Dkt. Mashingo: Hakiki taarifa za Afya ya Uzazi unazoziona mtandaoni kabla ya kuziamini

Dkt. Mashingo: Hakiki taarifa za Afya ya Uzazi unazoziona mtandaoni kabla ya kuziamini

News Tz1

Member
Joined
Nov 28, 2025
Posts
82
Reaction score
110

Dkt. Mashingo Lerise kutoka Marie Stopes Tanzania (MSI) ametoa wito kwa jamii, hususan vijana, kuwa makini na taarifa za afya ya uzazi wanazokutana nazo kwenye mitandao ya kijamii. Amesisitiza umuhimu wa kuhakiki taarifa hizo kabla ya kuziamini ili kuepuka taarifa zinazopotosha na zisizo na ukweli.
IMG_2684.jpeg

Akichangia mjadala ambao umeendeshwa na Mratibu wa afua za Vijana na Ujumuishaji wa Makundi maalum, Denice Simeo kuhusu Afya ya Uzazi na Ustawi wa Vijana, uliofanyika Agosti 11, 2026, jijini Dodoma katika kongamano kuelekea maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, Dkt. Mashingo amesema kuwa mitandao ya kijamii imejaa taarifa mbalimbali kuhusu afya ya uzazi, lakini baadhi yake hazina ukweli wa kutosha.
IMG_2683.jpeg

Amesema ni muhimu mtu anayekutana na taarifa kuhusu afya ya uzazi mtandaoni kuanza kwa kujiuliza kuhusu chanzo cha taarifa hiyo na iwapo anayetoa taarifa ana uelewa au utaalamu unaohusiana na jambo analolizungumzia.

“Mtu anayejua anatoa taarifa kwa lengo la kuelimisha. Kwa mfano, Instagram kuna watu wanatag, kwa mfano Wizara ya Afya au Wizara ya Vijana. Kwa hiyo, unaposoma taarifa hiyo, angalia nani ameshirikishwa na aina ya watu wanaomfuatilia. Lakini pia angalia sana mtu anayekupa taarifa halafu anakusisitiza kununua kitu, kwa sababu wengi wao wanakuwa wanafanya biashara,” amesema Dkt. Mashingo.

Aidha, Dkt. Mashingo amesema kumekuwepo na ushauri unaotolewa kwenye mitandao ya kijamii ambao unaweza kuwapotosha vijana na kusababisha athari mbalimbali. Amewataka vijana wa kiume na wa kike kuwa waangalifu wanapofanya maamuzi kuhusu matumizi ya bidhaa au huduma zinazohusiana na afya ya uzazi.

Akijibu hoja ya kijana mmoja kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, Dkt. Mashingo amesema ni kweli changamoto zinaweza kujitokeza, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha mtu anapata ushauri na huduma kutoka kwa mtaalamu aliyefundishwa, pamoja na kuendelea kuwa karibu na wataalamu baada ya kupata huduma.
IMG_2685.jpeg

“Unapoenda kuchukua njia ya uzazi wa mpango kwa mtu ambaye amefundishwa na ambaye ni mtaalamu, kuna vitu ambavyo ni lazima avifanye. Kwanza, lazima achukue historia yako ya afya na mahusiano, kisha akufanyie uchunguzi wa kiafya ili kujua ni njia ipi inayokufaa. Baada ya kukupa huduma, ataenda mbali zaidi kwa kukupa mfumo wa kurudisha taarifa endapo utapata changamoto,” amesema.

Taarifa sahihi bado ni changamoto kwa vijana

Kwa upande wake, Dkt. Mariam Ngaeje kutoka UNFPA amesema upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi bado ni changamoto inayowaathiri vijana katika masuala muhimu ya afya ya uzazi.

Amesema kuna umuhimu wa kuwa na programu zinazolenga kueneza taarifa sahihi za afya ya uzazi kwa vijana, pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana.

“Changamoto iliyopo ni taarifa. Jambo lingine bado tuna changamoto ya mazingira wezeshi kwa vijana. Kwa Tanzania, ni asilimia 69 ya vituo vya afya vinavyotoa huduma rafiki kwa vijana. Jambo lingine, hatuna programu zinazowalenga vijana balehe, hasa wa kiume. Tumewekeza sana kwenye vijana wa kike; tunawajengea uwezo na kuwapa fursa, lakini tumewaacha nyuma vijana wa kiume,” amesema Dkt. Mariam.

Naye kijana David Mwafura, ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wa mjadala huo, amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi, hususan katika maeneo ya vijijini.

“Sisi vijana wengi wa Kitanzania hatuna taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi. Mazingira ya vijijini ndiyo yanaathirika zaidi,” amesema.
IMG_2601.jpeg

IMG_2688.jpeg
Amesema mara nyingi vijana hukutana na kikwazo cha kutokujua wapi wanapoweza kupata taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi. Kwa msingi huo, ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kutafuta taarifa kutoka kwa wataalamu badala ya kuamini kila taarifa wanayoiona kwenye mitandao ya kijamii.

Serikali yawataka vijana kutoipuuza afya

Awali, akizungumza kabla ya mjadala huo, Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya vijana alisisitiza umuhimu wa kulipa uzito suala la afya kwa kuwa ni msingi wa maendeleo mengine katika maisha ya vijana.

“Ninawaomba msipuuze afya zenu kwa sababu ya harakati za maisha. Ndoto inahitaji mwili na akili yenye afya. Kijana akipitia msongo wa mawazo, huzuni inayodumu, hofu, matumizi ya dawa za kulevya, shinikizo rika au changamoto ya afya ya uzazi, asiogope kuomba msaada. Kuomba msaada si udhaifu,” alisema.
IMG_2687.jpeg

Maadhimisho hayo yanafanyika jijini Dodoma na yamewakutanisha zaidi ya vijana 1,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Yameandaliwa na wadau mbalimbali, ikiwemo Marie Stopes International (MSI) na Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya vijana.
 
Back
Top Bottom