Huwezi kutambua udini kwa kuangalia majina ya watu. Pia huwezi kutambua udini hata kama utazijua takwimu za asilimia za watu wa kila dini kwenye sehemu fulani. Udini huwa ni SERA (ya wazi au ya kificho) ya kuwapa watu wa dini fulani manufaa fulani kwa upendeleo dhidi ya watu wa dini nyingine. Aina zote za ubaguzi ziko hivyohivyo. Haihusiani na suala la idadi ya watu wa dini fulani kwenye hiyo sehemu hata kidogo. Mifano rahisi ipo: Kule Rwanda baada ya 1994 serikali iliundwa ya "mseto" ikichanganya watusi na wahutu. Ungehesabu idadi ya wahutu kwenye serikali kweli walikuwa wengi zaidi (Rais na Waziri Mkuu pia walikuwa wahutu), lakini watusi wachache ndio waliokuwa na nguvu na mamlaka hadi leo. Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake aliwahi kusimulia jinsi alivyotuhumiwa udini enzi za utawala wake, tena tuhuma zilienezwa kuwa si tu kwamba anapendelea wakristo kwenye baraza la mawaziri, bali walisema anapendelea wakatoliki. Kuonesha kuwa hakuwa na upendeleo akaitisha idadi ya viongozi na dini zao, akagundua wakatoliki walikuwa yeye na George Kahama tu (tena akadai Kahama "hakuwa mkatoliki" kwani alikuwa ameoa mke wa pili, kinyume na ukatoliki!) Lakini bado nasema mimi kuwa idadi ya watu si jibu. Sina ushahidi kuwa Nyerere alikuwa na udini au la, lakini njia aliyotumia kujibu kuwa hakuna udini haikujibu tuhuma kikamilifu (labda kama waliolalamika walizungumzia "idadi" ya wanaoteuliwa, na si sera ama utaratibu wa uteuzi ama nguvu za hao wateuliwa).
Kadhalika sina uwezo wa kusema kuwa huko Ifakara kuna udini au la (kwanza silijui hilo shirika kwa undani), lakini jibu lililotolewa la idadi ya watu halitusaidii kujua kuwa hilo shirika la Ifakara kuna udini au la! Kwa kuangalia tu hayo majina na hata ukijua dini zao wote, bado hutaweza kusema kuna udini!
Sisi tusiofahamu hilo shirika tungeweza kuamini kweli kuna udini au la iwapo masuali yafuatayo yangejibiwa:
a) Je katika shirika hilo dini ya mtu ndio kigezo cha mtu kupewa manufaa ambayo wasiyo na dini hiyo wanayakosa kwa sababu tu ya dini?
b)Je Katika shirika hilo dini ya mtu ndio kigezo cha yeye kusikilizwa au kukubaliwa mapendekezo ama maoni yake?
c)Je Katika shirika hilo kuna watu wanaotengwa ama kunyanyaswa kwa sababu ya dini zao?
d)Je Katika shirika hilo kuna watu wa dini yoyote ambao mahitaji yao ya msingi ya kidini (ambayo kiserikali yanakubalika) wananyimwa ama kuzuiwa? (Hali inayoweza kumfanya mtu aone kufanya kazi hapo huku ukiwa na dini hiyo ni mateso?) Mfano kumshurutisha mfanyakazi mambo ambayo ni kinyume na maadili ya dini yake na hata sheria za nchi, na hayo kumfanyia wa dini fulani tu (watu wa dini fulani sikukuu zao wanashiriki vizuri, wale wa dini nyingine sikukuu zao zikifika wanapangiwa majukumu, mfano). Je kuna mambo yanayofanana na hayo?
e) Je katika shirika hilo mamlaka (si madaraka) aliyo nayo mtu yanategemea dini yake?
Katika yote niliyotaja (a) hadi (e) hapo juu utagundua kuwa idadi ya watu si muhimu, muhimu ni kwamba hao waliopo wanatendewaje?
Kwa ujumla, tupewe ushahidi wa ki-SERA (ya kificho, isiyoandikwa, au hata ya wazi) unaoonesha upendeleo wa watu wa dini moja dhidi ya nyingine, huo ndio utakuwa udini. Idadi au majina si hoja. Mpaka sasa hakuna aliyetuthibitishia madai hayo ya udini dhidi ya Ifakara Research, na wala hakuna aliyetuthibitishia kuwa hakuna udini. Kilichokosekana ni utafiti. Kuwepo kwa udini hapo kwenye shirika inaweza kuwa tuhuma ni ya kweli ama ni ya uongo. Lakini kwa kuwa shirika hilo msingi wake si wa udini, ni busara a haki kuamini hakuna udini, hadi hapo ushahidi utakapoonesha vinginevyo. Mimi silifahamu hilo shirika, sijui kama kuna udini au la, lakini kwa kuwa udini ni tuhuma ya ubaguzi na ni mbaya, napenda kulitendea haki hili shirika (tuite natural justice, kwamba they are innocent unless there is evidence to the contrary). Kama evidence hiyo hakuna, ni aibu kwa watu wazima tena wasomi kujadili jambo kwa misingi ya "nasikia hivi, nasikia vile!" huo utakuwa udaku.