Dc korogwe: Sababu 11 za walimu kuichukia serikali

Dc korogwe: Sababu 11 za walimu kuichukia serikali

SG8

JF-Expert Member
Joined
Dec 12, 2009
Posts
3,955
Reaction score
2,133

  • Tukifanya yafuatayo zinaweza kuepukwa





LEO nimeona nami nianze kuweka mawazo yangu kwenye maandishi. Japokuwa kwa sasa ni kiongozi wa serikali, naamini nafasi hiyo haininyimi fursa ya kutoa mchango wangu wa mawazo kwa mustakabali wa taifa langu.
Nimekuwa nakiandika kwenye mitandao ya kijamii kama facebook pamoja na kutoa hotuba mbalimbali kwa watumishi na wananchi wilayani Korogwe. Nimeona niandike baadhi tu ya changamoto zinazowakabili walimu kwa kuwa nimekuwa nikijiuliza sana; mbona serikali inafanya mambo mengi kwa walimu lakini bado kuna baadhi ya walimu wanaichukia serikali yao?
Ninaandika masuala ambayo naamini yangefanyiwa kazi walimu wasingekuwa na manung’uniko makubwa. Sitazungumzia lile la kutaka kupandishwa mshahara kwa asilimia 100 ambalo kwa sasa naamini halitekelezeki.
Baada ya kutafakari yote hayo nimeona niandike uchambuzi ambao kwa kiasi kikubwa utazungumzia changamoto za kiutumishi za walimu wetu.
Kuwapandisha walimu madaraja
Hii ni changamoto inayowakabili walimu wetu Tanzania nzima. Wakati mwingine inasababishwa na ufinyu wa bajeti ya serikali pamoja na uzembe wa baadhi ya watendaji serikalini. Serikali mara nyingi imekuwa ikitoa maelekezo ngazi za halmashauri lakini mara nyingi yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa uzito unaostahili.
Katika kipengele hiki nitatoa mfano hai, nina ushahidi wa uzembe uliofanywa na Halimashauri ya Mji Korogwe kwenye bajeti ya mwaka 2012/2013. Walisahau kuwapandisha madaraja walimu zaidi ya 30 wa sekondari walioajiriwa mwaka 2009.
Walimu hao walitakiwa kupanda daraja kwenye bajeti ya mwaka 2012/2013, lakini wakasahaulika kwa uzembe pamoja na serikali kutoa muongozo kuwa watumishi wote wanaostahili kupanda daraja wapande wote.
Lakini wao wakawaweka kwenye bajeti ya 2013/2014 badala ya 2012/2013, nini tafsiri yake? Walimu hawa wataachwa nyuma kwa mwaka mmoja kimaslahi na walimu wenzao walioanza kazi pamoja, ikiwa ni pamoja na kutolipwa malimbikizo yao kwa sababu serikali ilikwishatoa muongozo kuwa wote wawekwe kwenye bajeti.
Kitendo kama hiki cha uzembe wa watu wachache (mkurugenzi na wenzake) kinawafanya walimu kuichukia serikali yao. Pia kuna malalamiko ya walimu kushushwa madaraja bila hatia yoyote pamoja na wengine waliokuja baada ya wao kuajiriwa, kupanda daraja na wa zamani kubaki pale pale.
Hii ni changamoto kubwa na jambo hili ni kilio cha walimu wilayani Korogwe hadi leo. Halimashauri ya Korogwe Vijijini hawana tatizo hili japokuwa wao wana eneo kubwa la utawala (Kilomita za mraba 3574 wakati za halmashauri ya mji ni kilomita za mraba 212), wao walifanikiwa kuwapandisha daraja walimu wote walioajiriwa mwaka 2009. Hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Malimbikizo ya madeni ya mshahara kwa walimu
Suala hili linahitaji kubadili mazoea katika utendaji. Kwa mtazamo wangu serikali kuu na serikali za mtaa zote ni serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lazima halmashauri zetu zibadilike na kubeba jukumu hili la malimbikizo ya madeni ya walimu ya mishahara na si kukusanya tu na kupeleka serikali kuu.
Sasa umefika wakati watenge pesa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kumaliza madeni ya walimu.
Nimekuwa nikitoa mfano kuwa kama wameajiriwa walimu 30 wa sekondari kwa ngazi ya shahada ambao mshahara wao ni 532,000 kwa mwezi kwa kila mmoja kwa walimu wa shahada, jumla yake hapa ni shilingi 15,960,000.
Unakuta halmashauri wanalipeleka deni hilo serikali kuu na inachukua zaidi ya miaka mitatu bila kulipwa, kumbe halmashauri wangeweza kulipa kupitia mapato ya ndani na kama serikali kuu italeta, halmashauri itawataka walimu walipe pole pole kwa kuwakata kwenye mishahara yao.
Hii ni muhimu kwa kuwa utakuta mwalimu katoka Kigoma na kupangiwa kazi Korogwe ambako hana ndugu na hakuna nyumba ya serikali ya kufikia. Mwalimu huyu na wenzie utakuwa umewaharibu kisaikolojia na wataiona serikali yote haina maana kwa sababu ya shilingi 15,960,000. Jambo hili lina wafanya walimu waichukie serikali yao.
Kukosekana motisha kwa walimu wa sayansi
Kwanza naunga mkono agizo la Rais Jakaya Kikwete, pamoja na jitihada za serikali na wananchi kujenga maabara kwa kila sekondari ya kata nchini. Wilayani Korogwe tunaendelea kwa kasi na mchakato huu.
Jitihada hizi zitatuondolea changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi mbele ya safari. Kwa sasa tunatakiwa kuwapa motisha walimu wa sayansi kutokana na uchache wao unaosababisha kupangiwa vipindi vingi kuliko wenzao wa masomo ya sanaa.
Mfano, kwa wiki mwalimu wa sanaa anakuwa na vipindi vinne hadi saba, wakati mwalimu wa sayansi anakuwa na vipindi kati ya 22 hadi 30 bila motisha yoyote. Mwalimu huyu lazima akate tamaa na ajione kama ananyonywa na serikali yake.
Jambo hili pia linawafanya walimu wa sayansi waichukie serikali yao. Lazima tutafakari namna ya kuwapa motisha walimu wetu wa masomo ya sayansi. Ni dhahiri, jambo hili linawafanya walimu wa sayansi waichukie serikali yao.
Aina ya wanafunzi wa kidato cha kwanza
Tunapeleka wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi waliopata alama 70 chini ya 250 ambayo ni sawa na asilimia 28 ambayo ni alama D.
Mwaka huu kwenye Mock wamesema angalau alama 100 chini ya 250 ambayo ni sawa na asilimia 40 na yenyewe kwangu pia ni D, kwa sababu nimezoea kuwa C inaanzia asilimia 41. Humu humu inasemekana wamo wasiojua kusoma na kuandika, maana hata hesabu zenyewe ni za kuchagua, inakutosha kuambia eti umefaulu.
Kwa mwanafunzi huyu pia mwalimu anawekewa Big Result Now (BRN). Kama anaingia kidato cha kwanza amefeli maana kapata D, tunatarajia nini kidato cha nne? Sisi tuliosoma teknolojia ya kompyuta tunasema kinachoingia ndicho kinachotoka.
Tunahitaji kupitia upya utaratibu wetu wa kuwapata wanafunzi wetu wa kidato cha kwanza. Lazima wizara iweke mikakati madhubuti kwenye jambo hili, ili kumsaidia Rais wetu aache alama ya kukumbukwa na Watanzania kwenye dhana ya BRN.
Mafunzo kwa walimu
Mafunzo kwa walimu ni muhimu sana. Kwenye vyuo vya ualimu walimu hufundishwa mbinu za kufundishia, ambazo kwa mazingira ya sasa zinahitaji kuboreshwa zaidi.
Ni vema serikali ikaliangalia vema jambo hili ili walimu wetu waendane na mahitaji ya elimu yetu ya sasa.
Nyumba za walimu
Nyumba za walimu ni muhimu sana. Kuna maeneo mengine hata nyumba za kupangisha walimu hakuna kutokana na mazingira yenyewe. Lazima halmashauri itambue maeneo kama haya wakati wa kutekeleza jambo hili.
Kwenye bajeti ya mwaka huu kila halimashauri itapewa shilingi milion 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Fedha hizi lazima zisimamiwe vizuri na tuachane na mambo ya wakandarasi ili tupate nyumba nyingi zaidi jambo ambalo limechangia halmashauri zetu kuwa mchwa na shamba la bibi.
Walimu kusimamia mitihani
Kulikuwa na utaratibu uliozoeleka kwa kikundi fulani cha walimu tu ndio waliokuwa wakisimamia mitihani. Kipindi fulani niliwahi kuuliza hivi kuna walimu waliosomea somo la kusimamia mitihani kiasi ambacho wengine wanakosa sifa hiyo?
Kama vigezo ni kuwa kazini miaka mitatu na kuwa na TSD namba pamoja ma vigezo vingine, sasa kwa nini kila mwaka wajirudie hao hao? Jambo hili linafanya walimu waichukie serikali yao.
Walimu kulipia vitambulisho vya kazi
Kumekuwa na utaratibu wa kuwalipisha walimu shilingi 2,000 kwa ajili ya vitambulisho, kitambulisho ni mali ya mwajiri ambaye ni serikali. Kuwalipisha walimu ni kinyume cha utaratibu. Halimashauri zimekuwa zikiwachangisha walimu wetu.
Nauliza, mbona vitambulisho vya taifa ni gharama zaidi lakini serikali inatoa bure? Jambo hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Walimu kulipia ujazaji wa fomu za OPRAS
Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya halmashauri nchini kuwataka walimu walipie gharama za photocopy za fomu za Opras. Fomu hizi ni mali ya serikali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi. Kumlipisha mwalimu kwa ajili ya fomu hizi ni kinyume cha utaratibu. Jambo hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Uhaba wa vitendea kazi
Hapa serikali inastahili pongezi maana imefanya kazi kubwa kwa upande wa vitabu. Jitihada zinatakiwa ziongezeke kwenye upande wa ofisi za walimu na maeneo mengine.
Nimegundua mambo kama haya ambayo yapo ndani ya uwezo wa serikali yanachangia kuongeza chuki kwa walimu dhidi ya serikali yao. Umefika wakati sasa wa kuwachukulia hatua za makusudi watumishi wote wanaoikwamisha serikali na watumishi wenzao, kwa sababu kila mwaka changamoto zimekuwa ni zilezile.
Sasa kwenye elimu tunazungumzia (Big Results Now- BRN - (Matokeo makubwa sasa), lakini kwa kweli bila kuangalia maslahi ya walimu itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
BRN kwenye elimu ni zaidi ya mjadala wa daraja sifuri (division 0) na daraja la tano (division 5) kwenye jamii yetu. BRN naikubali kwa asilimia 100, baadhi ya watendaji wa serikali tusikubali kuipotosha dhana hii nzuri kwa wananchi na kudhoofisha juhudi za serikali yetu, badala yake tujielekeze kwenye matatizo ya msingi ya walimu wetu.
RAIMA MWEMA (20/11/2013)


Mwandishi wa makala hii, Mrisho Gambo ni Mkuu wa Wilaya Korogwe, mkoani Tanga na msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu: +255766757575. barupepe; mrishogambo@gmail.com
 
Mkuu naona unafanya usanii kama si usanii basi uwe mkweli daima! Serikali inafahamu fika matatizo ya watumishi wake. Suala la kupandihwa cheo si la waalimu pekee yao ni suala linalohusu watumishi wote wa serikali. Serikali kupitia utumishi haipandishi watumishi madaraja watumishi mfano kuna watu walioajiriwa mwaka 2006 lakin mpaka leo wapo TGSD2 je unategemea nin? Na hapo hawajui hiyo TGSD2 itaenda mpaka lini? Hivi ni vichekesho vya serikali sikivu ya CCM kupitia kwa makatibu wakuu wake na wote hawafanyi kazi wako katika mikutano ya kitaifa na kimataifa. Watumishi wengine wako likizo na ndo maana afisa utumishi hana cha kufanya maana bosi yuko semina.
Mie naona ajabu sana mkuu kupata fursa ya kuandika maneno mengi hivyo na hii inaonesha mkuu huna link/website ya workshop maana wenzio hawaoni matatizo maana muda mwingi wako safarini na katika matamasha mbalimbali. Na hali hii inatishia cheo chako maana hutapata uzoefu ili uendelee kutawala na kuteuliwa tena maana hutafahamiana sana na watu kupitia semina na warsha mbalimbali. Natoa mfano baada ya semina elekezi ya makatibu wakuu pale St. Gaspar Dodoma makatibu walikuja kwa mbwembwe sana kuwa andikeni matatizo yenu na niondoke nayo hasa watumishi wakaao makao makuu Dodoma lakin mpaka leo pamoja na barua ya matatizo kuondoka nayo hakuna kilichofanyika zaidi ya kubadilishwa makatibu wakuu tena. Je ukiandika barua ili upandishwe itaonwa na nani kama aliyeichukua kwa mkono wake mbele ya watumishi ameshindwa hata kujibu kuwa matatizo ya fulan. fulan nk yanashughulikiwa ameshindwa je watumishi wataipenda serikali sikivu ya CCM?. Mie naona usanii mtupu kuanzia juu mpaka chini haiwezekani mtu anakatwa mshahara bila maelezo kisa mbio za mwenge mara michango ya miaka hamsin ya uhuru mara fuko wa rambi rambi mara mfuko wa kusaidia jamii hali mtu hayuko na hao Viongozi (mungu wau) wanaofanya maamuzi ya pesa ya mtu bila kumshirikisha halafu unalazimisha mtu ampende mbabe aliyekata pesa bila hata kunishirikisha. Naona mkuu kwa maneno yako kama yanaleta hasira maana wewe ni mteule wa Rais na je haya hamuongei naye ili mueleze matatizo yaliyoko kwa watumishi? Je huoni kuwa vyanzo vya siri za serikali kuvuja ni manyanyaso ya mtumishi dhidi ya haki zake za msingi? Je wewe kama ni mteule ni kweli uliteuliwa kwa kufaa au kwa hisani? Maana kama uteuzi ungelikuwa ni wa haki mkuu leo hii wakuu wote mngekuwa na sauti ya kusema na kusikika kwa aliyewateua! Ila kwa sababu ni teuzi za kiaina ndo mana leo hakuna na ndo maana nasema hakuna atakaye sema kama wewe ulivyosema maana ni maneno makali mbele ya umma wa wanaodhulimiwa haki zao. Leo wakuu wamekuwa makada wa kukandamiza haki za wananchi ili wageni wanufaike na rasilimali zetu na hakuna hatua zinazochukuliwa ndo maana nasema mkuu nyie hakuna anayeangalia nyendo zenu? Maana kama mteule anakuwa kibaraka wa mwekezaji je watumishi,wasiowatumishi na wananchi kwa ujumla watawapenda? Serikali yetu Viongozi wako katika semina,makongamano ya kimataifa,wengine wanaongoza na meshimiwa nje kujifunza jinsi ya kazi,wengine katika mabaliko ya tabia nchi,wengine kujifunza nje wenzao wanatawala vip na wengine kwenda shoping nje ya nchi, wengine kutabaruku kidogo, wengine kutafuta wawekezaji na kadha wa kadha na watumishi wako likizo isipokuwa waalimu kwa sababu ya kuuza kwao mandazi karanga,icecream na juice, madaktari kuuza kwao dawa, maaskari kuondoa magari barabarani na kuongea madereva, mahakimu kuandaa hati ya dhamana, wanajeshi kufanya mazoezi ya maadhimisho na kulinda mipaka kwa mazoezi ya ndege zao na wakufunzi wa vyuo kuuza compendium zao.
Hiyo ndo hali ya watanzania tuliyokuwa nayo na ni tofauti kabisa huenda na mtazamo wa mkuu wa nchi maana anatoa semina elekezi kumbe ndo anahamisisha semin elekezi kwa waloelekezwa na ndo hawakai ofisin na hata kuzunguka kupata matatizo na kero za walo chin yao. Na wakirudi kwa mkuu wa nchi wanatoa ripoti hali ya kuwa hawakuwepo vituon walikuwa katika semina na workshop na hawajuinin kinafanyika ndani ya ofisi zao.
Mwisho Haki na batili havikai pamoja Allah akusaidie upate wafuasi wa kutambua HAKI ili muwe na sauti moja msaidie wanyonge wanaoudhulimiwa haki zao na watumishi wateule wachache wa serikali sikivu ya CCM.
 
  • Thanks
Reactions: SG8
Mbona yeye wilayani kwake anawachangisha walimu pesa za ujenzi wa shule?
 
Back
Top Bottom