Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi (IPOA) imechukua hatua kufuatia kukamatwa na madai ya kushambuliwa kwa mwandishi wa Citizen TV, Francis Ode, wakati akiripoti maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta jijini Nairobi.
Soma Mwanahabari wa Citizen TV akamatwa na Polisi akiwa kazini wakati wa Maandamano Nairobi
IPOA inatarajiwa kuwahoji zaidi ya maafisa saba wa polisi ili kubaini mazingira ya tukio hilo, lililotokea Jumanne, Oktoba 20, 2026, katika eneo la Central Business District (CBD).
Wanaotarajiwa kuhojiwa ni pamoja na OCPD wa Central Police Station, Patrick Gogo, OCS Joab Onyapidi na maafisa watano wa vyeo vya chini wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja katika kumkamata mwanahabari huyo.
Ode alikuwa akiripoti maandamano yaliyohusishwa na kupinga kupanda kwa bei ya mafuta jijini Nairobi alipokamatwa na maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia kiraia. Mwanahabari huyo amesema alijitambulisha mara kadhaa kuwa ni mwandishi wa habari aliyekuwa kazini, lakini maafisa hao waliendelea kumkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Central.
Aidha alidai kuwa alifanyiwa ukatili wakati wa kukamatwa kwake, ikiwemo kuvutwa na kuharibiwa kwa nguo zake. Ode aliachiliwa baadae bila kufunguliwa mashtaka. Hata hivyo, kuachiliwa kwake hakujamaliza maswali kuhusu sababu za kukamatwa kwake na namna alivyotendewa.
Tukio hilo limekosolewa na mashirika ya wanahabari, yakiwemo Kenya Editors Guild na Crime Journalists Association of Kenya, ambayo yametaka uchunguzi huru na uwajibikaji kwa maafisa wowote watakaopatikana kukiuka sheria.
Mjadala huu unagusa Ibara ya 34 ya Katiba ya Kenya inayolinda uhuru wa vyombo vya habari, pamoja na umuhimu wa kuhakikisha wanahabari wanaweza kuripoti matukio ya umma bila kukumbana na vitisho au ukatili wanapotekeleza majukumu yao.
Je, kuwahoji maafisa saba wa polisi kutatosha kuhakikisha uwajibikaji katika kesi ya Ode Francis, au IPOA inapaswa pia kuweka wazi matokeo ya uchunguzi na hatua zitakazochukuliwa?
Na Je, wanahabari wanawezaje kulindwa wanaporipoti maandamano na matukio mengine nyeti kwa umma?