SoC04 Deni la Taifa, Tanzania Linaweza Kupungua Endapo Mifumo ya Maendeleo Itafanyiwa Mageuzi

SoC04 Deni la Taifa, Tanzania Linaweza Kupungua Endapo Mifumo ya Maendeleo Itafanyiwa Mageuzi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Joined
Jul 30, 2022
Posts
321
Reaction score
691
Utangulizi

Kwa miaka ya hivi karibuni, yaani mwaka 2021 hadi sasa, kumekuwa na mijadala mingi kuhusu ongezeko la deni la Taifa. Miongoni mwa makundi yanayohusika na mijadala hii na hata malalamiko ni yale ya Wanazuoni, asasi za kiraia na ya wanasiasa. Mijadala inajikita katika mambo muhimu kama, je kuna umuhimu wa kukopa kiasi hicho?; Matumizi ya mikopo hiyo yana tija? Naamini mijadala hii ni sahihi, kwa sababu ikiwa mikopo imetumika vizuri au vibaya, mlipaji wa mikopo hii pamoja na riba zake ni mwananchi, kupitia tozo mbalimbali za moja kwa moja, na ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali, jambo linalosababisha mfumuko wa bei.
Kwa mujibu wa gazeti la HabariLeo (Juni 13, 2024), deni la taifa limeongezeka na kufikia Sh. Trilioni 91.7 hadi Machi 2024, ikilinganishwa na Sh. Trilioni 77 kwa mwaka jana (2023), hii ni sawa na ongezeko la asilimia 19.1, alisema Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipangi na Uwekezaji. Taarifa inaendelea kusema, deni la ndani lilikuwa Sh. Trilioni 30.7, na deni la nje lilikuwa Sh. Trilioni 60.9.

Kwa nini Deni la Taifa Linaongezeka kila Mwaka?
Gazeti la HabariLeo (Juni 13, 2024) limemnukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiliambia Bunge, jijini Dodoma, ''Ongezeko la deni ilitokana na serikali kuendelea kupokea fedha za mikopo ya zamani na mipya kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji''.

Waziri Kitila Mkumbo, amefafanua kuwa ongezeko la deni lilichangiwa na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha pamoja na kuongezeka kwa riba kwenye mikopo ya nje ambayo riba zake hutegemea mabadiliko ya hali ya soko.

Kwa mtizamo wangu, kama tutaendelea na mfumo tulionao, deni halitakaa lipungue - hasa lile la nje. Tatizo ni kwamba tumerithi mifumo ya kikoloni, ambapo karibu kila kitu kinafanywa na serikali kuu.

Kuna mfumo mzuri wa utawala, yaani hata katika ngazi ya kijiji kuna serikali, lakini serikali kuu ambayo IPO Dodoma, inawajibika kununua chaki kwa ajili ya shule ya msingi iliyopo kijiji kilichopo tarafa ya Kalia, wilaya ya Uvinza, Kigoma. Uvinza ina vyanzo mbalimbali vya mapato ambayo yangeweza kutumika katika taasisi zake zinatoa huduma kwa jamii, kama shule, vituo vya afya na kadhalika, lakini mapato hayo (yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato - TRA), yanapelekwa wizarani, na baadaye zinarudishwa huko (wilayani), aidha kwa kuchelewa au kwa kiasi kisichotosheleza.

Hapa kuna mambo matatu; kwanza, kutokana na ukiritimba wa kukusanya mapato na kuwasilishwa serikali kuu, na baadaye kurudishwa maeneo husika, mara nyingi miradi ya maendeleo inachelewa kutekelezwa; pili, mara nyingi kiasi kinachopelekwa maeneo husika ni kidogo kulipo kile kinachohitajika; na tatu, ukiritimba huu (''bureaucracy''), unachochea mazingira ya ubadhirifu wa fedha.

Mizigo mingi na mikubwa inayobebwa na serikali kuu ni miundombinu ya Barabara, Reli, Viwanja vya Ndege, Umeme na Maji. Maeneo yote haya yanaweza kujiendesha kibiashara, lakini pia yana mamlaka zake, ingawa ni za serikali, lakini zinaweza kuwezeshwa zikashirikiana na sekta binafsi zikajiendesha vizuri bila kutegemea mikopo ya nje kwa kiasi kikubwa. Dhana ya Ushirikiano kati ya sekta za umma na zile za binafsi (yaani PPP - Public Private Partnership) haijazingatiwa vyema.

Serikali Inaweza Kutua Hii Mizigo
Nataka nikupitishe kwenye mifano miwili. Miaka ya 1990, serikali ya awamu ya pili ya rais Ali Hassan Mwinyi (maarufu kama Mzee Ruksa), kulikuwa na mageuzi katika mfumo wa uchumi, uliohusisha ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Utakumbuka, katika kipindi cha awamu ya kwanza na ya pili, mashirika mengi ya umma (hata yale ya uzalishaji) yalikuwa yakipatiwa ruzuku kila mwaka, lengo likiwa ni kulinda ajira za wananchi. Lengo la mageuzi haya lilikuwa kupunguza mzigo kwa serikali kugharamia mashirika yasiyo na faida; na hili lilikuwa moja ya masharti ya mashirika ya fedha ya kimataifa yaliyokuwa yakifadhili mpango huo.

Kampuni ya bia Tanzania (''Tanzania Breweries Limited - TBL''), ilikuwa moja kati ya makampuni yaliyobinafsishwa. Hadi sasa ni miaka zaidi miaka 30 toka TBL imebinafsishwa, inatoa gawio kwa serikali kila mwaka na ni miongoni kwa makampuni yanayoongoza kwa kulipa kodi serikalini. Kipindi hicho, kampuni ya bia ilikuwa moja tu nchini, lakini baada ya ubinafsishaji, kampuni nyingine za bia binafsi (Serengeti na Kibo Gold) zilianzishwa na kuongeza ushindani katika sekta hiyo, jambo lililofanya bidhaa ya bia kupatikana kwa wingi na kwa bei za kishindani. Katika muktadha huu, wigo wa kodi kwa serikali ulipanuka.

Mfano mwingine ni daraja la Mwalimu Nyerere la Kigamboni. Kwa mujibu wa tovuti ya sw.m.wikipedia.org limejengwa kwa gharama ya dola za kimarekani ($) 136 milioni, sawa na shilingi za kitanzania 337.5 bilioni. Daraja lina urefu wa mita 680 na upanda wa mita 27.5. Mradi huu ulianzishwa mwaka 2012 (kipindi cha serikali ya awamu ya NNE ya Mh. Jakaya Mrisho Kikwete) na kuanza kufanya kazi mapema mwaka 2016. Mradi uligharamiwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika Hifadhi ya Jamii (''National Social Security Fund - NSSF''); NSSF ilichangia asilimia 60, na serikali asilimia 40. Mradi huu unaendeshwa kibiashara, ambapo magari yanayotumia daraja hili yanatozwa ushuru, ambapo takriban shilingi milioni 40 zinakusanywa kila siku. Kumbe inawezekana kutekeleza miradi mikubwa kama hii bila kutegemea mikopo kutoka nje yenye masharti lukuki! Serikali ilikuwa na nafasi ya kushirikisha sekta binafsi kuchangia hiyo asilimia 40!

Dira ya 2025 - 2050
Natarajia kuona mageuzi makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa serikali.

Kila mkoa uwe na mamlaka ya kukusanya mapato yake na kuyatumia katika utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo. Hii ina maana gani? Mikoa itaendelea kutumia mamlaka ya mapato (TRA) pamoja na miundombinu yake, lakini mapato yatasalia mkoani, baada ya kutoa kiasi kitakachotumwa serikali kuu.

Miradi ya kimkakati itekelezwe kwa kushirikisha sekta binafsi, serikali ibaki kuwa mwezeshaji na mratibu tu. Kama mradi mkubwa kama ule wa daraja la Nyerere, umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa bila mkopo kutoka nje, basi inawezekana miradi mingine ikafuata mkondo huo.

Serikali iungane na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), katika kampeni ya kutaka nchi zinazoendelea (ikiwemo Tanzania) kufutiwa madeni na taasisi za kifedha za kimataifa.

HITIMISHO
Sekta binafsi nchini zinaweza kutekeleza vizuri miradi mikubwa, endapo itawezeshwa na kushirikishwa na serikali.

Rejea
HabariLeo, Juni 13, 2024; Deni la Taifa Lafikia Trilioni 91.7
Sw.m.wikipedia.org
www.dar24.com
www.news.un.org
 
Upvote 2
Mtindo wa kukusanya mapato kila eneo la nchi yenye watu takriban milioni 62, na kuweka kwenye kapu moja, hufanya wananchi wengi kudhani fedha zinazorudishwa na serikali kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao, ni HISANI, hata kama ni kidogo kuliko mahitaji halisi!!
 
Swala la kupunguza deni la taifa ni la kila MTU. Kila MTU atimize wajibu wake kila siku. Watu wengi nchini, hutegemea karibu kila kitu kutoka kwa watu wachache katika familia zao. Hii ni moja ya sababu za umasikini tulionao, maana wengi hawashiriki katika uzalishaji, bali hushiriki katika matumizi!!
 
Mgogoro wa Kenya, ni matokeo ya mikopo ya IMF, yenye masharti kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuongeza kodi kwa wananchi. Ni vizuri kutambua kuwa taasisi za fedha za kigeni hazijali mustakabali wa wananchi wa nchi husika.
 
Mwaka 1990, na kuendelea serikali ilianza kupunguza watumishi wa umma, wakati huohuo ikisitisha ajira mpya, ikiwa ni pamoja na waalimu na watumishi wa afya (ambao hawajawahi kutosha); hii ilifuatiwa na kufungwa kwa baadhi ya vyuo vya umma vya kati, vikiwemo vya afya, kilimo na ualimu. Huu ulikuwa utekelezaji wa baadhi ya masharti ya mikopo kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa (World Bank na IMF). Ingawa vyuo vilifunguliwa baadaye, athari za utekelezaji wa masharti yale zipo hadi Leo, ikiwa imepita miaka takriban 34.
 
Mwaka 1990, na kuendelea serikali ilianza kupunguza watumishi wa umma, wakati huohuo ikisitisha ajira mpya, ikiwa ni pamoja na waalimu na watumishi wa afya (ambao hawajawahi kutosha); hii ilifuatiwa na kufungwa kwa baadhi ya vyuo vya umma vya kati, vikiwemo vya afya, kilimo na ualimu. Huu ulikuwa utekelezaji wa baadhi ya masharti ya mikopo kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa (World Bank na IMF). Ingawa vyuo vilifunguliwa baadaye, athari za utekelezaji wa masharti yale zipo hadi Leo, ikiwa imepita miaka takriban 34.
Kinachotokea kenya ni result of what will happen pale hapatapo kuwa na control kwenye mikopo ya nchi, else 1990 itajirudia tena na athari zitakuwa kubwa mno
 
Back
Top Bottom