Inapatikana wapi hiyo sehemu ya pili ya kisa hiki?
Je, Kwanini Mwamwindi Alimpiga Risasi Kleruu? Nimefanya Mahojiano Na Mtoto Wa Mwamwindi (2)
Kleruu akamwuliza Mzee kwa ukali, " Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?". Baba akamwomba Kleruu waende wakuzungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; " Hapa ndipo unapozika mirija yako?" Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.
Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aia ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia;
" Kanichukulie bunduki yangu"…… Endelea…
" Je, aliposikia hayo Dr Kleruu alifanyaje?"
" Nadhani alipigwa na butwaa. Hakuamini kama baba angefikia hatua hiyo"
"Na ilikuwaje basi Mwamwindi alipoletewa bunduki?"
" Ilienda haraka, Mzee Mwamwindi akainua bunduki yake. Tayari ilikuwa loaded na risasa tangu jana yake alipotoka kuwinda. Kleruu aliinua mikono yote miwili kama mtu anayesalimu amri. Mwamwindi akampiga risasi ya kwapani. Kleruu akabaki hai. Akapiga risasi nyingine. Ikamwua pale pale." Anasimulia Mzee Amani Mwamwindi.
Kinafuatia kimya. Anainama, namwona usoni, kuwa huzuni imemjia. Bila shaka, ni kitendo kile cha baba yake kumpiga risasi na kumwua Dr Kleruu ndicho kilichoashiria mwanzo wa ukurasa mgumu katika familia ya Mwamwindi , Isimani na pengine Iringa kwa ujumla.
Nafikiria kumwuliza swali lifuatalo; Risasi ya pili ya Mzee Mwamwindi ilimpiga Dr Kleruu katika sehemu gani ya mwili? Nasitisha swali hilo. Litasubiri mara nyingine. Mzee Amani Mwamwindi anaendelea kunisimulia;
" Mdogo wangu Mohammed akiwa shambani alisikia mlio wa bunduki. Alidhani kuwa baba amepigwa risasi. Alikimbia kurudi nyumbani. Na pale ilipowekwa kumbukumbu ya Kleruu nyuma yake ndio ilipokuwa nyumba ya mzee. Hivyo, pale ulipowekwa mnara ni mbele ya nyumba. Kwa sasa nyumba hiyo haipo.
Alipofika nyumbani, Mohammed akamkuta baba amesimama, na Kleruu amelala chini, amekufa. Mzee alichukua kofia ya pama ya Kleruu, akaivaa. Akaingiza mkono mifukoni mwa Kleruu, akachukua funguo za gari la Kleruu. Mzee alimwambia mdogo wangu amsaidie kumwinua Dr Kleruu. Mzee alimshika miguuni na mdogo wangu Mohammed alimshika kwenye mikono. Wakamwingiza kwenye buti la gari.
Baba akaendesha mwenyewe gari lile la Mkuu wa Mkoa Kleruu, Peogeot Injection, rangi ya bluu likiwa linapepea bendera ya taifa. Aliendesha kuelekea mjini Iringa. Njiani kuna walioshangaa kumwona Mwamwindi akiendesha gari la Mkuu wa Mkoa huku akiwa kichwani amevalia pama la Kleruu.
Mzee alipoingia mjini Iringa breki ya kwanza ilikuwa hapa tulipo, nyumbani kwangu Mlandege. Kama nilivyosema, wakati huo nilikuwa kijana wa miaka 21. Nilishakuwa na mji wangu, nilijenga kibanda changu hapa tulipo. Nilifanya kazi kama karani wa Ushirika. Siku ile ya tukio nami nilikwenda kwenye shamba langu Ifunda.
Basi, Mzee alipofika hapa nyumbani akaambiwa kuwa nimekwenda shamba Ifunda. Alisikitika sana." Anasema Mzee Mwamwindi huku naye bado akionyesha huzuni machoni. Miaka 40 baada ya tukio.
Alipotoka hapa alipita nyumbani kwake pale Mshindo, na baadae akasimama kwa binamu yake. Ile nyumba ya njano nyuma ya benki ya CRDB, si unaijua?" Ananiuliza.
" Ndiyo" Namjibu.
" Pale alikuwa anakaa binamu yake na baba. Basi, alipofika pale akakutana n abinamu yake. Binamu yake yule alishangaa kumwona mzee akiwa na damu kwenye nguo zake. Akashangaa pia kumwona akiwa na gari la Kleruu lenye bendera ya taifa ikipepea. Akamwuliza nini kimetokea? Mzee hakuweza kuongea akaeleweka. Alitamka; " Nimeenda kwa Amani ( Mimi) nimeambiwa kaenda shambani kwake Ifunda". Alionekana kuchanganyikiwa.
Akaingia kwenye gari. Akaendesha moja kwa moja hadi Kituo cha polisi. Akamkuta polisi kijana. Akashuka, akamwambia; " Njoo chukua mzigo wako". Akaweka chini pia kofia ya pama ya Kleruu.
Polisi alipofungua buti ya gari akashangaa kuona mzigo wenyewe ni mwili wa Mkuu wa Mkoa, Dr Kleruu. Mzee akawa amejisalimisha.
Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia. Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa ni Jumamosi, siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka; " Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae". Nikaongea na Mzee.