Copy and paste :
𝗕𝗔𝗟𝗢𝗭𝗜 𝗡𝗖𝗛𝗜𝗠𝗕𝗜 𝗔𝗠𝗘𝗥𝗨𝗗𝗜𝗦𝗛𝗪𝗔 𝗡𝗬𝗨𝗠𝗕𝗔𝗡𝗜, 𝗞𝗪𝗔 𝗡𝗜𝗡𝗜 𝗕𝗔𝗗𝗢 𝗬𝗨𝗣𝗢 𝗠𝗜𝗦𝗥𝗜?
Na Abbas Mwalimu
(0719258484)
Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023.
Taarifa ya vyombo vya habari ya Alhamisi tarehe 28 Septemba 2023, ilimuonesha Balozi wa Tanzania nchini Misri, Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa ameambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro na Rais wa TFF, Wallace Karia, waliwa na kikosi cha Singida Big Stars nchini Misri.
Wadau wengi wa masuala ya diplomasia wamekuwa wakiuliza maswali kuwa, inakuwaje kwamba Balozi Dkt. Nchimbi amerejeshwa nyumbani lakini bado anaonekana yupo nchini Misri?
Ikumbukwe kuwa, taarifa ya Ikulu Mawasiliano ya tarehe 11 Agosti 2023, ilionesha kuwa Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo aliyekuwa kituo cha Rwanda amehamishiwa kituo cha Cairo nchini Misri, akichukua nafasi ya Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye kwa mujibu wa taarifa hiyo amerudishwa nyumbani.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa Balozi Meja Jenerali Ramson Godwin Mwaisaka ambaye kabla ya kuapishwa kwake alikuwa Balozi Mteule, anakwenda nchini Rwanda kuchukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo ambaye amehamishiwa nchini Misri.
Kutokana na sintofahamu hiyo, mimi Abbas Mwalimu , kama mwanataaluma wa masuala ya siasa za kimataifa na kidiplomasia nimeona ipo haja ya kulifafanua jambo hilo kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Uhusiano wa Kidiplomasia.
Kimsingi, Balozi huweza kurudishwa nyumbani (recall) kwa sababu kadhaa zikiwemo:
(i) Kuumwa na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo majukumu yake yatatekelezwa na chargé d’affaires ad interim kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 19
(ii) Kuisha kwa muda wa utumishi (mission) katika nchi aliyotumwa
(iii) Kuhitajiwa nyumbani kwa majukumu mahususi ya kimkakati
(iv) Kufariki kwa Balozi husika
(v) Kutohitajiwa na nchi iliyompokea endapo ametenda kosa katika nchi iliyompokea kwa mujibu wa ibara ya 41 (1) ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Uhusiano wa Kidiplomasia.
Katika sura ya kipekee, ni vema ifahamikke kuwa kurejeshwa nyumbani kwa Balozi si kitendo cha dakika moja, labda itokee Balozi husika ameenenda kinyume na Ibara ya hiyo 41, ibara Ndogo ya Kwanza ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, ambayo inawakataza mabalozi kuingilia mambo ya ndani ya nchi zilizowapokea.
Katika muktadha huo, endapo Balozi ataenenda kinyume na Ibara hiyo ya 41(1) basi nchi iliyompokea Balozi husika itaijulisha nchi iliyomtuma Balozi tajwa kuwa mtu huyo hakubaliki (persona non grata) katika nchi iliyompokea.
Nchi iliyompokea itafanya hilo kwa kutuma waraka wa kidiplomasia (demarche) kwa kuzingatia Ibara ya 9 ibara Ndogo ya Kwanza na ya Pili za Mkataba huo wa Vienna wa mwaka 1961.
Kwa kuzingatia taarifa ya Ikulu ya tarehe 11 Agosti 2023, ni wazi kuwa muda wa 'mission' ya Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi nchini Misri umeisha.
Hapa ndipo msingi wa ufafanuzi wangu unapokuja. Kikanuni ni kwamba, Balozi hukabidhiwa 'Hati ya Utambulisho' (Letter of Credence) wakati akielekea kwenye kituo alichopangiwa.
Hati hiyo ya Utambulisho huandikwa na Rais wa Nchi iliyomtuma Balozi husika kwamba, "Mimi Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimemteua ... na ninamtuma kwako kuwa mwakilishi wangu..."
Hati hiyo humuelezea aliyetumwa na Rais, kwa majina yake, wasifu wake na mwisho wa uwakillishi wake katika nchi aliyotumwa.
Aidha, licha ya kukabidhiwa Hati ya Utambulisho, Balozi husika hukabidhiwa Hati ya Kurejeshwa Nyumbani (Letter of Recall) ya mtangulizi wake.
Balozi husika hupangiwa siku maalumu ya kwenda kuwasilisha Hati ya Utambulisho. Siku hiyo atakayowasilisha Hati ya Utambulisho huwasilisha sambamba na Hati ya Kurejeshwa Nyumbani ya mtangulizi wake.
Kwa nini, Balozi hukabidhiwa Hati ya Kuitwa Nyumbani ya mtangulizi wake?
Jibu ni kwamba, kwa mujibu wa Ibara ya Kwanza ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Uhusiano wa Kidiplomasia, Mkuu wa Kituo (Head of Mission) ni mmoja tu, hivyo Balozi anayeenda kwenye kituo hukabidhiwa Hati ya Kurejeshwa Nyumbani kwa mtangulizi wake kwa sababu yeye ndiye mkuu mpya wa kituo.
Kadhalika, kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 196, kitendo cha Balozi (Mkuu wa Kituo) kuwasilisha Hati za Utambulisho hutafsiriwa kuwa ameanza majukumu yake. Kama ni hivyo, inawezekana vipi kuwa na mabalozi wawili katika kituo kimoja?
Hapa ndipo ilipo sababu ya kwa nini Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amebaki Misri.
Maana yake hapa ni nini? Ni kwamba, huwezi kuwa na mabalozi wawili ndani ya kituo kimoja.
Hivyo ni lazima wapishane airport, mmoja akiwa anaingia mmoja anatoka.
Tukumbuke kuwa, Balozi Meja Jenerali Makanzo anabadilishana kituo na Balozi Meja Jenerali Mwaisaka.
Lakini tukumbuke kuwa, Balozi Meja Jenerali Mwaisaka ambaye amepangiwa kituo cha Rwanda, ambaye ndiye anapaswa kubadilishana kituo na Balozi Meja Jenerali Makanzo, amemaliza mafunzo yake Chuo cha Dkt. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations hivi karibuni.
Huo ni utaratibu wa kawaida wa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa kila Balozi anayeteuliwa na kula kiapo cha Ubalozi, hupaswa kupelekwa Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Kurasini, ili kupitishwa katika maslahi mahususi ya taifa na diplomasia kwa ujumla.
Baada ya kumaliza mafunzo mabalozi wote hutakiwa kuwaaga viongozi wa kitaifa.
Hapa ina maana kwamba, mabalozi akiwemo Balozi Meja Jenerali Mwaisaka, watapaswa kuwaaga kwa mtiririko kwenda juu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010 na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, watapaswa kuwaaga Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hatimaye Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa kuzingatia kuwa Balozi Meja Jenerali Makanzo aliyepo Rwanda ndiye anapaswa kubadilishana kituo na Balozi Meja Jenerali Mwaisaki.
Aidha, kwa kuzingatia kuwa mabalozi kukutana na viongozi wa kitaifa hutegemea na ratiba za viongozi hao wa kitaifa zinavyoruhusu.
Hivyo, si rahisi kituo (Ubalozi) kukiacha pasina kuwepo na Mkuu wa Kituo kwa muda wote huo ingawa Charge d Affaires ad interim au hata En Titre huweza kukaimu kwa nyakati fulani kutegemea na mazingira ya nchi aliyotumwa Balozi.
Katika muktadha huo itampasa Balozi aliyeitwa nyumbani (Recalled) yaani Dkt.Emmanuel Nchimbi abaki kwenye kituo mjini Cairo, Misri mpaka pale Balozi Meja Jenerali Mwaisaka atakapomaliza kuaga viongozi wote wa kitaifa na kuanza safari ya kuondoka kuelekea kituoni Kigali, Rwanda kubadilishana na Balozi Meja Jenerali Makanzo.
Pia, hapo ndipo Balozi Meja Jenerali Makanzo atakapokwea ndege na kuelekea Cairo, huku Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akikwea ndege kurudi Tanzania.
Kimsingi kanuni inazuia watatu hao kukutana katika vituo vya kazi. Hivyo watapishana hewani.
Kwa msingi huo, Balozi Dkt. Nchimbi atabaki kituoni Cairo, Misri mpaka pale Balozi Meja Jenerali Makanzo atakapokwea ndege kuelekea Misri akipishana na Balozi Meja Jenerali Mwaisaka. Kwa kifupi watapishana angani.
Hivyo kuwepo Misri kwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ni katika kusubiri utaratibu huo.
Wenu:
Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse)
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).