27 June 2021
Tanga, Tanzania
MKUTANO MKUU WA BARAZA LA BAKWATA
Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt Philip Isdor Mpango hii leo Juni 27, 2021 amefungua Mkutano mkuu wa baraza la waislamu Tanzania (BAKWATA) Unaofanyika Jijini Tanga.
Makamu wa Rais amewahakikishia BAKWATA kwamba serikali ipo pamoja nao na ipo tayari katika kupokea ushauri na maoni watakayotoa juu ya mwenendo wa serikali wakati wowote.
Makamu wa Rais amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa, kuwahimiza wananchi kufanya kazi ambazo ni halali, kudumisha Amani na umoja katika taifa, kusisitiza maadili mema kwa jamii pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuwahimiza waumini kuchukua tahadhari juu ya janga la corona, ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo byote yanayotolewa na wataalamu wa afya nchini.
Makamu wa Rais amesihi BAKWATA, Viongozi wote wa dini ya Kiislam na dini nyingine na pia Wakuu wa Taasisi zote za Dini kujitahidi kuziendesha Taasisi hizo kwa mujibu wa Katiba zao na mafundisho ya Dini.
Awali akisoma hotuba ya BAKWATA Katibu wa Baraza hilo Sheikh Nuhu Jabir Mruma amesema Bakwata itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na kuwahimiza waumini wa dini ya kiislamu kulipa kodi kwa manufaa ya taifa.
Kwa Upande wake Mufti Mkuu wa Tanzania Aboubakar Zuber Bin Ali amewataka waislamu nchini kote kuongeza umoja na mshikamano ambao utaleta utulivu katika nchi.