Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa.
Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa, amedai serikali imewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini, kuisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ishinde mwaka huu.
Dk Slaa alitoa madai hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za urais zilizofanyika mjini Moshi jana.
Alisema Chadema ina mtandao ndani ya serikali na katika usalama wa taifa, uliosababisha kupata taarifa na mikakati inayopangwa kwa lengo la kuibeba CCM.
Hapa nina barua ya serikali ya Septemba 19, mwaka huu iliyotumwa kwa ma-DC, RC na wakurugenzi wa halmashauri ambao pia ni wasimamizi wa uchaguzi, zikiwaelekeza kutumia gharama yoyote ili CCM ishinde, alisema.
Aliongeza: mimi ninamwambia Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) kuwa asicheze na amani ya Watanzania, aheshimu utawala wa sheria na demokrasia, alisema.
Alisema Chadema haitakuwa tayari kuona wananchi wakinyanganywa haki yao ya demokrasia, iwapo serikali itatumia nguvu kuwabeba wagomnbea wa CCM. Pia, Dk Slaa alisema haoni sababu ya kupewa ulinzi na askari polisi kwa vile jeshi hilo linachangia kuhujumu kampeni zake.
Alisema polisi wameonekana kuibeba CCM na kutolea mfano tukio la juzi usiku, ambapo askari waliwakimbiza vijana waliokuwa wakipima maeneo ya kutua helikopta, maarufu kama GPS huko Moshi Vijijini.
Alisema helikopta anayoitumia kwa kampeni za urais ilishindwa kufika kwenye maeneo mengi kama ilivyokusudiwa, baada ya polisi kushikilia gari lililokuwa likimpeleka mtaalam wa kupima GPS juzi usiku.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, naapa nitakufa na wewe kama kazi zangu zitakwama
nasikia mnamshikilia dereva pamoja na gari kwa shinikizo la Dk. Cyrill Chami, alisema. Dk Chami ni mgombea ubunge wa Moshi Vijijini kupitia CCM ambaye hata hivyo Dk Slaa hakufafanua zaidi kuhusu ushiriki wake (Chami) katika sakata hilo.
Dk Slaa alihoji, umeleta ulinzi wa polisi hapa kufanya nini. alihoji Dk. Slaa.
Alilitaka jeshi la polisi kuliachia gari hilo na dereva wake ili kazi ya kupima GPS ifanyike kwa ufanisi.
Akisimulia mkasa wa kukimbizwa na polisi, mpimaji wa GPS, Gwakisa Gwakisa, alisema Dk. Chami akiwa na polisi kwenye gari yake binafsi, alianza kuwafuata kuanzia eneo la Uru na kwamba walipomaliza kupima GPS eneo hilo, walielekea Mkoringa lakini Dk Chami aliendelea kuwafuata.
Tukiwa Mkoringa baada ya kumaliza kupima GPS gari ya Chami lilikuja likiwa imewasha taa full, tulivyoona vile na sisi tuliwasha full halafu tukazima, alisema.
Wao wakazidi kuja, tukahisi si watu wazuri tukakimbia,walitufukuza kuanzia Mkoringa hadi Keys hoteli, alisema.
Tukiwa getini tukaona mlinzi anachelewa kufungua ikabidi mimi niruke geti na dereva akaondoa gari, nadhani walikimbizana naye hadi walipomkamata, alisema.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng'hoboko alisema gari la Chadema lililokamatwa limetokana na tuhuma ambazo zimewafikia kituoni hapo.
Ng'hoboko alisema kuwa gari hiyo ilipita katika eneo la Kibosho majira ya saa 8:00 lakini liliposimamishwa, dereva hakusimama. Alisema gari hilo iliyokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hakuweza kufahamika, lilifichwa mafichoni na dereva wake kukimbia.
Alisema kuwa walipofika eneo hilo waliikuta gari hiyo likiwa peke yake na ndipo walipoamua kuichukua na kuiweka kituoni hapo.
Kamanda huyo alisema kuwa tuhuma ambazo wamefikishiwa ni kwamba zinadaiwa kuwa usiku huo, yalitolewa mabango ya Rais Jakaya Kikwete pamoja na mgombea ubunge wa eneo hilo
Alisema kuwa hawajafanya njama zozote za kutaka kukwamisha kampeni za Dk. Slaa kwani mpaka sasa dereva wa gari hilo hajajitokeza.
"Unajua kuna tuhuma ambazo zimetufikia hivyo kuhusiana na suala hilo nitalitolea ufafanuzi kwa waandishi kesho (leo) ila mpaka sasa dereva bado hajajitokeza," alisema.
Habari hii imeandikwa na Restuta James Moshi na Beatrice Shayo, Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE