Posted Date::5/31/2008
Mwendesha Mashtaka akamilisha uchunguzi kuhusu Basil Mramba
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
UCHUNGUZI dhidi ya tuhuma za ufisadi dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya tatu, Basil Mramba, umechukua sura mpya, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eliezer Feleshi kukamilisha kazi yake.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa tayari jalada la uchunguzi huo limesharejeshwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya kufanyika kazi zaidi.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa, Mramba anachunguzwa kutokana na tuhuma za ufisadi katika misamaha ya kodi ambayo ilitolewa kwa mabilioni ya shilingi kwa wafanyabiashara katika mazingira tata.
Feleshi alilithibitishia Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalumu ofisini kwake, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa jalada la kesi hiyo lilifikishwa ofisini kwake na amemaliza kulifanyia kazi.
Alisema baada ya kumaliza kulifanyia kazi amewakabidhi Takukuru kwa ajili ya kulifanyia kazi zaidi.
"Tumelirudisha kwao ndiyo wanaojua ambacho wanaendelea nacho, kwa hiyo nini kinafanyika ni bora muwaulize wao," alisema Feleshi.
Alipoulizwa kama ofisi yake imetoa maelekezo ya kufunguliwa mashtaka au kulifanyia kazi zaidi jalada hilo, alisema kwa kawaida taratibu zao haziruhusu kueleza nini ofisi hiyo imeandika katika jalada la uchunguzi.
Feleshi aliongeza kwamba, Takukuru ambao ndiyo wanaochunguza tuhuma hizo ndiyo wenye mamlaka ya kueleza hatua iliyofikiwa.
Mkurugenzi huyo alifafanua kwamba, taratibu za kiutendaji haziruhusu kueleza nini ambacho ofisi hiyo imeandika kwenda kwa mhusika.
Alisema taratibu zote zinazofanyika ikiwamo kama ni mashtaka, mhusika pia anapaswa kupewa taarifa.
"Hakuna kitu kinafanyika kwa siri, hata mhusika (mtuhumiwa) lazima awe anapewa taarifa za mchakato," alisisitiza Feleshi.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini zaidi kwamba kuna mipango mbalimbali ya chini kwa chini, inayofanywa na serikali ya kutaka kuwafikisha mahakamani baadhi ya vigogo nchini kwa tuhuma za ufisadi.
Taarifa kutoka ndani ya serikali zinaeleza kwamba, majalada mbalimbali ya uchunguzi yameanza kupelekwa katika ofisi ya DPP.
Alipoulizwa taarifa za majalada ya baadhi ya vigogo wengine kuchunguzwa na kupelekwa ofisini hapo, alisema wingi wa majalada katika ofisi hiyo ni kitu cha kawaida.
Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Lilian Mashaka, alisema pamoja na taarifa hizo kuwa za kweli, hawezi kusema chochote kwa kuwa sio msemaji wa taasisi.
Alishauri gazeti hili kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea, kwa maelezo ya kina kuhusiana na suala hilo.
Kauli ya Mashaka ilirudiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa taasisi hiyo, Alex Mfungo, aliyesema kuwa taasisi hiyo ina taratibu zake katika kutoa taarifa na kwamba mkurugenzi mkuu ndiye msemaji.
"Nyie mkitaka taarifa hizo njooni ofisini, mfuate utaratibu, sio kila mtu anasema kila kitu. Msemaji wa taasisi ni mmoja tu," alisema Mfungo.
Hata hivyo, Dk Hosea hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake ya mkononi kuita mara kadhaa bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Mramba alipotafutwa kwa njia ya simu jana kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo, alisema hawezi kuzungumzia mambo yaliyopo katika ofisi za watu wengine bila kufafanua zaidi.
Ikiwa mwanasiasa huyo atafikishwa mahakamani, itakuwa ni mara ya pili kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwashtaki watendaji wake wa zamani ikianzia na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, anayeendelea kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Profesa Mahalu anatuhumiwa kuiibia Serikali Sh 2 bilioni kutokana na kuongeza bei wakati wa mchakato wa ununuzi wa Jengo la Ubalozi wa Tanzania, mjini Rome.
Pia kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa rasmi kwamba, serikali iko mbioni kuwashtaki watu wanaotajwa kuhusika katika wizi wa mabilioni ya fedha za umma, katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wale waliohusika kuipa zabuni kwa upendeleo Kampuni hewa ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development LLC.
Rais Kikwete alimuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, kuongoza timu ya wataalamu akisaidiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saidi Mwema na Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hosea kuchunguza na kuwashtaki watu ambao watabainika kuhusika na wizi wa Sh 133 bilioni kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika BoT.