Dk. Ashatu Kijaji: Wananchi msitupe majokofu ya zamani

Dk. Ashatu Kijaji: Wananchi msitupe majokofu ya zamani

Dalton elijah

JF-Expert Member
Joined
Jul 19, 2022
Posts
373
Reaction score
829
Serikali imewataka wananchi kuepuka kutupa majokofu ya zamani na vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni au kuongeza joto duniani. Aidha, wananchi wanashauriwa kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vya zamani.

Hayo yamesemwa leo, Septemba 14, 2024, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijaji, wakati akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, ambayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 16, 2024.

Pia soma: Punguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia hatua za kibinafsi

Dk. Kijaji alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itatoa elimu kwa mafundi wa viyoyozi na majokofu katika jiji la Dodoma kuhusu njia bora za kukarabati vifaa hivyo bila kuachia kemikali angani. Pia, elimu itatolewa kwa umma kupitia makala mjongeo kuhusu umuhimu wa kulinda Tabaka la Ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alieleza kuwa Tabaka la Ozoni linapoharibiwa, linaachia mionzi ya jua kufika kwenye uso wa dunia, hali inayosababisha magonjwa kama saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, na matatizo ya kinga mwilini. Kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni zinatokana na majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, na matumizi mengine.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni ni "Itifaki ya Montreal: Kupunguza Athari za Mabadiliko ya Tabianchi," ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kuhusu mchango wa Itifaki ya Montreal katika hifadhi ya Tabaka la Ozoni na jitihada za kupunguza mabadiliko ya tabianchi.

MtanzaniaDigital
 
Back
Top Bottom