Dk Slaa afunika
Tuesday, 27 July 2010 06:33
*Wapigakura waafiki aache jimbo awanie urais
Na Tumaini Makene, Karatu
MSAFARA wa kumsindikiza mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa ulisimamisha shughuli za wananchi wa mikoa ya Arusha na Manyara kwa eneo la takribani kilometa 20.
Msafara huo uliokuwa ukimsindikiza Dkt. Slaa kwenda kuomba ridhaa ya wananchi wa Karatu ili agombee urais badala ya ubunge wa jimbo hilo, na kisha kuchukua fomu ya kugombea urais, ulijumuisha magari ya kila aina takribani 80 na pikipiki zaidi ya 100 kuanzia katika Uwanja wa Ndege wa Arusha hadi Karatu.
Kutoka Arusha msafara huo ulikuwa na magari ya kifahari kama vile VX, VGX, Benzi na mengine ya kawaida zaidi ya 15. Ulipofika eneo la Mto wa Umbo ambalo liko katika Wilaya ya Monduli- Arusha, ambao ni umbali wa takribani kilometa 20 kutoka Karatu, msafara ulipokelewa na magari mengine mengi na waendesha pikipiki.
Kutokea hapo msafara ulikwenda kwa 'mwendo wa pole' ambapo mbali ya magari na pikipiki, msafara huo kuanzia eneo hilo, ulinogeshwa na helkopta iliyokuwa ikiufuata kwa juu kwenda Karatu.
Huku Dkt. Slaa akiwa amesimama ndani ya gari na nusu ya mwili ukiwa nje akiwapungia mikono watu, wananchi katika maeneo hayo walisimama kando ya barabara kushuhudia msafara huo na kupunga mikono yao, na wengine wakiamua kukimbia riadha kwa hatua kadhaa kuufuata.
Pamoja na msafara huo kuunganisha magari katika eneo la Mto wa Mbu, magari na pikipiki yalizidi kuongezeka kujumuika kadri muda ulivyokuwa ukikaribia kufika Karatu.
Hali ya shangwe ilitawala miongoni mwa wafuasia wa CHADEMA, baada ya msafara wao kulakiwa na umati mkubwa wa watu Mjini Karatu, ambapo ilionekana wazi shughuli nyingi kusimama na wananchi kuukimbilia msafara huo kueleklea Uwanja wa Bwawani.
Ni hapo ndipo Dkt. Slaa, mmoja wa wanasiasa machachari na mahiri nchini, ambaye amekuwa bungeni kwa miaka 15, aliamua kuikabidhi fomu yake ya kugombea ubunge Jimbo la
Karatu na badala yake akachukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kushawishiwa na watu wa kada mbalimbali nchini.
Alifikia uamuzi huo baada ya wananchi hao kuulizwa mara kadhaa na Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe na yeye mwenyewe Dkt. Slaa iwapo wanaridhia yeye kuacha ubunge na kwenda kugombea urais ili aweze kuwatumikia watu wengi zaidi na kupata mamlaka ya kutekeleza yale
ambayo amekuwa akiyapigania bungeni.
Akizungumza katika kadamnasi ya watu wa Karatu, Dkt. Slaa alikiri kuwa baada ya kushawishiwa na watu mbalimbali wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu waliotuma maombi maalumu, wananchi wa kawaida na wanachama wa CHADEMA kugombea urais, alihuzunika kwa sababu
alijua atawaacha watu wake wa Karatu.
"Nina majonzi kuwaaga lakini ninayo furaha...ni baada ya kupata ridhaa yenu, sina budi kwenda kuwatumikia Watanzania walioniita wakinitaka niwe rais...sauti ya watu ni Sauti ya Sauti ya Mungu...Mwalimu Nyerere alisema Ikulu si mahali pa kukimbilia, lakini nimeombwa na watu...Mungu ndiye huweka viongozi tukimtegemea na kumnyenyekea yeye tutaingia ikulu.
"Ninazo sababu nyingi za kukubali kuchukua fomu ya urais, nchi hii sasa inahitaji kiongozi makini, baada ya Nyerere na Mwinyi mamlaka ya nchi yamepokwa na kikundi cha watu wachache...nchi haiwezi kuendelea, wala utawala bora na wa sheria hautakuwepo kama ufisadi
hautapigwa vita.
"Taifa limeparanganyika kwa kukosa uadilifu, sasa wananchi maskini wanabaguliwa katika kupata huduma kama vile elimu na afya, tunahitaji rais wa kurudisha hatima ya wananchi kuamua mstakabali wa raslimali na maendeleo mikononi mwao, rais atakayetutoa katika matumaini yaliyopotea kuturejesha kwenye matumaini mapya," alisema Dkt. Slaa katika mkutano huo ulioombewa na viongozi wa dini za kiislamu na kikristo.
Katika maombi yao viongozi hao kwa nyakati tofauti walisema suala la ukombozi wa nchi halina dini wala rangi ya mtu.
Mapema akimkaribisha Dkt. Slaa kuwaeleza wananchi wa Karatu sababu za kumwomba na kumruhusu Dkt. Slaa kuondoka bungeni na kugombea urais, Bw. Mbowe alisema kuwa CHADEMA kimejipanga kushinda urais na kupata majimbo mengi ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba mwaka huu.
"Tumeweka mikakati maalumu ya kuwatumikia na kupigania maslahi ya Watanzania, Dkt. Slaa anakwenda kushinda urais tunaomba aungwe mkono...CCM wameshtuka kusikia anagombea urais. Zama zao na zama za Kikwete zimekwisha... ikitokea hajashinda na mkatupatia wabunge
wengi jueni kuwa Dkt. Slaa atakuwa ndiye spika wetu.
"Lakini pia msihofu kuwa Dkt. Slaa hatasikika, yeye ndiye Katibu Mkuu wa CHADEMA, ndiye mpishi wa mambo yote ya chama yanayoibuliwa na wabunge wa chama chenu bungeni, tumeamua kumtumia kuliokoa taifa, kama vile Mungu alivyomtoa mwanaye wa pekee, Yesu, kuwakomboa
wote wenye dhambi," alisema Bw. Mbowe.
SOURCE:
Dk Slaa afunika