Wananchi wa Kijiji cha Mlowa Bwawani, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, wamemlalamikia Diwani wa kata hiyo, Andrew Richard Mseya (CCM), kwa madai ya kutumia mamlaka yake kuwanyanyasa, kuwapiga, na kuwatoa vitisho pindi wanapodai maendeleo katika kijiji chao.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakazi hao wamesema wananyimwa uhuru wa kutoa maoni yao, hasa kuhusu masuala ya maendeleo. Wamedai kuwa Diwani huyo huwafuatilia, kuwanyanyasa, na hata kuwapiga wanapozungumza kwa uwazi kwenye mikutano au kupitia majukwaa mbalimbali.
Kwa mujibu wa mmoja wa wakazi hao, Abdulaziz Aboubakar, tukio la hivi karibuni lilitokea baada yake kuuliza maswali kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia kundi la WhatsApp la kata hiyo. Anadai kuwa kitendo hicho kilimkasirisha Diwani, ambaye baadaye alimtishia na hatimaye kumfuata na kumpiga.