Kesi ya Dowans yaiva Dar
• Pingamizi la wanaharakati kuanza kusikilizwa Mahakama Kuu
na Mwandishi wetu
HATIMAYE Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na mashirika 16 ya wanaharakati wamepokea hati ya kuanza kusikilizwa kwa pingamizi lao la kupinga nia ya serikali kutaka kuilipa fidia ya sh bilioni 94 Kampuni ya Dowans.
Novemba 15, mwaka jana Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker iliamuru TANESCO iilipe Dowans fidia ya sh bilioni 94 kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Kufuatia uamuzi huo, Januari 25 mwaka huu Dowans iliwasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam maombi ya usajili wa tuzo yake hiyo kupitia kwa Wakili wake, Kenedy Fungamtama, ili ulipwaji wa fidia yake hiyo ufanyike kisheria.
Maombi hayo ya Dowans yalikwisha kusajiliwa na kupewa namba ya usajili wa madai namba 8 ya mwaka 2011, na tayari yameshapangiwa jaji wa kuyasikiliza.
Lakini LHRC kwa niaba ya mashirika mengine ya wanaharakati waliwasilisha rasmi pingamizi lao wakiainisha hoja za msingi saba kupitia Kampuni ya uwakili ya South Law Chambers Advocates.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Ushawishi na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusi, alisema wamepokea hati hiyo ya kuitwa mahakamani na kwamba kesi yao imepangwa kuanza kusikilizwa Machi 2, mwaka huu.
Alisema kesi hiyo ilipangiwa jaji aliyemtaja kwa jina moja la E. Mushi, bila kutaja ni namba ngapi iliyopewa.
Katika hoja ya kwanza ya pingamizi hilo, wanaharakati hao wanadai kuwa hawakuridhika na tuzo hiyo iliyotolewa na ICC kwa Dowans kwani TANESCO ni shirika la umma linalomilikiwa na Serikali ya Tanzania.
Walidai kuwa ingawa TANESCO inaendeshwa kwa fedha zinazotokana na huduma zake, lakini sehemu ya fedha hizo zinatokana na Watanzania walipa kodi.
Katika hoja ya pili wanadai kuwa hakuna mkataba wa kisheria uliofungwa baina ya TANESCO na Kampuni ya Dowans uliosababisha kuwepo kwa mgogoro ulioilazimu ICC kutoa tuzo hiyo kwa kampuni hiyo.
Sambamba na hoja hiyo, wanaharakati hao wameambatanisha na mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond ambao Dowans iliurithi, unaodaiwa kuwa na mashaka kisheria, kama kielelezo.
Hoja ya tatu wanadai kuwa chini ya sheria za Tanzania, mkataba na tuzo hiyo kwa Dowans ni batili na umejaa dosari za kisheria.
Katika hoja ya nne, wanaharakati hao wanadai kuwa chini ya sheria za Tanzania, Kampuni ya Richmond haikuwa na nguvu ya kisheria kuingia mkataba na Serikali ya Tanzania au na TANESCO kwa niaba yake ambao unaweza kutekelezwa.
Wanaharakati hao wametia nguvu hoja yao hiyo kwa kuambatanisha na kielelezo cha taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wake.
Wanaharakati hao wanadai katika hoja yao ya tano kuwa kutokuwepo kwa mkataba hai kati ya Richmond na TANESCO, jukumu lilitakiwa kutekelezwa na wajibu pingamizi wa kwanza na wa pili, ambalo ndilo lilisababisha kutolewa kwa tuzo hiyo kuwa batili.
Hivyo, kwa mazingira hayo, wanaharakati hao katika hoja yao hiyo wanadai kuwa tuzo hiyo iliyotolewa na ICC haiwezi kukubaliwa wala kutekelezwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hoja ya sita ya pingamizi hilo, wanaharakati hao wanadai kuwa tuzo hiyo ilitolewa hata kabla ya mgogoro mwingine katika mahakama nyingine ya Houston nchini Marekani, baina ya Richmond na Dowans Tanzania Limited juu ya umiliki wa mashine za kuzalishia umeme, ambazo zinahusiana na tuzo hiyo.
Katika hoja ya saba ya pingamizi hilo, wanaharakati hao wanadai kuwa maombi ya usajili wa tuzo iliyotolewa na ICC ambayo yamewasilishwa Mahakama Kuu hayapaswi kukubaliwa kwa kuwa imetokana na mkataba batili baina ya Richmond na TANESCO.
Hoja za wanaharakati hao zitakuwa zikikabiliana na hukumu ya ICC ambayo kwenye ukurasa wa 89 majaji watatu waliotoa uamuzi huo walitamka kuitambua Richmond Development Company LLC kuwa ni kampuni halali kwa mujibu wa sheria za Texas, Marekani, kinyume cha ilivyotafsiriwa na Kamati Teule ya Bunge.
Katika kukazia hukumu hiyo ya ICC, majaji hao watatu walitumia hukumu mbalimbali za siku zilizopita za huko Texas zilizotumia kile walichokieleza kuwa ni ‘parole evidence' katika kuhalalisha uwepo wa Richmond kisheria huko Texas na hivyo kuufanya mkataba wake na TANESCO kuwa halali.
Wakati ICC ikikubaliana kwamba Richmond Development Company, LLC ni jina la kibiashara la RDEVCO, LLC, Kamati Teule ya Bunge katika ripoti yake ilieleza bayana kwamba uchunguzi wao walioufanya Texas kwa kushirikiana na taasisi za kisheria za huko ulithibitisha kwamba kampuni hiyo ilikuwa haina hadhi ya kuwa kampuni halali.
Mbali ya hiyo, ICC katika ukurasa wa 41 wa hukumu yake hiyo inasema taratibu za kuhamishwa kwa mkataba kutoka Richmond kwenda Dowans zilizingatia sheria za Tanzania na kwamba ziliridhiwa na TANESCO.
ICC inaeleza kuwa Desemba 4, 2006 Dowans Holdings SA (Costa Rica) iliiandikia barua TANESCO ikieleza kwamba ilikuwa inakusudia kuanzisha na kusajili kampuni nchini itakayoendesha na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya RDEVCO.
Hukumu hiyo katika ukurasa wa 54 inaonyesha kwamba Desemba 21, 2006, TANESCO waliridhia uhamishwaji wa mkataba wa Richmond kwenda Dowans, hali ambayo iliiwezesha kampuni hiyo ya Costa Rica kuanza kuzalisha umeme wa awali wa megawati 20 kuanzia Januari 26, 2007.