SoC02 Dini na athari zake hasi katika uchumi wa jamii na taifa na namna ya kuzikabili

SoC02 Dini na athari zake hasi katika uchumi wa jamii na taifa na namna ya kuzikabili

Stories of Change - 2022 Competition

Ndu o Ruwa

New Member
Joined
Sep 10, 2022
Posts
1
Reaction score
1
Utangulizi
Tanzania ni nchi isiyokuwa na dini, lakini watu wake wana dini. Hili ni jambo zuri kwani katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia wapo wengi ambao hawaoni tena umuhimu wa dini maishani mwao. Licha ya hilo, zipo athari nyingi hasi za wazi na zisizo za wazi zinazoweza kuathiri Uchumi wa weambazo huathiri waamini wa dini husika, jamii na Taifa kwa ujumla.

Nikiwa kama muumini Mkristo, nitatumia zaidi dini ya Ukristo kama ‘case study’ yangu kuelezea ‘Story of Change’ niliyoipa jina la Dini na Athari Zake Hasi katika Uchumi wa Jamii na Taifa, na Namna na Kuzikabili.” Pia, mwishoni nitatoa mapendekezo yangu kwa ufupi na hitimisho.

Zifuatazo ni athari hasi za Kiuchumi zitokanazo na dini kwa Jamii na Taifa letu;

Kwanza, Suala la Michango; hili ni jambo la hiyari na tendo la kiimani, lakini michango katika makanisa mengi imekuwa mingi. Yapo hata makanisa ambayo yameweka viwango vya chini vya sadaka mfano shilingi 5,000/= au hata juu zaidi. Kwa Mtanzania wa kipato cha chini, kutoa kiasi hicho au cha juu zaidi hasa unapowekewa kima cha chini, tayari inaathiri kipato chake cha Kiuchumi.

Katika hii michango pia, naweza kuzungumzia juu ya vitu ambavyo waamini hawa wamekuwa wakiuziwa makanisani ili kwamba wakivitumia watapate miujiza maana vina ‘upako’. Vipo vitu kama vile mafuta, chumvi, maji na vitambaa vya leso. Vyote hivi huwa wanavinunua kwa gharama kubwa, hivyo kuathiri pia uchumi wao!

Pili, Uvivu; huu upo kwa baadhi ya waamini wa makanisa haya. Uvivu huu unatokana na ahadi ambazo waamini wengi wanahaidiwa katika mikusanyiko yao ya kiimani kwa jina la miujiza. Mara nyingi tumeona katika mikusanyiko kama hiyo watu wakiahidiwa na wahubiri wao vitu mbalimbali kama nyumba, magari, vyeo kazini, viwanja nakadhalika bila kufanya kazi. Matokeo yake ni kuendekeza uvivu wa kutokufanya kazi kwa bidii, kukosa kipato kwa kutokufanya kazi, hivyo kupelekea uchumi wa familia, jamii na taifa kuzidi kuzorota.

Tatu, Matumizi Mabaya ya Muda; waamini wengi katika makanisa haya hutumia muda wao mwingi katika nyumba za ibada na mikutano ya injili kuliko kufanya kazi au kubuni njia za kujikwamua kiuchumi. Siku hizi ipo mikutano mingi inayojulikana kwa jina la mikutano ya Injili, pia ipo mikesha kwa waamini hawa. Kwa wengi wanaoshiriki, wanaishia tu kusali siku nzima, au hata siku tano kwa wiki. Muda huo wangeweza kuutumia vizuri, kusali kwa kiasi na kufanya kazi kwa bidii, wangeweza kuzalisha kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi. Katika Uchumi, muda ni mali.

Nne, Mikopo Isiyolipika; Wapo waumini wengi wanaokabiliwa na mikopo mikubwa ya benki na hata ya watu binafsi ambapo chanzo cha wao kukopa kwao ni kwa ajili ya michango kanisani lakini pia ile hamu na tamaa ya kuwa na vitu vya kifahari walivyoahidiwa kwenye maombi kwamba watavipata. Kwa mfano, Mtu anatoa ushuhuda kwenye nyumba ya ibada kwamba aikuwa hana gari au nymba au kiwanja, lakini alipokuja kwenye maombi akapata gari, lakini ukiendelea kumuuliza alipataje, atakuambia, alikopa. Mikopo hii imekuwa mzigo kwao na familia zao kulipa, na hivyo kuendelea kudidimiza uchumi wa familia zao na jamii kwa ujumla.

Tano, Migogoro ya Ndoa na Familia; Hii inatokana na sababu zilizotajwa hapo juu, kwamba endapo mfano, mama wa familia anatumia muda mwingi katika mambo ya ibada bila kujali kukaa na familia yake, kuna uwezekano mkubwa wa familia kukosa amani na kuingia kwenye migogoro ya kila mara. Ni hakika kwamba, endapo familia ina mgogoro, hata uchumi wa familia husika utayumba kwa sababu hakutakuwa na amani hata katika utafutaji.

Sita na mwisho, Kelele za vifaa vya muziki na vipasa sauti kutoka katika maeneo ya ibada, hasa nyakati za usiku, hufanya hata wale wasio waumini kutokulala vizuri. Ninaamini kwamba, iwapo mtu atakosa usingizi wa kutosha sababu ya kelele hizi hasa za usiku, hata akienda kazini siku inayofuata hawezi kufanya kazi kwa ufasaha maana hakulala vizuri usiku. Hii inaweza kuhatarisha shughuli zake za uzalishaji wa kiuuchumi.

Mapendekezo ya Kukabiliana na athari hizi hasi za kiuchumi;

Kwanza
, taasisi za kidini zizidi kuboresha zile athari chanya za kiuchumi zinazoweza kupatikana ndani yake kama vile; utoaji wa mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu kwa waumini wa dini husika kutoka katika taasisi za kifedha za dini zao.

Pili, Kuwe na semina mbalimbali za Ujasiriamali za kila mara kwa waamini wa kanisa husika kutoka wataalamu wa uchumi.

Tatu, taasisi za kidini pia ziwe na malengo ya kuwa na miradi ya muda mrefu ili kujiendesha kiuchumi na si kutegemea tu michango ya waamini wao. Zinaweza kubuni miradi mikubwa au midogomidogo ya kiuchumi ambayo itasaidia taaasisi zao za kidini kujiendesha zenyewe. Pia hili litasaidia kuzalisha ajira kwa waamini wake.

Nne, watu waendelee kuwa na uhuru wa kuabudu, huku wakijaribu kutumia Fikra zao na Imani yao kwa pamoja juu ya kile wanachokiamini na si kukubali tu kuwa watu wa imani, bali imani yenye matendo kwa kazi zao za kila siku.

Tano, Watu wafanye kazi kwa bidii huku wakiwa na imani zao, na si kutegemea tu miujiza ya utajiri bila kufanya kazi kwani hata Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Asiyefanya Kazi na Asile” (2Wathesalonike 3:10).

Sita, serikali iangalie tena suala la vibali vya kufungua makanisa, ili kuepusha watu kufanya makanisa kama mradi wa kibiashara. Ikiwezekana, hata iangalie viwango vyao vya elimu hasa ile inayohusiana na mambo ya kidini yaani Teolojia.

Mwisho, kuhusu kelele kubwa za vyombo vya muziki zinazotoka kwenye baadhi ya sehemu za ibada, mamlaka katika maeneo ya nyumba za ibada wajitahidi kudhibiti kwa namna inayofaa sauti. Njia hizo ni kama vile kutumia sauti inayowatosha tu waumini waliopo kwenye eneo la ibada au ikibidi watumie vizuia sauti.

Hitimisho, Ni imani yangu kwamba hii “story of change, italeta mabadiliko chanya kwa jamii yote ya Watanzania watakaoisoma kwa jicho la kipekee, na kuyafanyia kazi yale niliyoyaeleza. Ni imani yangu pia kwamba, watu wataendelea kuwa na mtazamo chanya juu ya dini zao na hivyo kutambua jinsi ya kuhusianisha imani zao za kidini na kazi zao hivyo kuleta tija kwao na kwa taifa.

Ninaomba Sana Uipigie Kura Makala hii Endapo Utavutiwa nayo.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom