Katika maisha ya ibada, mahubiri na mafundisho ni nguzo kuu za kukuza imani na kuwaelekeza waumini jinsi wanavyopaswa kuishi au kuenenda. Hata hivyo, muziki wa kwaya hutoa ladha ya kipekee inayogusa moyo moja kwa moja, mahali ambapo maneno pekee hayawezi kufika. Ibada bila nyimbo za kwaya ni kama chakula kisicho na chumvi. Kinajaza tumbo lakini hakiburudishi.
Nyimbo za kwaya huamsha hisia za kiroho, huleta mshikamano miongoni mwa waumini, na kuwasaidia watu kumkaribia Mungu kwa namna ya kipekee. Ndio sababu Mwimbaji wa Zaburi 100:2 anatuhimiza akisema: "Mtumikieni Bwana kwa furaha; njoni mbele zake kwa kuimba." Huu ni ushahidi kuwa ibada ya kweli hujumuisha pia nyimbo za sifa.
Zaidi ya hayo, kwaya huwafundisha waumini Neno la Mungu kwa njia ya nyimbo, hufariji waliovunjika moyo, na hufungua mioyo ya watu kupokea ujumbe wa Neno linalohubiriwa. Muziki hubeba uzito wa mafundisho kwa namna inayodumu muda mrefu akilini, hata baada ya ibada kuisha. Ndio sababu watu wanaweza kukumbuka zaidi wimbo fulani wa kwaya kuliko mahubiri.
Kwa hiyo, dini isiyojumuisha muziki wa kwaya katika ibada zake sio tu kwamba inakosa uhondo, bali pia inakosa njia mojawapo muhimu ya kugusa roho za watu na kulisambaza Neno kwa namna yenye ushawishi wa kina. Namshukuru Mungu aliyenifunulia mapema umuhimu wa kuwa miongoni mwa Wakristo. Ibada za Wakristo zinaburudisha mwili, nafsi na roho. Ni uhondo usio na kifani. Zaidi ya yote, tukifika mbinguni, tutakuwa na kazi moja tu: kuimba na kumsifu Mungu, bila jasho!