1. Tangu Dkt Harrison George Mwakyembe ajigambe kwamba anapambana na ufisadi, hasa baada ya Ripoti ya Richmond mwenendo wake katika upambanaji huo bado haujaeleweka hasa katika kauli zake na matendo yake!
2. Baada ya Ripoti ya Richmond alidai kwamba kuna mambo ambayo wao (wanakamati teule) waliyaacha (hawayakuyafanyia kazi) "ili kulinda heshima ya Serikali!" Hii Serikali ni ipi ambayo heshima yake ilitakiwa ilindwe maana Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowasa alitakiwa apime uzito mwenyewe, na kweli Lowasa alipima uzito na kuachia ngazi. Vile vile mawaziri Msabaha na Karamati waliachia ngazi. Sasa Serikali ipi ambayo Kamati Teule ilikuwa inailinda? Hapa tuliachwa vinywa wazi kuhusu dhamira hasa ya "wapambanaji" hao.
3. Kabla vumbi halijatua tukasikia kwamba Dkt Mwakyembe alijihusisha na umeme wa upepo na haku-declare interest wakati alipokuwa anaongoza Kamati Teule kuhusu Richmond. Japokuwa Mwakyembe alijitahidi kueleza sana kwamba alitakiwa a-declare "pecuniary interest" (financial interest) na sio vinginevyo kulingana na Kanuni za Bunge, katika suala nyeti kama hilo alitakiwa aliweke wazi ili kusionekane kuwa kuna mgongano wa maslahi! Hata hiyo aliyodai kuwa ni "pecuniary interest" ni subject to interpretation kiasi kwamba suala la umeme wa upepo linaweza kuwekwa kwenye mukhtadha huo!
4. Dkt Harrison George Mwakyembe aliitwa majuzi na TAKUKURU kwa ajili ya kueleza uhalali wa kupokea posho mara mbili akadai, tena kwa dharau kubwa kwamba, amekataa kwenda kwa sababu eti Dkt Edward Hosea, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, suala lake bado linachunguzwa na kwamba nia ya TAKUKURU ni kuwaziba midomo "wapambanaji." Hoja iliyopo ni kwamba, Je, kupokea posho mara mbili toka kwenye Serikali hiyo moja kwa kazi ile ile sio kosa? Katika maelezo ambayo Dkt Mwakyembe amekuwa anayatoa kwa waandishi wa habari ameeleza kwamba suala la kupokea posho zaidi ya mara moja kwa kazi ile ile limeanza muda mrefu! Huyu Mwalimu Mwanasheria akumbuke kwamba hatuongelei practice (mazoea) bali tunaongelea sheria na uhalali wa malipo hayo. Maelezo yake kwamba TAKUKURU nao waliwahi kuwalipa posho mara mbili hayana mshiko kwa sababu TAKUKURU ndio waliowaita kwenye Semina hizo na walistahili kuwalipa. Sasa kama waliapply posho kule Bungeni TAKUKURU wangejuaje kama wamelipwa Bungeni. Kwa nini Wabunge hawakuzikataa hizo posho?
5. Kuhusu Dkt Harrison George Mwakyembe kukataa kuhojiwa na TAKUKURU kwa madai ya kuwa na kinga na kwamba bunge ni muhimili kamili! Kama Bunge ni muhimili kamili, mbona Kamati Teule ya Bunge iliwahoji Utawala ambao pia ni muhimili kamili wa dola? Hivi mipaka ya kinga ya wabunge inaishia wapi? Mbona wakati akina Mramba walipohojiwa hatukusikia juu ya kinga za bunge na wabunge? Hii kinga inawahusu "wapambanaji" tu! Hebu tuangalie Ibara ya 100(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria na. 15 ya mwaka 1984 kuhusu kinga ya Bunge kama alivyodai Dkt Mwakyembe: "100 (1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge. (2) Bila kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo."
Ukisoma between lines utaona kwamba kinga ya Bunge ni ndani ya Bunge wakati wa majadiliano na kinga hiyo inahusu uhuru wa kutoa mawazo tu! Sasa hapa mambo ya kulipwa posho zaidi ya mara moja yanaingiaje?
Kwa hiyo Dkt Mwakyembe asijifiche kwenye kivuli ambacho hakipo, atekeleze Kifungu cha 10 (1) (a) na (c) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, 2007, Na. 11/2007 kinachomtaka aitikie wito anapoitwa kuhojiwa! Akisubiri aje akamatwe kwa kukataa kuitikia wito asifikiri kwamba ndio karata ya kisiasa ya kupanda chati, asome alama za nyakati, haziko upande wake kwa sasa!
6. Kwa maelezo hayo machache hapo juu, bado sijaelewa upambanaji wa Dkt Mwakyembe na wenzake katika vita dhidi ya ufisadi ambayo inapiganwa bila kuwafahamu kwa majina mafisadi wenyewe!