CM 1774858
JF-Expert Member
- May 29, 2021
- 5,621
- 5,029
Chongolo: Wasaliti wafukuzwe CCM.
Imeelezwa kuwa usaliti ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiyo chanzo kikubwa cha matokeo mabaya kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, huku akiagiza wote watakaobainika kwa usaliti wafukuzwe.
Alisema usaliti jeshini adhabu yake ni kifo, lakini kwenye chama msaliti anapaswa kufukuzwa kwa kuwa uwepo wake ndani ya chama ni hasara kuliko kuondoka kwake.
“Uwepo wa msaliti ndani ya chama ni hasara kubwa kuliko kuondoka kwake, tuna uhakika gani amejirekebisha, maana haiwezekani mtu anapogombea nafasi akikosa anataka chama chote kianguke, hakuna jina kubwa zaidi ya chama.
“Lazima tubadilike tujue jambo la chama ni la kufa na kupona, tutambue usaliti ni dhambi kubwa kuliko dhambi nyingine,” alisema Chongolo.
Chongolo alikumbushia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, akieleza wingi wa watu waliokuwepo kwenye mikutano na matokeo ni vitu tofauti, hali iliyoonyesha dhahiri kulikuwa na usaliti mkubwa.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, CCM ilipata majimbo mawili, la Mwanga na Same Magharibi, huku saba yakinyakuliwa na upinzani.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 CCM iliweka historia ya kunyakua majimbo yote ya uchaguzi, ikiwemo la Moshi Mjini ambalo limekuwa chini ya upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995.
Mbali na Moshi mjini, majimbo mengine ambayo yamekuwa na upinzani mkubwa ni jimbo la Hai anakotoka Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Jimbo la Vunjo ambako wanatoka Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa, James Mbatia na Mwenyekiti wa TLP Agustino Lyatonga Mrema.
Kitendo cha CCM kushinda majimbo yote katika uchaguzi mkuu 2020 kumefanya Mkoa huo kuonekana umetulia na viongozi wa chama hicho kutaka hali hiyo iendelee hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Uchaguzi ndani ya chama
Chongolo, ambaye ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani humo, alisema katika uchaguzi ndani ya chama, wanahitajika viongozi watakaokipigania chama kufa na kupona, ili kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Pia aliwataka wanachama wa chama hicho mkoani humo, kutofanya makosa katika chaguzi hizo zinazoendelea kwa kuchagua viongozi watakaoutuliza mkoa huo na kuwavusha katika uchaguzi wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
“Mkoa wa Kilimanjaro huko nyuma ulikuwa ukitusumbua sana, kulikuwa na changamoto za migogoro asubuhi, mchana na jioni, sasa hivi umetulia, endeleeni kuwa na viongozi ambao watautuliza, msifanye makosa, chagueni kwa nidhamu na msikate majina ya wagombea kwa masilahi binafsi,” alisema Chongolo.
“Viongozi mliopo acheni kutengeneza safu na makundi kwa ajili ya maslahi yenu binafsi, acheni wananchi na wana CCM waamue nani awaongoze, tusidanganyane, tuepuke rushwa, ukiona kiongozi anakupa shekeli ili kukushawishi umchague, hafai kwa sababu uongozi haununuliwi, unatolewa na Mwenyenzi Mungu na akikupangia wewe kuwa kiongozi hakuna wa kukukwamisha kwenye hilo, wekeni msukumo kwa watu ambao wanahangaika na shughuli za wananchi kutoka ndani ya mioyo yao, wanawasemea wananchi hata kama si viongozi,” alisema.