Hatimaye Manchester United na Leicester City wamekubaliana dau la Pauni 80 milioni kwa beki wa kati Harry Maguire.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kufanyiwa vipimo pale Manchester United wikiendi hii.
Anakuwa mchezaji wa tatu kusainiwa katika klabu ya Manchester United katika dirisha hili, wengine wakiwa ni Aaron Wan-Bissaka na Daniel James ambao walitua wakitokea Crystal Palace na Swansea kwa mfuatano huo.
Tangu amejiunga na Leicester City akitokea Hull City mwaka 2017, Maguire amecheza mechi 69.
Usajili huo unamaanisha kwamba Maguire amekuwa beki ghali zaidi duniani akipiku kiasi cha Pauni 75 milioni ambacho Liverpool waliilipa Southampton ili kumnasa Virgil van Dijk Januari, 2018.
United walikuwa wakimtafuta Maguire kwa muda mrefu lakini walishindwa kumnasa miezi 12 iliyopita hiyo ni kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa na dau kubwa zaidi wakati Man United walikuwa tayari kutoa Pauni 70 milioni.