Junius
JF-Expert Member
- Mar 11, 2009
- 3,181
- 144
Familia ya Mobutu itapata zaidi ya dola milioni sita
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepinga uamuzi wa mahakama moja nchini Uswisi, kwa kuamua akiba ya senti za rais wa zamani wa nchi hiyo, Mobutu Sese Seko, zikabidhiwe familia yake.
Waziri wa habari, Lambert Mende, ameielezea BBC kwamba Uswisi haikujitahidi kadri ya uwezo wake wote kuhakikisha pesa hizo zinarudi tena kwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema nchi yake haiwezi kukata rufaa, kwani utaratibu mzima wa kisheria umefikia tamati.
Zaidi ya dola milioni 6 (pauni milioni 3.7) za Mobutu zinazuiliwa katika akaunti za benk nchini Uswisi.
Familia ya marehemu Mobutu sasa inatarajia kupokea pesa hizo, baada ya mahakama kupinga ombi lililowasilishwa na mwanaharakati mmoja la kutaka fedha hizo ziendelee kuzuiliwa na serikali au zigawiwe mashirka ya misaada.
Siku ya Jumanne, mahakama hiyo ya Uswisi ilikataa ombi la pesa hizo kuendelea kuzuiliwa katika benki, na kuamuru zirudishiwe familia.
Uswisi imekuwa ikizizuia senti hizo, ambazo inasemekana zilipatikana kwa njia isiyo halali.
Kufuatia uamuzi huo Prof Mark Pieth ambaye alikuwa amewasilisha ombi la kutaka pesa hizo ziendelee kuzuiwa katika benki hizo nchini Uswisi, alielezea kusikitishwa na hatua hiyo.
Pesa hizo zimezuiliwa tangu mwaka wa 1997, baada ya kifo cha Mobutu Sese Seko, kufuatia madai kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Congo na familia yake walipata utajiri huo kwa kupora mali ya umma nchini mwao.
Serikali ya Uswisi ilikuwa imeweka muda wa mwisho wa kuzuia pesa hizo hadi mwezi Octoba mwaka huu.
Awali serikali ya Congo ilikuwa inataka pesa hizo zirudishwe mikononi mwake ili zitumike kwa mipango ya maendeleo nchini humo lakini juhudi zake zimeambulia patupu.
Rais Mobutu alitawala Zaire kwa jumla ya miaka 32, kipindi ambacho aliishi maisha ya kifahari huku wananchi wengi wakiishi kwa dhiki.
Alinunua majengo mengi ya kifahari katika nchi za ulaya kando na kuwa na akaunti nyingi katika benki za nchi hizo.
Baada ya serikali yake kupinduliwa na waasi walioongozwa na Laurent Kabila, babake kiongozi wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mobutu pamoja na vibaraka wake walitoroka.
Rais Mobutu alifariki nchini Morocco na hadi leo hakuna anayejua utajiri wake kamili.
SOURCE: BBC(KISWAHILI SERVICE)