Dunia inamwombolezea Jane Goodall, mwanasayansi maarufu wa etholojia, tabia za wanyama na mhifadhi, aliyefariki Jumatano akiwa na umri wa miaka 91. Utafiti wake wa awali katika Mbuga ya Taifa ya Gombe nchini Tanzania ulibadilisha mtazamo wa kisayansi kuhusu sokwe na kusaidia kuibua harakati za kimataifa za utunzaji wa mazingira.
Goodall aliwasili magharibi mwa Tanzania mwaka 1960, akiwa mtafiti mchanga mwenye umri wa miaka 26, ambapo wakati huo hakuwa na mafunzo rasmi ya kisayansi lakini alikuwa mdadisi asiyetosheka kuhusu ulimwengu wa asili. Kazi yake kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika ilisababisha uvumbuzi ambao uliondoa imani za muda mrefu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya zana za sokwe mtu, uhusiano tata wa kijamii, na akili ya kihisia ambayo wakati fulani ilidhaniwa kuwa ya wanadamu pekee.
“Jane Goodall alikuwa mwanzilishi wa uhifadhi ambaye alileta mapinduzi makubwa katika uelewa wetu kuhusu sokwe mtu,” alisema Godwell Ole Meing’ataki, kamishna msaidizi wa uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. "Kazi yake ilichangia kwa kiasi kikubwa uhifadhi nchini Tanzania na kuhamasisha vizazi duniani kote."
Mwandishi wa habari za mazingira Deogratius Mfugale alibainisha kuwa urithi wa Goodall unavuka elimu ya tabia ya wanyama. “Alitoa picha kubwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili viumbe hai vyote viweze kustawi,” alisema.
Shirika la Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira (WWF) Tanzania lilitilia mkazo maoni hayo. "Kujitolea kwake katika maisha yote kwa ajili ya binadamu, wanyamapori, na bayoanuwai kumehamasisha vizazi na kubadilisha jinsi ulimwengu unavyoelewa uhifadhi," alisema Amani Ngusaru, mkurugenzi wa WWF nchini Tanzania.
Uchunguzi muhimu wa Goodall, kuanzia tabia ya kuwinda sokwe mtu hadi uwezo wao wa kuwa na huruma, uliweka msingi wa elimu ya kisasa ya tabia za wanayama na kuathiri nyanja mbalimbali kama vile afya ya binadamu, ikolojia na biolojia ya mabadiliko.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi ya Jane Goodall, ugunduzi wake maarufu zaidi, kwamba sokwe hutumia zana, ulisifiwa kama wakati "uliofafanua upya wanadamu,"
Ikianzishwa na Goodall mwenyewe, taasisi hiyo imekua nguvu ya kimataifa ya uhifadhi, maendeleo ya jamii, na uwezeshaji wa vijana. Kazi yake inaendelea kuakisi imani yake kwamba kulinda asili hakuwezi kutenganishwa na kuinua watu.
"Matokeo ya Jane pia yaliathiri nyanja za afya ya binadamu, mabadiliko, na ikolojia. Shauku yake na werevu vilimfanya Jane kuwa mtu maarufu wa pekee katika mawazo ya kisayansi na kifalsafa," taasisi hiyo ilisema.
"Maisha na kazi ya Goodall sio tu yaliweka alama isiyoweza kufutika katika uelewa wetu wa sokwe mtu na viumbe vingine, bali pia kwa binadamu na mazingira ambayo sote tunashiriki," iliongeza taarifa hiyo.
Taasisi hiyo ilithibitisha katika taarifa hiyo kuwa Goodall alifariki dunia mjini Los Angeles alipokuwa kwenye ziara ya kutoa mihadhara nchini Marekani.
Wakati Tanzania inapomuenzi rafiki yake mpendwa na ulimwengu unapoakisi urithi wake, Goodall ataendelea kukumbukwa si tu kama mwanasayansi bali pia mtu mwenye maono ambaye huruma na ujasiri vilitengeneza upya uhusiano wa binadamu na ulimwengu wa asili.