Januari 15, 2026 Uganda inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu nchini humo ambapo
tume ya uchaguzi inaeleza kuwa Kwa mujibu wa Kifungu cha 61(2) cha Katiba ya Jamhuri ya Uganda, iliteua tarehe hiyo kufanya uchaguzi wa Rais na Wabunge (Mbunge wa kuchaguliwa moja kwa moja na Mwakilishi Mwanamke wa Wilaya bungeni).
Mnamo Septemba 23 na 24, 2025 Tume ya Uchaguzi ilifanya
uteuzi wa wagombea wa Urais uliofanyika katika viwanja vya Tume (EC) vilivyopo Lweza – Lubowa, Wilaya ya Wakiso ambapo kati ya walioteuliwa Rais Yoweri Kaguta Museveni (NRM) anayetetea kiti hicho, na Kyagulanyi Robert Ssentamu (NUP) maarufu kama Bobi Wine, ndiyo wanatajwa kuwa washindani wakubwa.
Madai
Kumekuwapo na kipande cha Video kinachomuonesha Rais wa Marekani Donald Trump akisema 'Bobi Wine' ni rafiki yake na atamuunga mkono katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari 2025.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Katika video hiyo JamiiCheck imebaini kichwa cha habari kinachosomeka 'President Trump meets with NYC Mayor-elect Mamdani' kikiambatana na nembo ya ABC News. Utafutaji wa maneno muhimu kupitia kichwa hicho, ulibaini
video halisi iliyochapishwa na ABC News ikiambatanishwa na maneno yanayosema,
"After months of criticism, President Trump praised Mamdani in the Oval Office, saying they agree more than expected." ('Baada ya miezi kadhaa ya ukosoaji, Rais Trump alimpongeza Mamdani katika Ikulu ya White House, akisema kuwa wanakubaliana zaidi kuliko ilivyotarajiwa.')
Zohran Mamdani, mzaliwa wa Uganda na mwanachama wa Democratic,
alishinda kinyang’anyiro cha Umeya wa Jiji la New York dhidi ya aliyekuwa Gavana wa New York, Andrew Cuomo — aliyekuwa akiwania kama mgombea huru.
Video inayomuonesha Trump akimtaja Bobi Wine imetengenezwa kwa akili unde ili kupotosha. Uchambuzi wa kifaa cha utambuzi wa maudhui '
Deepware' yaliyotengenezwa kwa Akili Unde kinabainisha kutumika kwa teknolojia hiyo katika kutengeneza video husika.