali imetoa bei nzuri kwa wakulima wa karafuu kwa ajili ya kuhakikisha zinauzwa kupitia ZSTC na sio kwa njia za magendo.
Kwa mujibu wa Mbwana, sheria inayopiga marufuku wananchi kukaa na karafuu majumbani bado ipo na lengo ni kudhibiti magendo na utoroshaji wa karafuu hizo.
"Wakulima wa karafuu wanapovuna mazao yao na mara baada ya kumaliza kazi ya kuanika, wanalazimika kuzipeleka katika vituo vya Serikali kwa ajili ya kuziuza... Sheria ya kupiga marufuku watu kuhifadhi karafuu majumbani bado ipo," alisema.
Msimu wa mavuno ya karafuu umeanza kisiwani Pemba ambapo wananchi wamekuwa wakichuma karafuu hizo na kuuza ZSTC. Hivi karibuni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Ahmed
Nassor Mazrui, alisema Serikali haina mpango wa kubinafsisha karafuu na kuingia katika soko huria.
Aidha Mazrui alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha mbele ya Baraza la Wawakilishi, Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo wa Karafuu, ambao miongoni mwa majukumu yake ni kuwalinda wakulima wa zao hilo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza mikakati ya kuimarisha karafuu pamoja na kupanda mikarafuu mipya milioni moja kwa kuimarisha vitalu vya miche katika mashamba ya watu binafsi.
chanzo. https://www.vtunnel.com/index.php/1...2d1fd4e9eb00a9a780c1c463b305b329788c17e117475