Dk. Slaa kugombea urais
*Kamati Kuu Chadema yampitisha rasmi
*Ndoa yake yazua mjadala katika vikao
*Ategemea udini wa Wakatoliki kushinda
*Viti Maalumu navyo vyawaletea kasheshe
HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemteua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilibrod Slaa, kuwa mgombea urais wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31.
Dk. Slaa alichaguliwa jana na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, Chadema sasa itakuwa na kazi ngumu kumpata mtu makini
atakayekiwakilisha chama hicho katika Jimbo la Karatu, lililokuwa likiongozwa na Dk. Slaa kwa awamu tatu.
Taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa, uteuzi wa Dk. Slaa ulitawaliwa na mvutano mkali baada ya yeye kutotaka nafasi hiyo, huku akitoa sababu kuu mbili.
Kabla mwanasiasa huyo kupitishwa, mwingine aliyekuwa amependekezwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesigwa Baregu, ambaye hakupitishwa. Baregu mwaka 2005 aliwatosa Chadema saa ya mwisho baada ya kukataa kuchukua fomu, ikabidi Mbowe ndiye ajitose.
Sababu ya kwanza iliyotajwa na Dk. Slaa alipokuwa akipinga kuwania nafasi hiyo, alisema hajafunga ndoa na mkewe, Rose Kamili, kwa kuwa alikosa sifa baada ya kujiondoa katika nafasi ya uongozi wa kiroho wa Kanisa Katoliki miaka mingi iliyopita.
Sababu nyingine iliyotajwa na Dk. Slaa kama kinga yake ya kumnusuru kuwania nafasi hiyo ni kitendo cha mkewe kuwania ubunge katika Jimbo la Hanang kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na sababu hizo, Dk. Slaa aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa iwapo atakiwakilisha chama katika nafasi hiyo muhimu, jamii haitamwelewa tofauti na chama kinavyofikiria.
"Mwanzoni kulikuwa na mvutano, Dk. alikataa katakata, alijieleza sana, lakini mwishowe wajumbe walimtoa hofu, wakamwambia anazo sifa za kugombea, asiwe na hofu.
"Wajumbe walimwambia kuwa, kama ni suala la ndoa, Katiba haisemi mahali popote kwamba, mgombea urais lazima awe amefunga ndoa.
"Baada ya hoja hizo na nyinginezo, hatimaye akalainika, akakubali kukiwakilisha chama na sasa anasubiri baraka za Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa chama," kilisema chanzo chetu.
Habari za ndani zilisema Dk. Slaa aliingia makubaliano yasiyo rasmi na baadhi ya maaskofu Katoliki alikokuwa kifanya kazi kwenye Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na anategemea kutumia ukaribu wake na maaskofu hao kupigiwa ndogo ndogo aingie Ikulu.
Mbali na mvutano huo, chanzo hicho kilisema mvutano mwingine ulioonekana kutikisa kikao ulikuwa katika hoja ya namna ya kuwapata wabunge wa Viti Maalumu wa chama hicho.
Katika kikao hicho, inasemekana baadhi ya wajumbe walitaka wajumbe wa mkutano unaowachagua wabunge wa Viti Maalum, wajigharamie nauli kutoka mikoani, wakati wajumbe wengine walitaka chama kiwagharamie wajumbe hao kwa kuwa kimekuwa kikiwagharamia wajumbe wa vikao vingine.
"Baada ya mvutano katika nafasi ya urais, shughuli nyingine ilikuwa kwa wabunge wa Viti Maalumu, kwani baadhi walitaka wajumbe hao wajigharamie na wengine walitaka chama kiwajibike kwao.
"Baadhi walisema iwapo wajumbe watajigharamia, wagombea na na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo watashindwa kuhudhuria kutokana na kutokuwa na fedha, jambo ambalo litawapa nafasi wabunge waliokuwa madarakani kushinda kwa urahisi kwa sababu wao wana fedha.
"Mvutano haukuishia hapo, wajumbe wengine walitaka wabunge wa viti maalumu waliomaliza muda wao, wasiruhusiwe kugombea ili kutoa nafasi kwa wengine ili nao wapate uzoefu kisiasa pamoja na fedha kama walivyo wenzao waliomaliza muda wao.
"Pamoja na hayo, wajumbe walitaka chama kitakapopeleka majina ya wagombea wa nafasi hizo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yapelekwe kwa kufuata uwiano wa kikanda ili kuepuka wabunge hao kutoka kanda moja kama ilivyo sasa," kilisema chanzo chetu.
Dk Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, walipopigiwa simu kwa nyakati tofauti ili kuzungumzia mkutano huo, hawakupokea simu zao.
MTANZANIA ilimwandikia ujumbe mfupi Dk. Slaa uliosema hivi: "Dk. Shikamoo. Hongera nakupigia hupokei… Nimeambiwa maaskofu Katoliki wamebariki uteuzi wako. Tunakwenda mitamboni na ndo habari yetu. Pia na suala la kutofunga ndoa na mvutano wa Viti Maalum uliotokea. Tunaomba maoni yako tuwe balanced. Asante Mhe." Hadi saa tatu usiku alikuwa hajajibu.
Source:
Gazeti Mtanzania