Hizi ni habari 2 zilizoandikwa ukurasa wa mbele wa gazeti la Tanzania Daima la leo 28/10/2009. nimeziweka kwa kufuatana, ikianza ya Dk Mwakyembe kisha spika sitta
Sometimes nashindwa kuelewa hivi mhariri mkuu wa gazeti hili naye hupokea posho toka kwa Mafisadi?
Tanzania Daima - 28/10/2009
Porojo za Dk. Mwakyembe
• Atamba anajua sheria, ataibwaga TAKUKURU
na Sauli Giliard, Dodoma
MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, jana aliwashangaza waandishi wa habari wanaohudhuria mkutano wa 17 wa Bunge mjini Dodoma, baada ya kuitisha mkutano nao na kuhoji kwanini wanakunywa chai ya wabunge wakati wamelipwa posho na vyombo wanavyofanyia kazi pasipo kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), badala ya kutoa ufafanuzi wa kama alipokea posho mara mbili au la.
Dk. Mwakyembe alihoji hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari wa Bunge, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wakati akitoa ufafanuzi wa kukataa kuhojiwa na TAKUKURU kuhusu kuchukua posho mara mbili kwa kufanya kazi moja.
Akizungumza kwa ghadhabu, Dk. Mwakyembe alisema kitendo cha kuhojiwa na TAKUKURU wakati huu ambapo wajumbe wa kamati iliyochunguza suala la Richmond wakitaka Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Edward Hoseah, ahojiwe, ni mbinu za kutaka kuwanyamazisha.
Dk. Mwakyembe alisema kupokea posho ni utaratibu wa siku nyingi na wa kawaida, hivyo kuhojiwa sasa ni mbinu tu ya TAKUKURU kutaka wabunge wasimhoji Dk. Hoseah.
Alisema kwa uelewa wake wa kisheria, ikizingatiwa kuwa yeye ni mwalimu wa sheria, pamoja na kubaini mchezo huo, hakukubali kuhojiwa kama alichukua posho mara ya pili katika kikao cha kamati ya Bunge kilichofanyika mjini hapa na alitamba kuwa hata kama TAKUKURU itaamua kumpeleka mahakamani, ataibwaga vibaya.
"Lunch allowances ni utaratibu wa siku nyingi na wa kawaida. Hata waziri akitembelea mikoani huwa anaandaliwa vizuri, licha ya kwamba amepewa posho. Kwani inawezekana kutomwandalia kwa sababu amekwishapewa posho?" alihoji Dk. Mwakyembe.
Aliwashangaza waandishi wa habari alipowahoji kwanini hawajawahi kuhojiwa na TAKUKURU kwa kunywa chai ya wabunge huku ikijulikana kuwa wametumwa na vyombo vyao wanavyovifanyia kazi, huku akidai kushangazwa na hatua ya wabunge kufanyiwa hivyo sasa.
Huku akilifananisha gazeti lililochapisha habari yake ya kukataa na kuomba msaada wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta ili asihojiwe na TAKUKURU kuhusu madai ya kupokea posho mara mbili, alisema kama hilo ni kosa, TAKUKURU ndio vinara wa kutoa posho.
Alitoa mfano wa hivi karibuni katika semina iliyoandaliwa na taasisi hiyo, ambapo licha ya kufahamu kuwa anaishi jijini Dar es Salaam, ilimpa posho ya malazi.
"Hawa TAKUKURU ndio vinara wa kutoa posho. Inafahamika mimi naishi Dar es Salaam, wananipatia posho, leo hii pamoja na mambo mengi yanayotaka majibu wanataka kutuhoji, kama hii si kuwadhalilisha wabunge ni nini?" alihoji huku akionekana kukasirika.
Mbunge huyo mara kwa mara akihusisha kitendo hicho na mchezo mchafu unaofanywa na aliowaita mafisadi. Alisema TAKUKURU imewaita wabunge kwa kutaka kuwahoji huku wao wakitaka serikali imchukulie hatua Dk. Hoseah na kwamba hilo ni lengo mahususi la kukwamisha juhudi za wabunge.
"Sisi tunataka utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge, mojawapo ni lile la kuhojiwa kwa viongozi wa TAKUKURU," alisisitiza.
Dk. Mwakyembe alibainisha kwamba, kukaidi wito wa TAKUKURU wa kuhojiwa juu ya suala hilo kunatokana na kinga aliyonayo kama ilivyobainishwa katika kanuni za Bunge sehemu ile ya 100 pamoja na 101, ambayo inamlinda kama mtumishi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Aliendelea kujigamba kuwa kamwe hakuna mtu wa kumng'oa jimboni mwake na aliwataka wale aliowaita mafisadi waelewe kuwa hawawezi kumng'oa, labda wapige kambi kwa miaka mitano wakiwa pamoja na wake zao.
"Mafisadi kuning'oa Kyela ni kazi ngumu, labda washinde Kyela kwa miaka mitano pamoja na wake zao, ndiyo wanaweza kufanya hivyo," alijigamba.
Alisema wakati TAKUKURU inaendelea kung'ang'ania kuwahoji, zipo hoja za msingi zinazotakiwa kujadiliwa, ikiwa ni pamoja na ile ya nani mmiliki wa Kagoda na Richmond.
Taarifa zilizotufikia kutoka ndani ya kikao cha ndani ya kamati ya wabunge wa CCM, muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni zilieleza kuwa wabunge hao wamegawanyika kuhusu suala la kuhojiwa na TAKUKURU, baadhi wakikubaliana na hatua hiyo na wengine wakipinga na kutaka isitishwe mara moja.
Taarifa hizo zilieleza kuwa kundi la kwanza linaloungwa mkono na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, linaunga mkono hatua hiyo ya TAKUKURU, kwa hoja kwamba fedha nyingi za serikali zimepotea kwa kuwalipa posho mara mbili wabunge. Kundi la pili linalodaiwa kuungwa mkono na Spika Sitta linadaiwa kuipinga hatua hiyo ya TAKUKURU, kwa madai kuwa inawadhalilisha wabunge. Hata hivyo habari hizo zilidai kuwa, licha ya Spika kutaka hatua hiyo isitishwe, Pinda alitangaza msimamo wake kuwa ni lazima kazi ya kuwahoji wabunge wote wanaotuhumiwa kuchukua posho mara mbili iendelee.
Spika Sitta kigeugeu
• Akana kauli zake, barua rasmi ya ofisi yake
na Charles Mullinda
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, sasa ameanza kutoa kauli tatanishi baada ya jana kuzungumza na Tanzania Daima Jumatano na kueleza kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekiuka taratibu kwa kuwaita na kuwahoji baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kuchukua posho mara mbili, baada ya kufanya kazi moja.
Sitta ambaye yuko mjini Dodoma anakoongoza mkutano wa 17 wa Bunge, alihojiwa na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu msimamo wake dhidi ya TAKUKURU kuwahoji wabunge na kutoa ufafanuzi wa barua iliyoandikwa na Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah, ambayo gazeti hili limeiona, kwenda kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah, ikimtaka alitafutie ufumbuzi suala la wabunge kulipwa posho mara mbili. Katika majibu yake Spika Sitta alikana kuifahamu barua hiyo na kueleza kuwa si jambo la ajabu kwa ukarimu wa Kitanzania wabunge kulipwa posho mara mbili na aliwashutumu baadhi ya viongozi wa juu wa serikali bila kuwataja majina kwa kulitisha Bunge ili lisitekeleze majukumu yake inavyotakiwa.
Kauli hii ya Sitta imekuja siku chache baada ya Jumatatu wiki hii kunukuliwa katika baadhi ya vyombo vya habari akilalamika kuwa TAKUKURU inawadhalilisha wabunge inapowaita na kuwahoji bila kufuata utaratibu wala kanuni na jana alinukuliwa tena na baadhi ya vyombo vya habari akitoa mwongozo kwa wabunge kukubali kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU inapowaita kuwahoji.
Awali alinukuliwa akieleza kuwa hatua iliyofikiwa na TAKUKURU kuwaita wabunge na kuwahoji ni uhdalilishaji na imekiuka utaratibu, kanuni na sheria za nchi dhidi ya Bunge kama taasisi inayojitegemea.
Katika kauli hiyo, Sitta pia alieleza kuwa hajui kuwapo kwa jambo hilo kwa sababu hajataarifiwa na kwamba hajui kinachohojiwa na TAKUKURU kwa sababu taarifa hizo anazisoma katika vyombo vya habari.
Alitoa tahadhari kwa taasisi nyingine za uchunguzi ikiwamo TAKUKURU kutoa taarifa ya maandishi ofisini kwake linapotokea jambo kama hilo ili Bunge liwe na taarifa na litoe utaratibu.
Siku moja baada ya Spika kunukuliwa akitoa kauli hiyo, jana alinukuliwa akitoa kauli nyingine aliyokuwa ikipingana na ile ya kwanza.
Gazeti moja la kila siku liliandika habari za ndani kutoka katika kikao cha wenyeviti wa kamati za Bunge, ambapo Spika Sitta alitoa mwongozo kwa wabunge kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TAKUKURU wanaowaita kuwahoji.
Hata hivyo alipozungumza na gazeti hili jana, Spika Sitta alisema msimamo wake halisi kuhusu suala hilo ni kupinga TAKUKURU kuwaita wabunge na kuwahoji bila yeye kutaarifiwa.
"Ninayoyaongea sasa, ndiyo unapaswa kuyachukua kwa sababu ndio msimamo wa Spika. Kwanza mimi siijui barua hiyo. Pili, TAKUKURU wamekosea kulifanya suala hili la kawaida sana, wabunge si watu wa kuchezea, ni watu wakubwa na muhimu sana wanaopaswa kuhojiwa kwa heshima na viongozi wa juu wa vyombo vya usalama.
"Na kabla ya kuhojiwa, ni lazima Spika ningetaarifiwa kwanza na kuandaa mazingira ya kuhojiwa kwao. Haiwezekani watu wa chini wasiojua maana ya mbunge kumhoji mbunge pasipo Spika kujua. Na kikawaida, takrima kwa ukarimu wa Kitanzania ni jambo la kawaida, ni ukarimu wa Kitanzania, hivyo hakuna posho mara mbili hapo. Ni ukarimu tu na wabunge wanaruhusiwa kuchukua," alisema Spika Sitta.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Katibu wa Bunge, Kashililah kama ni wa shaka kiasi cha kuandika barua nyeti inayoomba msaada wa taasisi nyingine pasipo kumtaarifu, Spika Sitta alisema haamini kama Kashililah aliandika barua hiyo na kama aliandika, basi alilazimishwa na viongozi wa juu wa serikali.
Katika hatua ya kushangaza, Spika alitoa kauli nyingine kuwa hata kama Kashililah aliandika barua hiyo, basi alikuwa anatekeleza majukumu yake ya kiutalawa hivyo anaweza asimtaarifu lakini TAKUKURU walipaswa kutochukua hatua zozote kulingana na barua hiyo kabla ya kumtaarifu.
"Mambo ya utalawa sishiriki kila jambo, mhusika mkuu ni katibu na nadhani alilichukua kiutawala zaidi. Lakini TAKUKURU kabla ya kuanza kuifanyia kazi barua hiyo ni lazima wangenitaarifu kwanza Spika.
"Hili jambo tumelijadili sana jana na juzi, tumebaini kuwa Katibu wa Bunge alitishwa sana. Watu wakubwa serikalini wamekaa vikao vingi tu, wamemtisha sana katibu kuwa ni lazima aandike barua hiyo, oh… eti ni maagizo ya rais, wakamlazimisha kuandika barua ile. Hili mimi siliafiki na tumefikisha malalamiko kwa waziri mkuu leo.
"Bunge haliwezi kuendeshwa kwa vitisho, serikali iache kabisa kulitisha Bunge…. Bunge litakataa. Kama mbunge anatuhumiwa kuna Kamati ya Maadili ya Bunge, itashughulikia tuhuma hizo, si mambo haya yanavyofanyika sasa. Ni njama tu, lakini kamwe hatulegezi kamba, Bunge litaendelea na kazi yake pamoja na vitisho vyote," alisema Spika Sitta. Wakati Sitta akitoa kauli tatanishi kuhusu barua iliyoandikwa na Kashililah kwenda kwa Hoseah huku akisisitiza kutoifahamu, Tanzania Daima Jumatano imefanikiwa kuiona barua hiyo yenye kumbukumbu namba CEB.50/155/05/81 ikiwa na kichwa kinachosomeka: ‘Baadhi ya kamati za Bunge kuomba takrima serikalini na katika mashirika ya umma.'