Wild Flower
JF-Expert Member
- Jul 20, 2023
- 977
- 1,966
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, amewataka Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu, akisisitiza kwamba bima haziwezi kumlinda mtu anayejiletea madhara kwa makusudi kutokana na kushiriki vurugu wakati wa uchaguzi. Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), tukio lililoambatana na uwasilishaji wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2024, Dkt. Mkuya amesema ni jukumu la kila raia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani bila uvunjifu wa sheria.
“Uchaguzi bila ya vurugu inawezekana. Ukiwa unakwenda kufanya vurugu, bima haitakulinda, kwa sababu utakuwa umetafuta jambo la makusudi. Tunaomba sana ushiriki uchaguzi huu kwa sababu ni haki yako kikatiba, lakini uchaguzi huo tukaushiriki kwa amani na utulivu,” amesema Dkt. Mkuya.
Waziri huyo amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha sekta ya bima inakuwa imara na inawanufaisha wananchi wote, huku akihimiza Watanzania kuendelea kujiunga na huduma za bima kwa maendeleo yao binafsi na ya Taifa.