Hata hivyo, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, 12 Septemba 2005, siku ambayo kampuni ya Manji na baba yake wanadai kufunga mkataba wa kukopa mabilioni ya shilingi, Kagoda yenyewe ilikuwa haijasajiliwa.
Cheti cha usajili wa Kagoda Na. 54040 kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA), kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005, siku 17 baada ya Manji kufunga mkataba na kampuni ya kitapeli.
Watu muhimu katika siri ya Rais Kikwete kuhusu wezi wa fedha za BoT ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Said Mwema, Mkurugezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah na Mwanyika, ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Maalum ya rais ya kufuatilia walioiba benki.
Kazi za kamati hii zimebaki siri ya watu hao wanne; hata idadi ya watu waliogundulika, walioahidi kulipa na kiasi watakacholipa imebaki siri yao.
MwanaHALISI lina taarifa, tangu miaka mitatu iliyopita, kuwa mwenye kampuni ya Kagoda au anayejua shughuli zake ni Rostam Aziz.
Wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam, katika andishi rasmi kwa Kamati ya rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), anakiri kuwa ni yeye alishuhudia
mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.
Anasema alishuhudia mkataba wa Kagoda ndani ya ofisi za kampuni ya Caspian Construction Limited ambayo inamilikiwa na Rostam iliyoko Mtaa wa Milambo Na. 50 katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Sanze anasema, Niliitwa na Bw. Malegesi ofisini kwa Bw. Rostam Aziz
Nilipofika
niliwakuta Bw. Rostam Aziz, Peter Noni (Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa benki ya raslimali) na Bw. Malegesi; wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake.
Andishi la wakili linaeleza kuwa Rostam Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia Sanze kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu Benjamin Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana Ballali kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.
Bali taarifa zilizoenea Dar es Salaam zinasema Rostam aliamua kumuuzia kesi Manji ili kujinusuru na kashfa ya Kagoda. MwanaHALISI lilipowasiliana na Manji kutaka kufahamu iwapo madai hayo ni kweli alijibu, Hivi sasa ni vita. Hata hivyo, Manji hakufafanua vita hivyo vinalenga kuangamiza nani.
Nyaraka zilizo mikononi mwa gazeti hili zinaonyesha risiti kadhaa za serikali zinazodaiwa na wa ndani wake kuwa ndizo zilizotolewa na serikali kuthibitisha Manji kurejesha fedha za Kagoda.
Miongoni mwa risiti hizo ni Na. 31494282 yenye thamani ya Sh. 4.5 bilioni; 31494264 ya Sh. 4.5 bilioni na 31494283 ya Sh. 4.5 bilioni. Bali tarehe za risiti hizo zinagongana na zile ambazo Manji alielekeza katika mawasiliano yake na Mwanyika ya tarehe 28 Aprili 2008.
Juhudi za kuthibitisha uhalali wa risiti hizo na malipo yanayodaiwa kufanyika hazikufanikiwa. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile hakupatikana kwa maelezo ya Katibu Muhtasi wake kuwa alikuwa katika mkutano akijiandaa kwenda bungeni Dodoma.
Baada ya mwandishi kusisitiza ni lazima aonane na Likwelile kwa sababu kuna jambo la dharula, katibu huyo alisema Likwelile hawezi kuwa na muda huo.
Kwanza umepitia mapokezi? Huwezi tu kuja ofisini kwa mtu kwa vile wewe ni mwandishi na ukapewa nafasi ya kuzungumza naye. Ukitaka labda nikupangie miadi uje siku nyingine, alisema mwanamama huyo.
Mwandishi aligoma kuondoka kutoka katika ofisi hiyo na ndipo katibu huyo aliposema kuwa bosi wake (Likwelile) ameagiza kama kuna maswali yapelekwe katika ofisi ya uhusiano ya wizara.
Risiti hizo zilipelekwa kwenye ofisi ya uhusiano ambayo nayo ilizipeleka kwenye ofisi inayohusika na hundi zilizolipwa na hazina, lakini majibu hayakuweza kupatikana kwa madai kwamba jambo linalozungumziwa ni la miaka mitatu